Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 14 Mei 2014 13:01

Sura ya An Nur, aya ya 35-38 (Darsa ya 613)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 613 na kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 35 ambayo inasema:

اللَّهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ مَثَلُ نُورِهِ كَمِشْكَاةٍ فِيهَا مِصْبَاحٌ الْمِصْبَاحُ فِي زُجَاجَةٍ الزُّجَاجَةُ كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّيٌّ يُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ مُّبَارَكَةٍ زَيْتُونَةٍ لّا شَرْقِيَّةٍ وَلا غَرْبِيَّةٍ يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِيءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ نُّورٌ عَلَى نُورٍ يَهْدِي اللَّهُ لِنُورِهِ مَن يَشَاء وَيَضْرِبُ اللَّهُ الأَمْثَالَ لِلنَّاسِ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa hiyo imo katika tungi. Tungi hilo ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotokana na mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.

Aya hii ambayo ni maarufu kwa jina la Ayatun Nur na ambayo kwa sababu yake sura hii imepewa jina la Suratun Nur, inamuarifisha Mwenyezi Mungu jalla fii ulaah kuwa ni chemchemu na asili ya ulimwengu wa maumbile na mwangaziaji na mpaji nuru na mwangaza kwa ulimwengu wa viumbe. Katika aya hii, Allah SW amefananishwa na nuru. Kama tujuavyo, katika vitu na masuala ya kimaada ambayo mwanadamu anayaelewa na anao uwezo wa kuyadiriki, nuru ndicho kitu nadhifu zaidi na ndiyo chemchemi ya vitu vyote jamili na vyenye kupendeza. Nuru ni chimbuko la mambo yote ya kheri, na wala shari na madhara haviwezi kupatikana ndani yake. Uhai na ubakiaji wa mimea, wanyama na watu unategemea nuru ya jua, na bila ya kuwepo nuru, maisha hayawezi kuwa na maana yoyote. Nuru, yenyewe ni mwanga, na pia inaviangazia vitu vingine na hivyo ni sababu ya kuwa na mwanga vitu hivyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu ni nuru, mtoaji nuru na pia ndiye sababu ya kuwepo na kudhihirika ulimwengu mzima wa maumbile na vyote vilivyomo ndani yake. Allah SW ni Muumba wa ulimwengu, na kuendelea kudumu na kuwepo kwa ulimwengu huo na viumbe vyake vyote kunamtegemea Yeye Muumba wao ambaye pia ndiye anayeziendesha na kuziongoza mbingu na ardhi pamoja na mahuluku wote. Ni kama inavyoeleza aya ya 50 ya Suratu Taha ya kwamba:  aliye kipa kila kitu umbo lake, kisha akakiongoza. Kisha Ayatun Nur inaendelea kwa kuufananisha uongofu na mwongozo wa Mwenyezi Mungu Tabaaraka Wata'alaa na taa yenye mwangaza mkubwa ambayo inaangazia nuru yake ndani ya kila nyumba na kuwaondolea giza watu wa nyumba hiyo. Na taa hiyo basi huweko katika mahala mwafaka kabisa, na kutokana na kuzungushiwa chemni huwa salama na hatari ya kuzimika, na imetiwa ndani yake mafuta safi na halisi. Ni wazi kwamba taa ya aina hiyo huwa na nuru na mwanga mkubwa, hutoa nuru na mwangaza wake muda wote na wala mwanga wake haufifii wala hauzimiki abadani. Naam! Uongofu utokao kwa Allah ambao huwafikia wanadamu kupitia wahyi, vitabu vya mbinguni na Mitume wake na kujaa ndani ya nyoyo za waumini huwaangazia waumini hao muda wote na kuwatoa kwenye giza totoro la dhulma na ujahili kama inavyoeleza Qur'ani kwamba Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ulimwengu wa maumbile ni mwanga wa nuru ya Allah ambayo imejidhihirisha katika ulimwengu wa kimaada. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa uongofu wa Mwenyezi Mungu unaziongoza mbingu na ardhi kuelekea kwenye makusudio maalumu na pia unamuelekeza mwanadamu kwenye ukamilifu anaotakiwa kuufikia. Kadhalika aya hii inatuelimisha kwamba imani ya kweli inajengeka kwa uongofu unaomuelekeza mtu kwenye njia iliyonyooka na isiyokengeukia kwenye upotofu wa aina yoyote, uwe wa mashariki au wa magharibi.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 36 ambayo inasema:

فِي بُيُوتٍ أَذِنَ اللَّهُ أَن تُرْفَعَ وَيُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ يُسَبِّحُ لَهُ فِيهَا بِالْغُدُوِّ وَالآصَالِ

Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameruhusu ziinuliwe, na kutajwa humo jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni.

Aya iliyotangulia imemalizia kwa kubainisha nuru na uongofu utokao kwa Allah SW. Amma aya hii ya 36 inasema, hapa ardhini, taa ya uongofu wa Mola huwaka ndani ya nyumba na kuwaangazia watu waliomo ndani ya nyumba hizo ambao ni waswalihina, wasimamishao Sala na wenye kumdhukuru na kumkumbuka Allah. Ni nyumba ambazo Yeye Mola Azza wa Jalla amezitukuza na kuziinua daraja zao kuliko nyumba nyinginezo na ambazo zinapasa ziwe na hadhi na daraja ya juu mbele ya waumini. Hakuna shaka kuwa Nyumba Tukufu ya Al Kaaba iliyoko huko Makka pamoja na misikiti yote na mwahala mutakatifu mwa dini tukufu ya Uislamu katika kila pembe ya dunia vina sifa hizo na kwa hivyo watu wanapaswa kwenda mwahala humo kwa ajili ya kupata uongofu wa Mola. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba misikiti inapasa iwe na upambanuzi na hali bora na tukufu zaidi kwa kila namna kulinganisha na nyumba na majengo mengineyo. Funzo jengine tunalopata katika aya hii ni kuwa nyumba yoyote ambayo ndani yake linadhukuriwa na kutajwa jina tukufu la Allah hupata thamani na utukufu unaoipambanua na kuitafautisha na nyumba nyenginezo.

Darsa yetu ya 613 inahatimishwa na aya za 37 na 38 ambazo zinasema:

رِجَالٌ لّا تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلا بَيْعٌ عَن ذِكْرِ اللَّهِ وَإِقَامِ الصَّلاةِ وَإِيتَاء الزَّكَاةِ يَخَافُونَ يَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالأَبْصَارُ

Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kusimamisha Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.

لِيَجْزِيَهُمُ اللَّهُ أَحْسَنَ مَا عَمِلُوا وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ وَاللَّهُ يَرْزُقُ مَن يَشَاء بِغَيْرِ حِسَابٍ

Ili Mwenyezi Mungu awalipe bora ya yale waliyoyatenda, na awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

Wanaume na wanawake waumini ambao wananufaika na uongofu wa Allah wanajishughulisha na kufanya kazi zikiwemo za biashara ili kujipatia pato la kuwawezesha kukidhi mahitaji yao ya kimaada na ya kidunia, lakini pamoja na hayo kazi na mashughuliko hayo ya kidunia hayawazuii na kuwakosesha kutekeleza wajibu na majukumu yao ya kidini, na muda wote huwa wanafikiria nini itakuwa hatima ya amali zao, kwa sababu huwa wanatambua kwa yakini kwamba lazima watasimama mbele ya mahakama ya Siku ya Kiyama na kuwajibika kwa amali zao na yote waliyoyafanya hapa duniani. Na jambo hili ni sababu kubwa inayowafanya waumini wajiepushe na maasi na mambo maovu na kuwashajiisha kufanya mambo mema na ya kheri. Bila ya shaka Allah SW anawafanyia fadhila, na kuamiliana nao kwa rehema waja wake wema; na kwa upande wa wabaya na waovu, anaamiliana nao kwa uadilifu. Kwa hivyo kwa tendo jema moja afanyalo mja wake humpa thawabu na malipo mara kadhaa hata kufikia mara mia saba, lakini kwa baya moja alifanyalo mja humlipa malipo ya adhabu sawa na kiwango cha tendo hilo baya la dhambi. Uraufu, fadhila na rehma za Allah kwa waja wake wema ni kwamba anazipokea amali zao na upungufu zilionao na badala yake anawapa thawabu na malipo kamili kwa amali zao hizo. Lakini mbali na hayo ni kwamba riziki na malipo atakayowapa waja hao wema huko Akhera ni makubwa mno na ya zaidi ya matarajio anayoweza kuwa nayo mtu au yanayoweza kufikirika na kutasawarika katika hisabu za watu hapa duniani. Kwa mujibu wa hadithi, sifa za waja wazuri na wa kweli wa Allah ni kwamba wakati wanaposikia sauti ya adhana huacha kazi walizonazo mikononi mwao na kwenda kutekeleza nguzo ya Sala. Na wakati wanapokuwemo ndani ya Sala huwa hawashughulishwi na kitu chochote kile ghairi ya ibada hiyo tukufu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kuwa mali na utajiri na masuala ya kimaada vina mvuto kiasi ambacho kama mtu hatokuwa makini anaweza kughafilika na kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa biashara inayoambatana na kumdhukuru na kumkumbuka Allah, kusali na kutoa Zaka ndio yenye thamani. Waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu wanafanya juhudi kwa ajili ya maisha yao ya kimaada, lakini wakati huohuo hawagahfiliki na Akhera. Kwa maneno mengine ni kwamba biashara na uchumi unaomweka kando Allah hauna maana wala thamani yoyote na ni sababu pia ya kuporomoka mtu. Kwa hakika ni utajo wa Allah na Sala ndivyo vinavyoitia baraka biashara na kuieletea ustawi jamii. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa Siku ya Kiyama kila kitu kitabadilika. Vile ambavyo hapa duniani vilikuwa vikionekana kung'ara na kuvutia vitakuwa duni na visivyo na thamani huko Akhera, na vile vilivyokuwa vikidharauliwa ndivyo vitakavyokuwa na maana. Na vilevile aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba watu wanaosamehe kupata faida na tijara katika biashara zao kwa ajili ya Allah watapata faida isiyohesabika ukubwa wake kwa Yeye Mola aliyetukuka. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 613 inaishia hapa. Tunamwomba Allah asikufanye kuhangaikia kwetu maisha ya dunia, kuwe sababu ya kughafilika na Akhera. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)