Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 14 Mei 2014 13:21

Sura ya An Nur, aya ya 43-47 (Darsa ya 615)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 615 na kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 43 na 44 ambazo zinasema:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يُزْجِي سَحَابًا ثُمَّ يُؤَلِّفُ بَيْنَهُ ثُمَّ يَجْعَلُهُ رُكَامًا فَتَرَى الْوَدْقَ يَخْرُجُ مِنْ خِلالِهِ وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاء مِن جِبَالٍ فِيهَا مِن بَرَدٍ فَيُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاء وَيَصْرِفُهُ عَن مَّن يَشَاء يَكَادُ سَنَا بَرْقِهِ يَذْهَبُ بِالأَبْصَارِ

Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mrundo? Basi utaona mvua ikitokea kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmemetuko wa umeme wake kupofua macho.

يُقَلِّبُ اللَّهُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ إِنَّ فِي ذَلِكَ لَعِبْرَةً لِّأُولِي الأَبْصَارِ

Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hilo yapo mazingatio kwa wenye busara.

Aya hizi zinaashiria jinsi Allah SW anavyouendesha kwa irada yake ulimwengu wa maumbile na kueleza kwamba mzunguko wa usiku na mchana ambao ni matokeo ya harakati iliyoratibiwa na yenye mpangilio na nidhamu maalumu ya sayari ya dunia, mwezi na jua ni kazi inayofanywa na Mwenyezi Mungu, na wala si jambo linalotokea kwa sadfa na bila ya ratiba wala mpangilio. Hivi kweli akili inaweza kukubali kwamba mfumo wenye nidhamu makini, iliyokamilika na ya kustaajabisha kama hii uwe umetokea kwa sadfa tu? Ni sawa kabisa na mfano wa mtu atakayedai kwamba herufi za alfabeti zilizoparaganyika na kuchanganyika pamoja zimeweza zenyewe kutengeneza kitabu cha mashairi yaliyonadhimika na yenye vina na vibwagizo vya kuvutia mno! Je kuna mtu anayeweza kuamini maneno hayo? Si mwendo wa sayari ya dunia tu na kuingia na kutoka usiku na mchana, bali hata mwendo wa mawingu angani pia unafanyika kwa irada na tadbiri ya Allah SW. Uvumaji wa upepo na kukusanyika na kutanda wingu zito linalosababisha kunyesha mvua ya maji na hata wakati mwengine ya mvua ya mawe, japokuwa ni tukio la kimaumbile lakini kunategemea irada na kutaka Yeye Mola, na ndiyo maana baadhi ya wakati mvua hunyesha katika eneo moja na kuacha kunyesha katika eneo jengine. Kinyume na mzunguko wa usiku na mchana ambalo ni jambo thabiti na linaloweza kuhesabika katika kipindi cha mwaka mzima, harakati na mwendo wa mawingu, na kunyesha mvua pamoja na udondokaji wa theluji na mvua ya mawe kunakotokea katika maeneo tofauti ya dunia ni mambo yanayobadilika na si yenye hali thabiti. Kwa hivyo inawezekana katika eneo moja la ardhi ikanyesha mvua kwa wingi kwa muda wa mwaka mmoja au miaka kadhaa, kisha miaka kadhaa inayofuatia, eneo hilohilo likakabiliwa na ukame. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba visababishi vya kimaumbile katika mfumo wa maumbile vinafanya kazi kwa qudra, nguvu na irada ya Allah, na huviendesha kufanya kazi kwa hikima yake  na kwa namna anayoona  Yeye Mola kuwa na ina manufaa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kunyesha kwa mvua, theluji na hata mvua ya mawe kunaweza kuwa na faida na kunaweza kuleta madhara pia, na yote hayo mawili yanategemea irada na kutaka kwa Allah SW.

Ifuatayo sasa ni aya ya 45 ambayo inasema:

وَاللَّهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِن مَّاء فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى أَرْبَعٍ يَخْلُقُ اللَّهُ مَا يَشَاء إِنَّ اللَّهَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Na Mwenyezi Mungu amemuumba kila mnyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu minne. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia jinsi mvua inavyonyesha na usiku na mchana unavyoingia na kutoka, aya hii inaashiria maudhui nyengine kuhusu maisha ya wanyama na anuai zao na kueleza kwamba viumbe hao wote walioko ardhini, angani au majini, wameumbwa kwa tadbiri maalumu ya Mola kutokana na maji. Viumbe wenye uhai wanaumbwa kutokana na tone la maji ya mbegu ya uzazi, na baada ya kuja duniani huwa wanahitajia maji ili waweze kubaki na kuendelea kuishi. Anuai za viumbe vilivyoko ardhini na kuwepo namna kwa namna za wanyama, ambao baadhi yao wameashiriwa katika aya hii, ni ishara ya qudra na uwezo usio na ukomo wa Muumba wa ulimwengu ambaye ameumba aina zote hizi za viumbe mbalimbali na wenye hali tofauti kutokana na maji na udongo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba uumbaji wa viumbe haujafikia mwisho, bali Allah Tabaaraka Wa Taalaa daima yuko katika hali ya uumbaji. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa maji ndio chembe ya asili ya viumbe vyote. Na hii ni alama na ishara ya qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu SW ya kuumba viumbe vyote hivyo vya aina na namna tofauti kutokana na mada hiyo moja tu na ya kawaida. Wa aidha aya hii inatutaka tuelewe kwamba ikiwa mtu hatopiga hatua mbele na kukwea daraja za kimaanawi, upigaji hatua wake kimaada kwa kutembea utakuwa katika hali sawa na viumbe vingine vitambaavyo, na hadhi yake haitokuwa zaidi ya ile ya mnyama.

Darsa ya 615 inahatimishwa na aya za 46 na 47 ambazo zinasema:

لَقَدْ أَنزَلْنَا آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ وَاللَّهُ يَهْدِي مَن يَشَاء إِلَى صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

Hakika tumeteremsha Ishara zinazobainisha. Na Mwenyezi Mungu hummwongoza amtakaye kwenye Njia Iliyonyooka.

وَيَقُولُونَ آمَنَّا بِاللَّهِ وَبِالرَّسُولِ وَأَطَعْنَا ثُمَّ يَتَوَلَّى فَرِيقٌ مِّنْهُم مِّن بَعْدِ ذَلِكَ وَمَا أُوْلَئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ

Na wanasema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume, na tumet'ii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala hao si wenye kuamini.

Baada ya aya zilizopita kubainisha ishara za uwezo wa Allah katika mfumo wa uumbaji, aya hizi zinaashiria kuteremshwa kwa wahyi katika mfumo wa uwekaji sheria zake Mola kwa ajili ya kuwaongoza watu kuelekea kwenye saada na uongofu na kueleza kwamba aya za kitabu cha mbinguni zinawaangazia na kuwaita watu kwenye njia sahihi na iliyonyooka ya maisha ambayo ni ya kujiweka mbali na kila aina ya mkengeuko na upindukiaji mpaka. Ni njia ambayo Allah SW amemtandikia mwanadamu ili kuweza kufikia kwenye lengo alilowekewa na akawatuma na Mitume pia na akawapa jukumu la kumwongoza kiumbe huyo katika kuifuata njia hiyo iliyonyooka. Tab'an siku zote yamekuwepo baadhi ya makundi ya watu ambao wanadai kwa sura ya uongo kwamba wao ni wafuasi wa Mitume na wafuataji wa kweli wa njia yao lakini hayo wanayoyadai kwa ndimi zao sio yaliyomo ndani ya nyoyo zao, wala sio yashuhudiwayo katika matendo yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutokana na Mwenyezi Mungu kutuma Mitume na kuteremsha wahyi wa aya zake zenye kubainisha na kuweka wazi kila kitu amewafungulia njia waja wake ya kuufikia uongofu na vilevile ameondoa dhima juu yao ya kutokuwa na kisingizio cha kuja kusema hatukufuata uongofu kwa kuwa haukutufikia. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa unafiki ni hatari inayozikabili jamii za Kiislamu na yenye kuziletea madhara. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hizi kwamba tusiwe watu wa kuamini mambo haraka na wala tusitekwe na sha'ar za maneno matamu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 615 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azisafishe nyoyo zetu na kila maradhi machafu ya kiroho yakiwemo ya unafiki. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)