Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 29 Aprili 2014 12:20

Sura ya An Nur, aya ya 6-14 (Darsa ya 607)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa darsa ya Qur'ani, hii ikiwa ni darsa ya 607 ambapo kwa sasa tunaizungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 6 hadi 10 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ يَرْمُونَ أَزْوَاجَهُمْ وَلَمْ يَكُن لَّهُمْ شُهَدَاء إِلاَّ أَنفُسُهُمْ فَشَهَادَةُ أَحَدِهِمْ أَرْبَعُ شَهَادَاتٍ بِاللَّهِ إِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ

Na wale wanaowasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.

وَالْخَامِسَةُ أَنَّ لَعْنَتَ اللَّهِ عَلَيْهِ إِن كَانَ مِنَ الْكَاذِبِينَ

Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.

وَيَدْرَأُ عَنْهَا الْعَذَابَ أَنْ تَشْهَدَ أَرْبَعَ شَهَادَاتٍ بِاللَّهِ إِنَّهُ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ

Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba huyo mume ni miongoni mwa waongo.

وَالْخَامِسَةَ أَنَّ غَضَبَ اللَّهِ عَلَيْهَا إِن كَانَ مِنَ الصَّادِقِينَ

Na mara ya tano ya kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake kama mume ni miongoni mwa wanaosema kweli.

وَلَوْلا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّهَ تَوَّابٌ حَكِيمٌ

Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na ya kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpokeaji toba, Mwenye hekima.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa ikiwa mtu atamsingizia mtu mwengine tuhuma ya zinaa na akashindwa kuleta mashahidi wanne, yeye mwenyewe atapigwa bakora 80 kwa kosa la kumzulia mtu tuhuma. Aya hizi tulizosoma zinabainisha hali zilizo nje ya hukumu hiyo kwa kueleza kuwa, lakini kama mume atamshuhudia mkewe anafanya uchafu na mwanamume mwengine na akaenda mbele ya Kadhi kutoa ushahidi hatohitajia kuleta mashahidi wengine. Bali inatosha kwa yeye mwenyewe kula yamini mara nne kwa jina la Allah kwamba anayoyasema ni kweli, na kisha aseme mara moja ya tano kuwa ikiwa mimi ni muongo basi laana ya Mwenyezi Mungu inishukie. Sambamba na yamini hiyo anayokula mume mtu, mke naye itabidi ima aungame kuwa kweli amefanya uchafu wa zinaa na kuyakubali madai aliyotoa mume wake au akanushe kuwa hakufanya hivyo. Akifanya hivyo itabidi ajitetee nafsi yake ambapo kama alivyofanya mumewe atatakiwa naye pia ale yamini mara tano. Katika mara nne za mwanzo atatakiwa aseme, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa mume wangu anasema uongo, na mara ya tano aseme, ghadhabu za Mwenyezi Mungu zinishukie ikiwa mume wangu atakuwa amesema kweli. Baada ya mke na mume kula yamini, ile adhabu ambayo alikuwa apewe mume kwa kuzua tuhuma na ya mke kwa kufanya uchafu wa zinaa zitaondoka. Pamoja na hayo viapo hivyo vina taathira zake pia. Na miongoni mwa hizo ni kwamba wawili hao, pasina kuhitajia kupeana talaka watakuwa wameshaachana moja kwa moja, na hadi mwisho wa uhai wao hawatokuwa na haki ya kurejeana au kuoana tena. Kwa hivyo katika hali ambazo watakosekana mashahidi, kula yamini tu kwa jina la Allah kunaweza kuwa kipimo cha kukubali au kupinga dai linalotolewa; na katika suala hilo hakuna tofauti yoyote kati ya mwanamke na mwanamme. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ili kulinda heshima ya mke na mume na kuzuia kuenea ufuska katika jamii, katika masuala ya kifamilia, maneno yao wenyewe wawili hao ni hoja, na wala hawahitajiki mashahidi wa nje. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa taratibu za Uislamu kuhusu viapo na kula yamini zimewekwa kwa madhumuni ya kuwadhibiti watu ili wasije wakafedheheshana. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika jamii ya Kiislamu kula yamini kwa jina la Allah kunapasa kuwe na heshima na utukufu ili mtu yeyote yule asithubutu kula yamini ovyo ovyo au kuisuta na kuikana yamini anayokula mtu dhidi yake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 11 ambayo inasema:

إِنَّ الَّذِينَ جَاؤُوا بِالإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ لا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الإِثْمِ وَالَّذِي تَوَلَّى كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ

Hakika wale walioleta uwongo mkubwa ni kundi miongoni mwenu. Msiufikirie ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa.

Aya hii wapenzi wasikilizaji inaendelea na maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu adhabu ya kuwazulia tuhuma wanawake walioolewa wenye kujistahi kwa kuashiria kisa kilichotokea katika zama za Bwana Mtume Muhammad SAW kuhusu mmoja wa wake wa mtukufu huyo. Katika vitabu vya historia imeelezwa kwamba wakati Bwana Mtume alipokuwa katika moja ya safari zake, alimchukua pamoja naye mkewe Bibi Aisha. Wakati walipokuwa wakirudi Madina Bibi Aisha alijitenga na msafara kwa ajili ya kukidhi haja zake binafsi na hivyo akaachwa nyuma na msafara huo. Kwa bahati mmoja wa masahaba ambaye naye pia alikuwa ameachwa nyuma na msafara alifanya kazi ya kumuunganisha tena Bibi Aisha na msafara wa Bwana Mtume. Baadhi ya watu walimzulia mke huyo wa Bwana Mtume na sahaba huyo wa mtukufu huyo tuhuma za kufanya uchafu na uongo huo ukasambazwa na kuenezwa kwa watu.

Na hapo ndipo ilipoteremshwa aya hii ili kumliwaza Bwana Mtume SAW na masahaba zake ambao waliudhiwa na kuumizwa sana na jambo hilo na kuwaambia kwamba kuna kheri iliyokuwa imejificha ndani ya mkasa huo, nayo ni kufichuka na kufedheheka baadhi ya wanafiki ambao waliweza kutambuliwa na watu kutokana na kueneza kwao uongo na uvumi huo; na kila mmoja wao atapata adhabu kulingana na jinsi alivyochangia katika jambo hilo. Tab'an kati ya wote hao, Abdullah Ibn Ubay, kiranja mkuu wa wanafiki wa Madina, na ambaye ndiye aliyekuwa na mchango mkubwa katika kutunga uongo huo na kueneza tuhuma hizo, yeye atapata adhabu kali zaidi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba si kila mara adui hufanya hujuma yake kutokea nje, bali baadhi ya wakati wanafiki wa ndani hutumia mbinu ya kueneza sumu ya uvumi na kuiletea jamii ya Kiislamu chungu ya mabalaa na matatizo. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa katika madhambi yanayofanywa na watu kwa pamoja, kila mmoja miongoni mwa walioshiriki katika kufanya dhambi hiyo atakuwa na hatia kwa kadiri ya alivyochangia. Na hapana shaka kuwa adhabu ya watu waliokuwa na jukumu kuu la upangaji njama na fitna itakuwa kubwa na kali zaidi kulinganisha na wengine.

Aya za 12, 13 na 14 za sura yetu ya An Nur ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

لَوْلا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ

Kwa nini mlipousikia, waumini wanaume na waumini wanawake hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?

لَوْلا جَاؤُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاء فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاء فَأُولَئِكَ عِندَ اللَّهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ

Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na ilivyokuwa hawakuleta mashahidi wanne basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo.

وَلَوْلا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ

Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na Akhera, bila ya shaka ingelikupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyojiingiza.

Aya hizi tulizosoma zinaendelea na maudhui iliyogusiwa katika aya zilizotangulia kwa kuwahutubu baadhi ya waumini, ambao kutokana na kuamini mambo haraka na kirahisi waliathiriwa na uvumi, na pasina kuchunguza wala kufanya uhakiki nao pia wakaanza kuwasimulia wenzao uvumi wa tuhuma chafu, na kuwauliza kwamba: kwa nini wakati mliposikia maneno ya wanafiki kuhusu waumini wenzenu hamkuwa na dhana njema kwa waumini hao na kwa nini hamkusema huu ni uongo mkubwa na wa wazi kabisa? Wakati nyinyi mlikuwa na uhakika kuhusu usafi wa mke wa Mtume na kuhusu tabia chafu ya wanafiki ya kueneza uwongo, kwa nini mliyapokea na kuyaamini maneno hayo? Kwa nini hamkuwataka walete mashahidi wanne, ili kama hawakufanya hivyo muwape adhabu kwa kuwazulia tuhuma chafu watu wasafi wanaojistahi? Kwa hakika ujumbe wa aya hizi kwa waumini ni kwamba sio tu nyinyi wenyewe msiwe na dhana mbaya kwa watu wengine lakini kama mtasikia tuhuma pia msizikubali bali msimame kuwatetea watu wanaojistahi na wenye kujiheshimu, ila pale itakapothibitika kwa ushahidi madhubuti na wa wazi kabisa kwamba watu hao wamefanya makosa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tunatakiwa tuchukue hatua mwafaka kukabiliana na uvumi usio wa kweli unaoenezwa katika jamii; na haijuzu kuunyamazia kimya wala kuchangia katika kuueneza. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuzusha tuhuma dhidi ya mwanajamii yeyote ni sawa na kuwazulia tuhuma wanajamii wengine. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuwa na dhana njema na waumini ni msingi unaopasa kutawala katika mahusiano baina ya watu wa jamii ya Kiislamu. Na kadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba kulinda na kuchunga mipaka ya heshima kwa Bwana Mtume na familia yake ni jambo la lazima na la wajibu kwa Waislamu wote na inapasa kukabiliana kikamilifu na kila anayejaribu kwa namna yoyote ile kuchupa mipaka ya heshima hiyo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 607 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atuepushe na maradhi mabaya ya kinafsi ya kuzusha na kueneza tuhuma hususan dhidi ya Waislamu wenzetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)