Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 14 Mei 2014 12:38

Sura ya An Nur, aya ya 32-34 (Darsa ya 612)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 612 ambapo kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 32 ambayo inasema:

وَأَنكِحُوا الأَيَامَى مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ إِن يَكُونُوا فُقَرَاء يُغْنِهِمُ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ وَاللَّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ

Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatosheleza katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.

Katika aya tulizosoma kwenye darsa iliyopita, tuliona kuwa ili kulinda heshima na staha katika jamii, lilizungumziwa suala la kudhibiti macho katika mahusiano ya kijamii na kuwataka waumini wanaume na wanawake wachunge suala la usafi wa maadili na haya katika utizamaji wao, uzungumzaji wao pamoja na mwenendo wao. Baada ya hayo, aya hii ya 32 inagusia suala la ndoa ambayo ina nafasi ya msingi kabisa katika uzima na usafi wa jamii ili kuweza kutakasika na maovu ya kiakhlaqi. Mahitaji ya kijinsia ni miongoni mwa ghariza ambazo Allah SW amewajaalia wanadamu kuwa nazo ili kizazi chao kiweze kuendelea kubaki katika sayari hii ya dunia. Na ndoa, ndio njia halali na ya kimaumbile aliyowawekea wanadamu kwa ajili ya kukidhi ghariza na matamanio yao hayo ya kijinsia. Kinyume na mitazamo ya baadhi ya viongozi wa Kanisa katika Ukristo ambao wanazichukulia ghariza na matamanio ya kijinsia kuwa ni shahawa za kishetani na kulifanya suala la kuoa kuwa ni kitu kisichopendeza na chenye kuchukiza, na hivyo kuwazuia makasisi na watawa wao wasifunge ndoa, Uislamu unaielezea ndoa kuwa ni jambo zuri na linalopasa kufanywa. Kwa kuzingatia kuwa kikawaida udhuru wanaokuwa nao watu wengi na kuwafanya washindwe kufunga ndoa ni tatizo la umasikini na kutokuwa na uwezo wa kifedha, Qur'ani tukufu imelizingatia na kulipa umuhimu maalumu suala hilo. Hivyo inawausia wazazi wa wasichana na wavulana kuwapa wake na waume watoto wao wanapofikia umri wa kufunga ndoa, na kutokuwa na hofu ya dhiki watakayokuwa nayo wakati wa kuanza maisha yao ya ndoa na hivyo kuwa sababu ya kuchelewesha kuwaozesha kwa kisingizio hicho. Kwa upande mwengine watumishi wanaume na wanawake waliomo ndani ya nyumba za watu, nao pia wana ghariza na matamanio ya kijinsia, hivyo kama hawatofikiriwa wanaweza kujisababishia matatizo wao wenyewe au kwa watu wa nyumba wanazoishi. Kwa hivyo Allah SW anawausia wazee wa nyumba hizo wafikirie pia suala la watu wa kama hao na kutoghafilika na mahitaji yao hayo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba viongozi wa utawala wa Kiislamu wanatakiwa waandae mazingira na suhula za kuwawezesha vijana kufunga ndoa ili kuzuia kufanyika maasi ya kijinsia na kuweza kupambana na ufuska na ufisadi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ndoa katika Uislamu ni jambo tukufu na lenye kutiliwa mkazo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa atawawepesishia maisha yao watu wanaofunga ndoa, na ataifanya ndoa yao kuwa sababu ya kupata ukunjufu wa riziki na kumiminikiwa na baraka pia. Kwa hivyo ufakiri usiwe kizuizi cha kumfanya mtu asioe.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 33 ambayo inasema:

وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لا يَجِدُونَ نِكَاحًا حَتَّى يُغْنِيَهُمْ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ وَالَّذِينَ يَبْتَغُونَ الْكِتَابَ مِمَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ فَكَاتِبُوهُمْ إِنْ عَلِمْتُمْ فِيهِمْ خَيْرًا وَآتُوهُم مِّن مَّالِ اللَّهِ الَّذِي آتَاكُمْ وَلا تُكْرِهُوا فَتَيَاتِكُمْ عَلَى الْبِغَاء إِنْ أَرَدْنَ تَحَصُّنًا لِّتَبْتَغُوا عَرَضَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَن يُكْرِههُّنَّ فَإِنَّ اللَّهَ مِن بَعْدِ إِكْرَاهِهِنَّ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatosheleze katika fadhila zake. Na wanaotaka kuandikiwa uhuru katika wale ambao imewamiliki mikono yenu ya kuume, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyokupeni. Wala msiwalazimishe wajakazi wenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakayewalazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko (atawasamehe), kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Aya hii ya 33 inaendeleza maudhui iliyoashiriwa katika aya iliyopita na kueleza kwamba, kama mtakuwa mmefanya jitihada kadiri ya uwezo wenu lakini ikashindikana kutayarisha mazingira ya kukuwezesheni kuoa, jambo hilo haliwezi kuwa kisingizio cha kufanya madhambi na kughariki kwenye lindi la maingiliano machafu ya kijinsia, kwa sababu Mwenyezi Mungu aliyemjaalia mwanadamu kuwa na ghariza za kijinsia ndiye huyo huyo aliyempa uwezo wa kustahamili na kuzidhibiti ghariza na matamanio hayo. Na tofauti baina ya mwanadamu na mnyama iko hapo; yaani wakati mnyama mwenye njaa anapokifikia chakula huwa hawezi kuidhibiti nafsi yake na hulazimika kula chakula hicho kwa kusukumwa na ghariza zake. Lakini mwanadamu, ambaye naye pia amejaaliwa kuwa na ghariza hizo na haja ya kula chakula huweza kuidhibiti nafsi yake hata anapokuwa ameshikwa na njaa au kiu kali kiasi gani! Kama ambavyo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani watu wanaofunga huvumilia kukaa na njaa na kiu kwa masaa chungu nzima. Ghariza za kijinsia nazo haziwezi kumlazimisha mtu kwa sura mutlaki afanye madhambi, kama ambavyo wakati Nabii Yusuf (AS) alipoitwa na Zuleikha, japokuwa alikuwa kijana na alikuwa na ghariza na matamanio hayo, na licha ya kwamba alikuwa mtumwa wa Zuleikha na hivyo ilikuwa wajibu kwake kutii amri yake, lakini aliukwepa mtego wa Zuleikha na kukimbilia kwa Mwenyezi Mungu kuomba amlinde na fitna hiyo. Na Yeye Mola Mtukufu akamfungulia milango iliyokuwa imefungwa, na kutokana na kuchunga staha yake na usafi wake, akamfikisha kwenye kilele cha izza, mamlaka na utukufu.

Kisha aya inaendelea kwa kuwaelekea watu wenye watumwa na wajakazi majumbani mwao na kuwapa maagizo mawili: La kwanza ni kwamba ikiwa kukomboka na utumwa na kuwa huru watu hao kuna manufaa kwao na wanao ustahiki na uwezo wa kujiendeshea maisha yao, basi wasaidieni kuwapa uhuru wao na wagaieni pia katika mali zenu ili waweze kuwa na maisha ya kujitegemea wao wenyewe. Ama agizo la pili ni kwamba msiwafanye wajakazi wenu wenzo na chombo cha kujipatia pato na wala msiwalazimishe kuzini kwani kitendo hicho kitakufanyeni mpate adhabu kali, hata kama wao watapata msamaha wa Mwenyezi Mungu kutokana na kufanya tendo hilo kwa kulazimishwa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba watu wasio na wake au wake zao wako mbali nao, hawana ruhusa ya kufanya dhambi chafu ya zina. Bali wawe na subira, wazichunge staha zao na kuzidhibiti nafsi zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa siku zote tuchukue hatua zenye manufaa kwa waliochini yetu ili waweze kupata kheri na neema kutokana na sisi. Na si kuwalazimisha wao kufanya mambo ambayo si wajibu wao ili sisi tuweze kupata faida na manufaa. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba sheria za Kiislamu zimekuwa zikilenga kuwakomboa na kuwarejeshea watumwa uhuru wao. Miongoni mwao ni sheria ya mkataba wa kujinunua tena hatua kwa hatua watumwa ili kuweza kujikomboa. Na aidha tunajifunza kutokana na aya hii kuwa haijuzu kulimbikiza mali na utajiri kwa njia zisizo halali.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 34 ambayo inasema:

وَلَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ وَمَثَلا مِّنَ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُمْ وَمَوْعِظَةً لِّلْمُتَّقِينَ

Na hakika tumekuteremshieni Aya zinazobainisha na mifano kutokana na waliotangulia kabla yenu na mawaidha kwa wachamngu.

Katika sehemu hii ya mwisho ya aya hizi za Suratun Nur Allah SW anasema: Tumeziteremsha aya ambazo zinakufafanulieni kwa uwazi kabisa njia ya maisha, na zinazokubainishieni pia yale yaliyojiri katika historia ya waliotangulia, ili mpate ibra na mafunzo kutokana na tajiriba ya watu hao. Tab'an ni wale wenye taqwa na wamchao Mwenyezi Mungu tu ndio wanaosikiliza na kuyakubali mawaidha ya Qur'ani; amma wengineo huwa hayawafaidishi chochote mawaidha hayo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Qur'ani ni kitabu cha nuru na mwangaza ambacho kinamuaidhi mwanadamu kwa kutumia mifano ya historia. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa hakuna mtu yeyote asiyehitajia kusikiliza nasaha na mawaidha, hata kama ni mtu mwema na mchamungu. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah azijaalie ndoa zetu ziwe ndoa halisi za Kiislamu na azitakase familia na jamii zetu na kila aina ya ufuska na uchafu wa kimaadili. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)