Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 14 Mei 2014 13:06

Sura ya An Nur, aya ya 39-42 (Darsa ya 614)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 614 na kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 39 na 40 ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَعْمَالُهُمْ كَسَرَابٍ بِقِيعَةٍ يَحْسَبُهُ الظَّمْآنُ مَاءً حَتَّى إِذَا جَاءَهُ لَمْ يَجِدْهُ شَيْئًا وَوَجَدَ اللَّهَ عِندَهُ فَوَفَّاهُ حِسَابَهُ وَاللَّهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ

Na waliokufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) jangwani. Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.

أَوْ كَظُلُمَاتٍ فِي بَحْرٍ لُّجِّيٍّ يَغْشَاهُ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ سَحَابٌ ظُلُمَاتٌ بَعْضُهَا فَوْقَ بَعْضٍ إِذَا أَخْرَجَ يَدَهُ لَمْ يَكَدْ يَرَاهَا وَمَن لَّمْ يَجْعَلِ اللَّهُ لَهُ نُورًا فَمَا لَهُ مِن نُّورٍ

Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyofunikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru, basi hawi na nuru.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia uongofu wa Allah na wale walioongolewa kwa kufuata uongofu huo ambao hapa duniani watakuwa na saada katika maisha yao, na huko akhera watapata jaza na malipo makubwa ya thawabu. Baada ya maelezo hayo aya tulizosoma zinalinganisha hali ya makafiri na ya waumini na kueleza kwamba badala ya maji, makafiri wanafuata sarabi na mazigazi, na hatimaye wanaishia kufa kwa kiu, hali ya kuwa waumini wameiendea chemchemi safi ya uongofu ambayo maji yake yanazipoza na kuzitosheleza nyoyo zao. Waumini, wao daima wamo katika hali ya kupokea na kunufaika na nuru ya uongofu itokayo kwa Mola wao ambayo ni "nurun alaa nuur", yaani nuru juu ya nuru nyengine; lakini makafiri, wao wanazama na kuzama zaidi kwenye lindi la giza totoro na kutingwa na "dhulumaatun baadhuha fauqa baadh", yaani viza juu ya viza vingine.

Katika aya hizi Mwenyezi Mungu Tabaaraka Wa Taala amepiga mifano miwili katika kueleza hali ya makafiri. Mmoja ni wa mtu mwenye kiu ambaye yuko kwenye jangwa kavu, anahaha kuyafuata maji lakini hawezi kuyafikia, na mfano mwengine ni wa mtu aliyetingwa na giza totoro akiwa ameghariki kwenye bahari ya kina kikubwa na dhoruba ya mawimbi makali na wala hakuna njia ya kujiokoa. Kinachotoa mguso katika mifano hii ni kwamba mfano wa kwanza ni wa mtu anayekufa kwa kukosa maji na wa pili ni wa yule anayeghariki na kukata roho kutokana na mawimbi makubwa ya maji. Wa kwanza anatekwa na sarabi na mazigazi na kuingia tamaa kwa kuyadhani ni maji baada ya mawingu kutonyesha mvua, na wa pili anaishia kwenye giza totoro kutokana na wingu zito na jeusi linalotanda. Wa kwanza anahadaiwa na nuru na mwanga bandia unaomfanya ayahisi mazigazi kuwa ni maji, na wa pili anasombwa na mafuriko makubwa yanayomhilikisha na kumtoa roho. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba yamkini matendo ya makafiri yakaonekana katika dhahiri yake kuwa yenye kuvutia na kughilibisha, lakini batini yake ni uovu na kiza kitupu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa matendo maovu na yenye kuchukiza ya mtu kafiri ni mithili ya pazia jeusi ambalo limeugubika ujudi na nafsi yake. Kila anachojaribu kufanya kuipinga haki vinazidisha wimbi la giza juu ya mawimbi ya giza yaliyokuwa yamemgubika kabla yake na kumfanya azidi kuzama na kughariki kwenye giza totoro zaidi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba amali njema za makafiri ni sarabi na mazigazi na amali zao mbaya ni viza vitupu. Aidha aya zinatutaka tuelewe kuwa kama haitokuwepo nuru ya imani, nuru ya elimu na akili peke yake haitoshi na hivyo haiwezi kumuokoa mwanadamu.

Aya ya 41 na 42 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ

Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwishajua Sala yake na tasbihi yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wayatendayo.

وَلِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَإِلَى اللَّهِ الْمَصِيرُ

Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya wote.

Baada ya kulinganishwa hali ya waumini na makafiri katika aya zilizopita aya hizi zimeashiria jinsi Allah SW alivyo mkwasi na asivyohitajia ibada na t'aa za wanadamu na kueleza kwamba: Ulimwengu wote wa maumbile, wakiwemo hata ndege warukao angani, wote wanamsabihi Mwenyezi Mungu na wanamdhukuru na kumhimidi Yeye Mola. Kwa mujibu wa maelezo ya Qur'ani, viumbe vyote vya ulimwengu wa maumbile kuanzia vyenye roho mpaka visivyokuwa na roho, vimo katika hali ya kumhimidi na kumsabihi Allah SW. Kwa sababu vina namna fulani ya hisi na ufahamu wa kumtambua Mola wao, na kila mmoja wao na kwa lugha yake anamhimidi Yeye Mola.

Katika aya hizi na aya nyengine kadhaa za Qur'ani, suala la ndege warukao angani limeashiriwa peke yake. Huenda ikawa ni kutokana na maajabu mengi mno yaliyopo katika maumbile ya viumbe hao na ambayo ni ishara na alama za wazi kabisa za tauhidi yaani kuwepo Mola mmoja tu wa haki asiye na mshirika. Ndege wapenzi wasikilizaji, wanaruka na kupaa angani kwa namna ya ajabu inayowawezesha kuizuia nguvu ya mvutano isiwavute chini. Wakati viumbe hao wanapotaka kutafuta punje na chakula chao hutoka kwenye viota vyao, na pasina kuwepo mwongozo wowote wa alama na njia huko angani huweza kuvitambua viota vyao vilipo na kurejea moja kwa moja kwenye viota hivyo bila ya kupotea baada ya mahangaiko yao marefu ya kujitafutia riziki.

Katika aya hizi mbali na kumsabihi Mwenyezi Mungu imeashiriwa pia sala ya viumbe kwa ujumla pamoja na ndege. Na hilo limeelezwa kwamba linafanyika kwa uelewa unaodhihirisha hisia na ufahamu wa hali ya juu na unyenyekevu wao mbele ya Muumba wa ulimwengu. Hakika ya mambo ni kuwa ni jambo lililoko nje ya uwezo wa mwanadamu wa kawaida kufahamu hamdu na tasbihi wanazoleta viumbe mbalimbali kumtukuza na kumuadhimisha Mola wao Muumba. Ni Mitume na mawalii wa Allah tu ndio wanaoweza kulidiriki hilo kwa njia za ushuhudiaji wa kinyoyo na wa ndani ya nafsi. Ni kama inavyoeleza bayana aya ya 44 ya Suratul Israa ya kwamba: Na hapana kitu ila kinamsabihi kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kusabihi kwake.

Lakini pia baadhi ya watu wanaitakidi kwamba kusabihi kunakofanywa na viumbe wakiwemo ndege ni kwa hali ya kimaumbile tu, yaani nafsi za viumbe hao, zenyewe zinathibitisha utakasifu wa Allah SW wa kutokuwa na chembe ya kasoro wala kuwa na mshirika yoyote. Lakini dhahiri ya aya hizi inathibitisha kinyume chake. Na hasa baada ya aya kuashiria kusabihi kunakofanywa na viumbe zinasisitiza pia kwamba jambo hilo linafanywa na viumbe hao kwa ujuzi na uelewa na wala hawaleti tasbihi hizo bila ya kujifahamu na bila ya kutaka. Aya hizi kwa hakika ni indhari kwa mwanadamu kwamba ikiwa viumbe vingine vyote vya mbinguni na ardhini vimo katika hali ya kumsabihi Allah SW, kwa nini yeye mwanadamu ameghafilika na anaacha kumdhukuru na kumsabihi Mola wake? Yeye anazishuhudia ishara na alama za kuonyesha adhama ya Muumba wake mbinguni na ardhini lakini anashindwa kufungua kinywa chake na kutikisa ulimi wake kumhimidi na kumshukuru Allah kwa chungu ya neema alizomjaalia na anakataa pia kutii na kutekeleza maamrisho yake Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba viumbe vyote vinazo hisi; na kusali kwao na kumsabihi kwao Mola kunafanyika kwa uelewa. Kwa hivyo tusividhanie viumbe hivyo ni vitu visivyo na hisi na sisi kujikweza na kujitukuza zaidi yao. Funzo jengine tunalopata katika aya hizi ni kuwa sala na dua huwa na thamani zinapotekelezwa kwa elimu na uelewa kwa mtu mwenye kusali kutambua ni nini anachosema na nini anachokifanya. Na aidha aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba mfumo wa ulimwengu wa maumbile una mwendeshaji wake na una lengo maalumu ulilowekewa; na mbingu, ardhi na vyote vilivyomo ndani yao vimo katika harakati ya kuelekea kwenye lengo hilo. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wasioghafilika na kumdhukuru na kumsabihi Yeye Mola, na wanaofanya hivyo kwa ujuzi na uelewa. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)