Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 14 Mei 2014 11:37

Sura ya An Nur, aya ya 24-29 (Darsa ya 610)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani, hii ikiwa ni darsa ya 610 ambapo kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 24 na 25 ambazo zinasema:

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyokuwa wakiyatenda.

يَوْمَئِذٍ يُوَفِّيهِمُ اللَّهُ دِينَهُمُ الْحَقَّ وَيَعْلَمُونَ أَنَّ اللَّهَ هُوَ الْحَقُّ الْمُبِينُ

Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawapa sawa sawa malipo yao ya haki, na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki Iliyo Wazi.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoeleza kwamba watu wanaowazulia tuhuma wenzao hapa duniani motoni yatakuwa ndio makaazi yao huko akhera. Baada ya kuelezwa hayo aya hizi tulizosoma zinasema: Katika mahakama ya Siku ya Kiyama si ndimi pekee zitakazoungama dhambi alizofanya mtu lakini kwa irada ya Allah SW viungo vingine vya watu waovu navyo pia vitatamka siku hiyo na kukiri yale viliyoyatenda hapa duniani. Itakuwa ni kama kwamba viungo vya miili ya watu hao viliyarekodi vyenyewe matendo viliyoyafanya hapa duniani na siku hiyo vitayatamka kwa irada ya Mola. Na kutokana na kukiri na kuungama huko ambako kutafanywa na viungo vya watu waovu bila ya wao wenyewe kupenda, mahakama ya uadilifu ya Allah itatoa hukumu kwa watu hao na kuwalipa jaza ya amali zao pasina kuwazidishia au kuwapunguzia adhabu yao. Ni wakati huo ambapo watu waovu watabainikiwa kwa uwazi kabisa na hakika ya yale waliyokuwa wakiyakanusha na kuyakadhibisha au waliyokuwa wameghafilika nayo hapa duniani; lakini kubainikiwa huko hakutowafalia kitu kwani haitokuwepo tena fursa ya kurejea duniani na kufidia kuyafanya yale waliyoyadharau na kuyapuuza. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama mtu hatokuwa na mamlaka juu ya viungo vyake bali si hasha viungo hivyo vikatoa ushahidi dhidi yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa viumbe na vitu vyote vya ulimwengu wa maumbile hata vile visivyokuwa na roho vina aina fulani ya hisi na kuelewa yale yanayojiri kando yao. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba ni Siku ya Kiyama tu ndipo jaza na malipo ya amali njema na mbaya za mwanadamu zitalipwa kwa ukamilifu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 26 ambayo inasema:

الْخَبِيثَاتُ لِلْخَبِيثِينَ وَالْخَبِيثُونَ لِلْخَبِيثَاتِ وَالطَّيِّبَاتُ لِلطَّيِّبِينَ وَالطَّيِّبُونَ لِلطَّيِّبَاتِ أُوْلَئِكَ مُبَرَّؤُونَ مِمَّا يَقُولُونَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ

Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayoyasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.

Aya hii inaashiria kaida na kanuni ya kifitra na ya kimaumbile ambayo inathibitishwa na kutiliwa nguvu na sheria za Allah na kueleza kwamba mwanadamu, kikawaida anapochagua mwenza katika ndoa hutafuta mtu anayelingana naye kifikra na kitabia. Silka ya watu safi huwa ni kutafuta mambo mema na mazuri na kuchanganyika na watu safi, wema na wenye kujistahi. Na kinyume chake ni kwamba watu wachafu na waovu huwatafuta watu wachafu na waovu wenzao. Kwa mujibu wa kanuni za sheria za dini pia Mwenyezi Mungu SW hajaruhusu wanaume wema na wasafi waoe wanawake wachafu na waovu na kujichafua kimaadili, bali wawaache watu hao kama walivyo ila pale kama watatubia na kurejea kwenye njia ya sawa. Ni kitu chenye kutoa mguso kwamba katika aya hii, kigezo muhimu zaidi kilichotajwa katika kuchagua mwenza katika ndoa ni kutilia mkazo suala la kujiweka mbali na uchafu wa kimaadili na kuzingatia usafi wa fikra na matendo. Ni usafi wa kutakasika na uchafu wa shirki na kufru, wa kujitakasa na maneno machafu na yasiyofaa na pia usafi wa kujiepusha na kila tabia na akhlaqi zisizowapendeza na wasizostahiki kuwa nazo watu waumini. Ni wazi ni kuwa rehma na baraka za Allah na riziki safi na ya halali huruzukiwa watu safi na wema kama hao ambao wamefunga ndoa na kuanzisha familia yao juu ya msingi wa usafi, kujiheshimu na kujistahi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mbali na upande wa dhahiri, tujitahidi pia, bali ndio zaidi, kuzingatia masuala ya usafi wa batini zetu kwa kuhakikisha katika masuala yetu ya maisha, uchaguaji mke na mume, marafiki na kadhalika, tunajiepusha na watu waovu na kukurubiana zaidi na watu safi na wema. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kizazi safi kinapatikana kwa kuchagua mke na mume aliye msafi wa maadili; na watu safi na wema wanatakiwa wawe makini na kulipangia ratiba maalumu suala la malezi ya kizazi chao ili kikulie na kuinukia kwenye njia ya maadili sahihi na akhlaqi njema.

Darsa yetu hii inahatimishwa na aya za 27, 28 na 29 ambazo zinasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّى تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَى أَهْلِهَا ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ

Enyi mlioamini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka mwombe ruhusa, na mwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.

فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فِيهَا أَحَدًا فَلا تَدْخُلُوهَا حَتَّى يُؤْذَنَ لَكُمْ وَإِن قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا هُوَ أَزْكَى لَكُمْ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ

Na msipomkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.

لَّيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ مَسْكُونَةٍ فِيهَا مَتَاعٌ لَّكُمْ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا تَكْتُمُونَ

Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisiokaliwa ambazo ndani yake yamo manufaa yenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyadhihirisha na mnayoyaficha.

Aya hizi zinataja baadhi ya maamrisho na mafundisho ya kijamii ya Uislamu katika suala la kuchunga mipaka ya faragha za watu na kueleza kwamba msiingie majumbani mwa watu ghafla ghafla tu na bila ya taarifa. Kwani kufanya hivyo kunakiuka mipaka ya faragha za watu binafsi na za familia na pia ni jambo ambalo haliwiyani na umuhimu wa kuchunga heshima na haya baina ya watu na umuhimu wa suala la usalama wa jamii. Kuwa wazi mlango wa nyumba hakumaanishi kupewa ijaza na ruhusa mtu ya kupita na kuingia ndani bali lazima aombe idhini kwanza ya kufanya hivyo kwa wenye nyumba. Tab'an kwa mtazamo wa adabu za Kiislamu, wenye nyumba hawalazimiki kumruhusu mtu aingie ndani, kwani kama watakuwa hawako katika utayarifu wa kupokea mgeni wanaweza kumkatalia mtu huyo. Kwa sababu nyumbani ni mahala pa mapumziko na pa kupatia utulivu, hivyo si sawa mtu kuwakosesha wenye nyumba haki yao hii. Na ikiwa wenye nyumba watampa mtu ruhusa na idhini ya kuingia ndani basi adabu za Kiislamu zinataka wakati mtu anayekaribishwa aingiapo ndani ya nyumba awatolee salamu wenye nyumba kwa uso wa uchangamfu, upendo na bashasha. Katika aya hizi tulizosoma imesisitizwa kuwa Mwenyezi Mungu anayajua myatendayo na yaliyofichika ndani ya nyoyo zenu. Huenda ikawa ni kwa sababu ya kutaka watu wasiingie ndani ya nyumba za watu kwa nia ya kupeleleza na kukashifu siri za watu; na kama wanakwenda majumbani kwa watu kwa madhumuni ya kuwatembelea wasitake kupeleleza na kudadisi kuhusu yale yanayojiri majumbani humo. Kwa sababu kufanya hivyo kwa namna yoyote ile ni kitendo kiovu na kisicho cha kiakhlaqi, bali baadhi ya wakati kinakuwa hakijuzu na tena ni haramu. Lakini kwa upande wa maeneo ya umma ambayo si makaazi rasmi ya watu kama kwenye maduka na maeneo ya biashara ambayo milango yao huwa wazi kwa ajili ya watu wote wanaoingia na kutoka huko kwa ajili ya haja zao za manunuzi, hukumu yake inakuwa tofauti, na wala si lazima mtu kuomba idhini ya kuingia ndani yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba nyumbani ni mahala pa makaazi, mapumziko na pa kupatia utulivu. Mtu yeyote yule hana haki ya kuwavurugia wenye nyumba raha yao ya kupumzika na kupata utulivu huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa nyumbani ni mahala pa faragha ya binafsi ya watu, hivyo mtu yeyote hana haki ya kuingilia faragha hiyo bila ya idhini na ruhusa ya wenye nyumba. Ikiwa wenye nyumba hawakuturuhusu kuingia ndani tuwakubalie udhuru wao wala tusiwachagize na kuwatafuta muhali. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba kutoa salamu ni katika adabu za Kiislamu za kutekeleza mtu anapokutana na watu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 610 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kuutekeleza Uislamu katika kila kipengele cha maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)