Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 29 Aprili 2014 12:50

Sura ya An Nur, aya ya 21-23 (Darsa ya 609)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani, hii ikiwa ni darsa ya 609 ambapo kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 21 ambayo inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ وَمَن يَتَّبِعْ خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ فَإِنَّهُ يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاء وَالْمُنكَرِ وَلَوْلا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ مَا زَكَا مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ أَبَدًا وَلَكِنَّ اللَّهَ يُزَكِّي مَن يَشَاء وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

Enyi mlioamini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakayefuata nyayo za Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingelitakasika miongoni mwenu kabisa hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

Baada ya kumalizika aya zilizozungumzia uzushi wa tuhuma chafu dhidi ya mmoja wa wake wa Bwana Mtume SAW aya hii ya 21 inaashiria kaida na kanuni jumla kwa kuwahutubu waumini kwamba: jihadharini na shetani, kwa sababu yeye hukuelekezeni hatua kwa hatua kuelekea kwenye upotofu. Istilahi ya "khutuwati shaitaan" kwa maana ya hatua na nyayo za shetani imetajwa mara nne ndani ya Qur'ani tukufu ili kutanabahisha na kutahadharisha juu ya hatari hii kubwa, kwamba shetani humuingiza na kumtumbukiza mtu kwenye lindi la madhambi hatua kwa hatua. Ufanyaji dhambi yoyote ile huitia doa la upotofu fikra na roho ya mtu; na kila anapoikariri dhambi hiyo ndipo mtu hujikuta anatumbukia kwenye dimbwi la ufanyaji madhambi makubwa zaidi na hatimaye kuishia kwenye hilaki.

Qur'ani tukufu imebainisha vigezo na vipimo vya kumuelewesha muumini wasiwasi na vitendo vya shetani ambavyo ni kila amali na matendo machafu na maovu yanayokubalika mbele ya kila mtu mwenye akili timamu na mwenye kuzingatia fitra na maumbile halisi ya kiutu kuwa ni maovu; kama kusaliti, kuzua tuhuma, kuiba, kuua n.k. Tab'an Mwenyezi Mungu, Mola mwenye hekima na huruma amempa mwanadamu nyenzo za nje na za batini yake za kumwezesha kuudhibiti wasiwasi wa nafsi yake na ule unaotokana na shetani. Akili na fitra, yaani maumbile, ni nyenzo za batini na za ndani, na kitabu chake Allah pamoja na Mitume wake ni nyenzo za nje, ambazo zote hizo huwa zinampa indhari mtu kila mara na kumwonyesha njia sahihi ya maisha. Lau kama vyote hivyo visingikuwapo, nafsi na matamanio ya mwanadamu kwa upande wa batini, na wasiwasi wa shetani kwa upande wa nje vingekuwa muda wote vikimsukuma na kumuelekeza kiumbe huyo kwenye matendo maovu na machafu na kuwafanya wanadamu wote watumbukie kwenye lindi la madhambi na ufasiki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba waumini wasitegemee imani zao tu, wasiingiwe na ghururi kwa sababu ya imani hizo na wala wasijichukulie kuwa wameshaokoka kwa kuwa kwao waumini. Kwani mwandamu huwa muda wote anakabiliwa na wasiwasi wa shetani na hatari ya kukengeuka haki na kufuata upotofu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa shetani hujipenyeza ndani ya roho ya mtu taratibu, kidogo kidogo na hatua kwa hatua. Kwa hivyo tujihadhari na njia zake zote anazotumia kujipenyezea na tujichunge nazo kuanzia kwenye hatua yake ya kwanza.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 22 ambayo inasema:

وَلا يَأْتَلِ أُوْلُوا الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَى وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا أَلا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّهُ لَكُمْ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa jamaa zao na masikini na waliohama katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Tumeona jinsi aya zilizotangulia zilivyowakemea na kuwalaumu vikali watu waliomzulia tuhuma chafu mke wa Bwana Mtume, na jinsi Allah SW alivyowakanya vikali Waislamu kwa kosa walilofanya katika kadhia hiyo. Kufuatia kadhia hiyo baadhi ya watu waliokuwa na mali na uwezo walichukua uamuzi wa kutowasaidia kwa namna yoyote ile kifedha na kimali wale waliochangia katika kueneza uvumi wa tuhuma hiyo, hata kama ni jamaa zao au watu walio wanyonge na wahitaji. Kwa sababu hiyo aya hii iliteremshwa na kuwatahadharisha na kufanya jambo hilo. Huenda ikawa ni kwa sababu ya kuonyesha kwamba kuwazuilia misaada ya mali wahitaji, hata kama watakuwa wamefanya makosa si njia sahihi ya kuwaadibisha. Bali inapasa waendelee kusaidiwa na kuendeleza mahusiano ya kijamii na wao kwa namna ambayo itawafanya waelewe kosa lao na hivyo kusamehewa na jamii ya Kiislamu. Kisha aya inaashiria nukta moja muhimu kwa kuwahoji watu hao kwamba kwani nyinyi wenyewe hadi sasa hamjawahi kufanya makosa? Na kama mmefanya, mnatarajia nini kwa Mwenyezi Mungu? Mnatarajia kupewa fursa na muhula wa kutubia na kurejea kwake Yeye Mola au kuharakishiwa adhabu na ikabu yake? Ikiwa mnatarajia kupata msamaha wa Mola, basi na nyinyi pia wasameheni waja wenzenu waliofanya makosa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mtu anayesamehe makosa ya wenzake na akawa tayari pia kuwasaidia kwa mali yake basi na yeye atapata msamaha wa Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa haifai kuchukua hatua kali mno na za kufurutu mpaka kwa watu wanaofanya makosa na kuamua kuwafungia njia zote za kupatia msamaha. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kuwa mhitaji na mwenye shida ni sharti tosha la kupatiwa mtu misaada ya hali na mali na wala si lazima mhitaji huyo awe mtu mwema.

Aya ya 23 ya sura yetu ya An Nur ndiyo inayotuhatimishia darsa yetu hii. Aya hiyo inasema:

إِنَّ الَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ الْغَافِلاتِ الْمُؤْمِنَاتِ لُعِنُوا فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

Hakika wanaowasingizia wanawake, wanaojihishimu, walioghafilika, walio Waumini, wamelaaniwa duniani na Akhera, nao watapata adhabu kubwa.

Katika kuhitimisha aya zilizozungumzia uzushi, ambao ulihusisha tuhuma chafu dhidi ya mke wa Bwana Mtume, aya hii inatoa pia kaida na kanuni jumla kuhusu wanawake wote wasafi na wanaojistahi kwa kueleza kwamba hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kumtuhumu kuwa amezini na kumharibia heshima yake mwanamke muumini ambaye hana mahusiano haramu na mwanamme, kwa kutegemea dhana mbaya tu au maneno na habari za uvumi alizosikia mtu kwa watu wengine. Mtu mwenye kufanya kitu kama hicho anapaswa ajue kwamba kwa kufanya hivyo anakabiliana na Mwenyezi Mungu; na Yeye Mola ni mwenye kuwatetea wanaofanyiwa dhulma na kwa hivyo atamwadhibu mtu huyo kwa adhabu kali. Hapa duniani atamnyima rehma zake zisizo na ukomo na huko akhera, motoni ndiko yatakakokuwa makaazi yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata katika aya hii ni kwamba kulinda haki za wanawake wema wanaojiheshimu na kujistahi ni miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa na kuwekewa ratiba maalumu na Qur'ani na katika dini tukufu ya Uislamu. Kadhalika tunajifunza kutokana na aya hii kuwa katika mahusiano yao ya kifamilia na ya kijamii, wanawake wanatakiwa wajiepushe na kila aina ya mienendo na vitendo vinavyoweza kuwa sababu ya kuandamwa na tuhuma. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji, tunaifunga darsa yetu ya 609 ya Qur'ani. Tunamwomba Allah atulinde na tabia chafu ya kuzua tuhuma dhidi ya watu na pia ya kueneza uvumi juu ya tuhuma hizo. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)