Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 29 Aprili 2014 12:22

Sura ya An Nur, aya ya 15-20 (Darsa ya 608)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani, hii ikiwa ni darsa ya 608 ambapo kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 15 na 16 za sura hiyo ambazo zinasema:

إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّهِ عَظِيمٌ

Mlipoyapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa.

وَلَوْلا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَذَا سُبْحَانَكَ هَذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ

Na kwa nini mlipoyasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kundi moja la wanafiki wa Madina lilimzulia tuhuma kubwa mmoja wa wake wa Bwana Mtume kwa kudai kwamba alikuwa na uhusiano haramu na mmoja wa masahaba wa mtukufu huyo. Na tukasema kwamba Waislamu nao badala ya kukabiliana na watu walioeneza uvumi huo, walifanya kazi ya kueneza uvumi huo kwa watu wengine. Kitendo hicho kilimuudhi na kumuumiza Bwana Mtume na mkewe huyo yaani Bibi Aisha. Katika aya hizi tulizosoma Allah SW anasema: Kwa nini mulikuwa mukisimuliana na kunukuliana mdomo kwa mdomo kuhusu kitu ambacho hamkijui na hamna yakini nacho, na mkawa mnaichezea heshima na staha ya watu wengine? Kwani mlikuwa hamjui kwamba haifai kukurupuka tu na kusimulia kwa watu kila kitu kinachowahusu watu wengine, na hasa tena tuhuma kubwa kama hii ambayo mmoja kati ya watu wanaohusishwa nayo ni mke wa Mtume wenu?

Aya hizi zinaashiria majukumu mawili muhimu ya kijamii: La kwanza ni kwamba msikubali tu kila mnachokisikia katika jamii bila kuwepo hoja na ushahidi, ili muweze kuwazuia watu wanaotaka kueneza uvumi wa uwongo katika jamii. Na la pili ni kuwa haifai kuwasimulia watu wengine kila tunalosikia na tunalolijua kwa sababu si hasha baadhi ya wakati kufanya hivyo kukasababisha kuvunjika heshima za baadhi ya watu katika jamii, jambo ambalo halipendezi hata kidogo kwa mtazamo wa Uislamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusiyakubali tu yatokayo midomoni mwa watu pasina kuyachunguza na kuyafanyia utafiti. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kueneza tuhuma na kuharibu heshima za wengine mbele za watu ni kitu chepesi na rahisi, lakini mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ni jambo ovu mno na lenye kuchukiza sana. Na pia aya hizi zinatufunza kwamba kutetea heshima za watu wengine ni wajibu wa wanajamii wote. Badala ya kueneza yale tunayoyasikia inatakiwa tuchukue hatua na kukabiliana na mwanzishaji wa uvumi.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:

يَعِظُكُمُ اللَّهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

Mwenyezi Mungu anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!

وَيُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الآيَاتِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Na Mwenyezi Mungu anakubainisheni Aya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.

Kwa kuzingatia kuwa kuwazulia tuhuma watu, na tena basi katika suala la staha na heshima ya mke wa mtu, ni jambo zito mno mbele ya Mwenyezi Mungu, hivyo aya tulizosoma zimerudia tena kuzungumzia suala hilo na kueleza kwamba Allah SW, kama alivyo baba mwenye huruma na uchungu kwa mwanawe, anayempa mawaidha ili asije akafanya makosa tena, anakuaidhini na nyinyi pia kuwa mjichunge na mtahadhari kosa hili lisije likarudiwa tena katika jamii ya Kiislamu. Kwa sababu mambo kama haya hayalaiki kwa watu waumini. Ikiwa huko nyuma mlifanya kosa hili kwa sababu ya ujinga na mghafala, kwa kuwa sasa mshakuwa na uelewa nalo tubieni kwa mliyoyafanya hapo kabla na pia wekeni azma ya kutoyarudia tena hayo katika siku za usoni, na mjue pia kwamba Mwenyezi Mungu anayaelewa vyema mnayoyafanya, mnayoyafikiria na mnayoyanuia ndani ya nafsi zenu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwanadamu ni kiumbe anayehitajia nasaha na mawaidha, na Qur'ani ni kitabu bora zaidi cha mawaidha. Kwa hivyo tukisomeni na kupata ibra na mazingatio kutokana na aya zake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuwazulia tuhuma watu ambako hutokana na dhana mbaya na kuwatizama kwa jicho baya ni alama ya kuwa na imani dhaifu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuaidhika kuliko bora zaidi ni kwa mtu kutubia madhambi aliyofanya ambako humfanya afutiwe yale aliyoyafanya huko nyuma na pia humlinda na kuyarudia tena makosa na madhambi hayo katika mustakabali.

Darsa yetu hii wapenzi wasikilizaji inahatimishwa na aya za 19 na 20 ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَاللَّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لا تَعْلَمُونَ

Kwa hakika wale wanaopenda uenee uchafu kwa walioamini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.

وَلَوْلا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّه رَؤُوفٌ رَحِيمٌ

Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na kuwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu....

Katika aya hizi, Allah SW anatueleza kuwa kuwazulia tuhuma watu ni uovu mkubwa mno na kwamba si kuwazulia tuhuma watu na kueneza tuhuma hizo tu katika jamii ni dhambi, bali hata kama mtu ndani ya moyo wake pia atakuwa anapendezwa kuona heshima ya muumini inaharibiwa na kuporomoka kwa kujulikana yeye mbele za watu kuwa ni mfanya maovu, huko kutaka na kutamani ndani ya moyo wake mtu huyo pia ni dhambi hata kama hatochukua hatua yoyote kivitendo kuhusiana na jambo hilo. Ijapokuwa katika mafundisho ya Kiislamu, kiujumla nia, kusudio na dhamira ya kufanya dhambi haihukumiwi kuwa ni dhambi, lakini katika mambo mawili, Qur'ani tukufu imeielezea nia na hisia za ndani ya nafsi ya mtu juu ya mambo hayo kuwa ni dhambi. La kwanza ni kuwa na dhana mbaya juu ya mtu, ambapo kitabu hicho kitukufu kinasema:"Hakika baadhi ya dhana ni dhambi", na la pili ni hili la kupendezwa mtu na kufurahia kuondoka na kuharibika heshima ya mtu, ambapo hata kama hatofanya lolote kivitendo, lakini atakuwa amefanya dhambi. Na bila ya shaka kama tujuavyo, ghairi ya Allah SW hakuna mwengine yoyote ajuaye nia walizonazo watu nyoyoni mwao; na sisi hatuna ujuzi wa kuwatambua watu walio na nia na wenye kufurahia heshima za wenzao ziharibike na kuporomoka; lakini Yeye Mola kutokana na uraufu na upole wake kwa waja wake, haharakishi adhabu yake kwa watu hao ili asaa watubie na kuacha mwenendo wao huo. Amma wale ambao wanachukua hatua za kivitendo na kuwachafulia wenzao heshima zao, hao watapata adhabu hapa duniani ya kuchapwa bakora themanini, mbali na adhabu kali ya moto inayowangojea huko akhera. Miongoni mwa mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kwamba kupendezwa na dhambi ni utangulizi wa kuifanya. Na kati ya madhambi mbalimbali, dhambi pekee ambayo hata kupendezwa nayo tu kunahesabiwa kuwa ni dhambi, ni kumzulia tuhuma mtu na kumharibia heshima yake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kueneza machafu katika jamii ya Kiislamu, iwe ni kwa maneno au kwa matendo kunamharibia mtu dunia yake pamoja na akhera yake pia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 608 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na maradhi ya nafsi ya kuwadhania watu vibaya na kufurahia kuharibika na kuporomoka kwa heshima zao, amin. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)