Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 14 Mei 2014 12:27

Sura ya An Nur, aya ya 30-31 (Darsa ya 611)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani, hii ikiwa ni darsa ya 611 ambapo kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 30 ambayo inasema:

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ذَلِكَ أَزْكَى لَهُمْ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ

Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za wanayoyafanya.

Aya hii na ile itakayofuatia zinawaasa waumini wanaume na waumini wanawake kuchunga heshima, haya na staha katika mahusiano yao ya kijamii ili kuepusha kutokea na kuenea upotofu wa kimaadili na kijinsia katika jamii. Ukweli ni kwamba macho ya mwanadamu yana uwezo wa kuona mbali na kumpa uelewa na ufahamu kiumbe huyo wa kutambua kwa upeo wa masafa ya mbali yale yanayojiri katika mpaka huo wa uoni wake. Hata hivyo mwanadamu anapaswa kudhibiti hali yake ya utizamaji mambo, yaani isiwe ni kutazama kila macho yanakogeukia, na kuangalia kila yanachokitaka. Aya hii tuliyosoma inaeleza kiujumla kwamba wanaume waumini ni watu wanaoyadhibiti macho yao na huyafumba inapofika mahala pa kutaka kutazama mambo yasiyompendeza Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa hadithi, miongoni mwa misdaqi na vielelezo muhimu vya aya hii ni mtu kumwangalia mwanamke asiye maharimu yake, ambapo kama mwanamke huyo atakuwa hajajisitiri, huwa haifai kabisa kumtazama, na la kama atakuwa amejisitiri basi kumtazama kwake kuwe ni kwa kiasi cha dharura tu bila kufikia hadi ya kuingiwa na uchu na matamanio. Mbali na kuyadhibiti macho, aya tuliyosoma inawataka waumini wanaume wachunge na kulinda tupu zao pia na mambo yoyote machafu ya matamanio ya kijinsia. Katika jamii zetu za leo mahusiano haramu na yasiyo na mipaka katika maingiliano ya kijinsia yameenea katika sura tofauti baina ya wasichana na wavulana. Suala hili limesababisha kuzuka upotofu wa kijinsia, matatizo mengi ya kifamilia pamoja na magonjwa mbalimbali ya uasherati. Lakini katika mtazamo wa Uislamu uhusiano wa maingiliano ya kijinsia baina ya mwanamme na mwanamke, unajuzu na unakubalika katika sura ya ndoa tu; na nje ya mstari na mpaka huo, uhusiano wa namna nyengine yoyote ile wa kijinsia, na kwa sura yoyote ile huwa ni haramu. Kisha aya inaendelea kwa kuwatahadharisha watu wote na hasa waumini kwamba msidhani kuwa utizamaji wenu umefichika na hauonekani na Mwenyezi Mungu, bali tambueni kuwa si utizamaji tu bali hata nia mlizonazo nyoyoni mwenu katika vile mnavyovitazama anazijua vyema Yeye Mola, kwani ni mjuzi kamili wa dhahiri na batini ya amali zenu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba miongoni mwa masharti ya imani ni mtu muumini kujiepusha na kujiweka mbali na kila aina ya mahusiano machafu, na watu wengine pia kusalimika na utizamaji wake haramu na usiofaa.  Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa utangulizi wa kuwa safi mtu kimaadili ni kuliweka safi kwanza jicho lake kwa kuliepusha na kuangalia watu wasio maharimu zake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ikiwa tutakuwa na imani ya yakini ya kutambua kwamba Allah SW anazijua vyema nia zetu na utizamaji wetu tutayadhibiti zaidi macho yetu na kuyazuia kuangalia yasiyofaa kutizamwa.

Aya ya 31 ndiyo inayotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hiyo inasema:

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلاَّ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ وَلا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلاَّ لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاء بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاء بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَى عَوْرَاتِ النِّسَاء وَلا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ وَتُوبُوا إِلَى اللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَا الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto wadogo ambao hawajajua mambo yaliyokhusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu nyote enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.

Katika aya iliyotangulia Allah SW alitoa amri mbili kwa waumini wanaume. Ya kwanza ni kudhibiti macho yao na ya pili ni kuhifadhi na kulinda tupu zao na matamanio yao. Aya hii pia kwanza kabisa imebainisha amri hizo hizo za Mola kwa waumini wanawake na kisha ikatilia mkazo mambo matatu kwa ajili ya kuwahifadhi na kuwalinda wanawake na kutazamwa na watu wasio tayari kudhibiti shahawa na matamanio yao ya kijinsia. La kwanza ni kuvaa ushungi au mtandio ambao utafunika uzuri na urembo wao wa kimaumbile wa nywele, shingo na kifua. La pili ni kufunika na kuficha mapambo yao kama herini, kidani na bangili mbele ya wanaume wasio maharimu zao, na jambo la tatu ni kutakiwa wanawake waumini wasipige miguu yao chini wakati wanapotembea, wala kutembea kwa namna itakayovuta na kushughulisha hisia za watu wengine. Jambo lililo wazi kabisa ni kwamba namna ya uzungumzaji, mlahaka na uvaaji wa mavazi wa wanawake na wanaume vina taathira kubwa katika suala la usalama wa mahusiano ya kijamii na katika kuchunga staha, haya na heshima katika mazingira ya hadhara. Na ndiyo maana Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa upande mmoja ameuharamisha utizamaji wa matamanio, na kwa upande mwengine amekataza pia kujiremba wanawake hadharani na kudhihirisha mapambo na vitu ambavyo vitachochea ghariza na matamanio ya kijinsia ya wanaume.

Tukiyaangalia kiujumla yale yanayojiri katika dunia yetu ya leo tutaona kuwa kile ambacho ulimwengu wa Magharibi unakinadi na kukitangaza kwamba ni uhuru wa mwanamke, si kitu kingine ila ni uhuru wa mahusiano ya kijinsia na kuwaendesha uchi wanawake, jambo ambalo halijawa na tija nyingine ghairi ya kuwastarehesha zaidi wanaume wenye uchu wa kukidhi matamanio yao ya kijinsia. Hali ya kuwa athari na madhara ya kuwepo mahusiano ya aina hiyo ni wasichana na wanawake kufikwa na anuai za masaibu makubwa na ya kusikitisha yakiwemo ya kubakwa, kutoa mimba na hata kuamua kujiua. Kwa kuzingatia matokeo hasi na yenye madhara ya mahusiano ya kijinsia yasiyo na mipaka wala udhibiti, hebu na tujiulize: uhuru wa maingiliano ya kijinsia unaweza kuwa na maana nyengine ghairi ya kuendelea wanaume tu kuwatumia wanawake katika jamii kama chombo cha kujistareheshea kwa macho yao, masikio yao na migusano yao? Kwa mujibu wa mafundisho ya dini, wanaume na wanawake wasafi na wenye kujistahi huwa wanajistarehesha kwa wake na waume zao tu; na kwa njia hiyo kuifanya jamii iwe ni mahala pa mazingira safi na ya salama yaliyoepukana na kila aina ya mivuto na vivutio vya matamanio ya kijinsia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hakuna tofauti yoyote baina ya mwanamme na mwanamke katika suala la kudhibiti macho na kuchunga staha yake mtu, bali wote wawili na kwa uzito sawa wana wajibu wa kuyachunga na kuyazingatia mambo hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Uislamu haupingi wanawake kujipodoa na kujipamba, bali unawasisitiza hasa wanawake wawe warembo na wajipambe kwa ajili ya waume zao, lakini inachopinga dini hiyo tukufu ni wanawake kujionyesha na kudhihirisha urembo na mapambo yao hayo katika jamii mbele ya wanaume wasio maharimu zao. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba utembeaji wa namna yoyote ile utakaosababisha kudhihirika mapambo yaliyofichika ya mwanamke ni haramu. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hii kuwa hijabu ni vazi la faradhi na wajibu ambalo Mwenyezi Mungu SW ameliamrisha ndani ya Qur'ani na kulibainishia pia mipaka yake. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 611 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kulinda macho yetu, masikio yetu, ndimi zetu na viungo vingine vyetu vyote na yale yaliyoharamishwa. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)