Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 29 Aprili 2014 12:04

Sura ya An Nur, aya ya 1-5 (Darsa ya 606)

 Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, hii ikiwa ni darsa ya 606 ambayo itaanza kuzungumzia sura ya 24 ya An Nur. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya kwanza ya sura hiyo ambayo inasema:

سُورَةٌ أَنزَلْنَاهَا وَفَرَضْنَاهَا وَأَنزَلْنَا فِيهَا آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ لَّعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ

Ni Sura tuliyoiteremsha na tukawajibisha (hukumu zilizomo ndani yake); na tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi ili mkumbuke.

Suratun Nur ni sura iliyoteremshwa Madina na ina aya 64. Kupewa sura hii jina la "Nur" ni kwa sababu ya aya yake ya 35 ambayo ndani yake imemtambulisha Allah SW kuwa ni nuru ya mbingu na ardhi. Nusu ya kwanza ya sura hii hadi aya ya 35 inawausia waumini kufunga ndoa, kujenga familia, kuchunga staha na heshima, kujiepusha na mashusiano haramu na masuala mengine kama hayo. Na nusu ya pili ya sura hii ya An Nur inabainisha mafundisho ya dini kuhusu kumjua Mwenyezi Mungu, kuwafuata Mitume wake Allah, kuundwa utawala wa waja wema, baadhi ya masuala ya kifamilia n.k. Japokuwa aya zote na sura zote za Qur'ani zimeteremshwa na Mwenyezi Mungu lakini kutajwa jina la sura mwanzoni mwa sura hii kunabainisha umuhimu wa aya na masuala yaliyozungumziwa ndani yake ambayo baadhi yake yanahusiana na hakika halisi ya Tauhidi na baadhi nyengine inahusu hukumu za waumini wanaume na wanawake katika uhusiano wa kifamilia na kijamii. Ni wazi kwamba kudumisha na kuimarisha imani juu ya Allah huwa sababu ya kupungua tabia chafu na mwenendo potofu ndani ya jamii na kuyafanya masuala yote ya kijamii yafuate mkondo sahihi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Qur'ani tukufu ni kitabu cha sheria kwa Waislamu, na kufuata hukumu na maamrisho yaliyomo ndani yake ni faradhi na wajibu kwao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mafundisho ya Qur'ani huondoa utando wa wingu la mfaghala na kumkumbusha mwanadamu yale yenye chimbuko la akili, fitra na maumbile yake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 2 na ya 3 ambazo zinasema:

الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ وَلا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ

Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini.

الزَّانِي لا يَنكِحُ إِلاَّ زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً وَالزَّانِيَةُ لا يَنكِحُهَا إِلاَّ زَانٍ أَوْ مُشْرِكٌ وَحُرِّمَ ذَلِكَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ

Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo yameharimishwa kwa Waumini.

Katika Uislamu malipo hasa ya thawabu na adhabu yako huko kwenye ulimwengu wa akhera. Lakini hapa duniani pia ili kuilinda jamii na ufisadi na upotofu Mwenyezi Mungu ameweka hukumu za adhabu kwa waovu ili kuzuia kuenea uchafu, ufuska na maovu katika jamii, ikiwemo ya kisasi kwa muuaji au ya mwizi kukatwa mkono. Aya hizi tulizosoma zinatoa onyo kwa watu wenye mahusiano haramu ya ngono kwamba japokuwa adhabu yao hasa ya dhambi hiyo kuu waliyofanya wameekewa Siku ya Kiyama lakini Allah SW ameamuru hapa duniani pia wapewe adhabu kali mbele ya kadamnasi ili iwe funzo na ibra kwa wengine. Tab'an ikiwa ovu hilo halijadhihirika, Mwenyezi Mungu hajajuzisha wala kuruhusu kupekechuliwa kwa kufanyiwa upelelezi kwa lengo la kulianika hadharani. Hata hivyo ikiwa watu wasio na haya wanaochupa mipaka kwa kutojali wala kuionea aibu dhambi ya kuwa na uhusiano haramu wa kiuasherati hawatotiwa adabu, watasababisha kuenea ufuska na uchafu wa zinaa katika jamii. Kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu ameweka adhabu kali kwa watu hao ili adhabu hiyo itoe funzo na kuwa ibra na mazingatio kwa wao wenyewe na kwa wengine pia. Kisha aya zinaendelea kwa kukataza wanaume na wanawake wasafi na wenye kujistahi kuoana na wanawake na wanaume wachafu wafanyao ufuska. Hii ni kwa ajili ya kuwakinga wanaume na wanawake wema wasije wakaharibika na kupotoka kutokana na taathira za kuwa na ukuruba na maingiliano na watu hao na vilevile kwa madhumuni ya kuepusha kuenea ndani ya jamii maradhi mbalimbali yanayosababishwa na vitendo vya uasherati. Inapasa tuelewe pia kwamba hukumu ya bakora mia moja iliyotajwa katika aya ya pili ya Suratun Nur inawahusu wanaume wasio na wake, na wanawake wasio na waume, na ambao wamefanya tendo la zinaa kwa ridhaa na hiyari yao wenyewe. Lakini kama wanaume wenye wake na wanawake wenye waume watawaendea kinyume wake na waume zao na kuwa na mahusiano haramu ya uasherati na wanawake au wanaume wengine hukumu yao itakuwa na kuuawa. Kama ambavyo mwanamme atakayemkamata mwanamke kwa nguvu na kumlazimisha azini naye, au akafanya tendo hilo na maharimu yake, hukumu yake huyo pia itakuwa ni kifo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mtazamo wa Uislamu, uhuru wa ngono na uhusiano wa uasherati ni moja ya madhambi makubwa na wala hauruhusiwi katika dini hiyo tukufu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa adhabu ya watu wanaofanya na kueneza ufuska na uasherati katika jamii inapasa iwe kali na ya kuzuia vitendo hivyo, na wala utekelezaji wake usiathiriwe na hisia za upole na huruma. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kumpa adhabu mhalifu kunafanywa kwa madhumuni ya kumuadibisha na kulinda mipaka ya staha na heshima ndani ya jamii. Aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba kuzini kuna uzito unaofikia kiwango kama cha kumshirikisha Mwenyezi Mungu na hivyo kumvua mtu imani yake. Na vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa staha na hulka njema ni miongoni mwa masharti muhimu zaidi katika kuchagua mchumba kwa ajili ya ndoa.

Aya ya 4 na ya 5 ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu hii kwa leo. Aya hizo zinasema:

وَالَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَأْتُوا بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاء فَاجْلِدُوهُمْ ثَمَانِينَ جَلْدَةً وَلا تَقْبَلُوا لَهُمْ شَهَادَةً أَبَدًا وَأُولَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

Na wale wanaowasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wanne, basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio mafasiki.

إِلاَّ الَّذِينَ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Isipokuwa wale waliotubia baada ya hayo na wakatengenea; kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kurehemu.

Kutokana na kuainishwa adhabu ya wanaume na wanawake waliozini, yamkini hukumu hii ikatumiwa vibaya na baadhi ya watu ili kuanza kupeleleza maisha ya watu wengine na kuzusha shaka na dhana mbaya na hatimaye kuwavurumizia tuhuma za uchafu wa zinaa wanaume na wanawake wasafi na wenye kujistahi. Kwa sababu hiyo aya tulizosoma zimetaja adhabu kali kwa watu wanaotaka kuitumia vibaya hukumu hiyo ili kuwasingizia watu hao tuhuma hizo na kueleza kuwa ili kuthibitisha dai hilo lazima walete mashahidi wanne waadilifu, la sivyo kila mmoja kati ya hao waliozusha dai hilo atatandikwa bakora 80.

Kiujumla ni kwamba maneno ya watu kama hao yatakuwa hayana thamani wala itibari, na katika siku za usoni pia ushahidi wao katika jambo lolote lile hautokubaliwa ila pale watakapoacha mwenendo wao huo wa kuzusha tuhuma za uchafu, wakatubia na kujirekebisha. Imeelezwa katika hadithi kwamba Imam Jaafar Sadiq (AS) aliulizwa:" Kwa nini katika kuthibitisha mauaji mashahidi wawili wanatosha lakini katika kuthibitisha zinaa lazima wawepo mashahidi wanne?" Mtukufu huyo akajibu kwa kusema: "Shahidi wa mauaji anatoa ushahidi kwa ajili ya kumpa adhabu mtu mmoja, lakini shahidi wa zinaa ni kwa ajili ya adhabu ya watu wawili, yaani mwanamke na mwanamme aliyezini." Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwasingizia tuhuma za zinaa wanawake walioolewa wenye kujistahi kumewekewa adhabu kali. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa adhabu ya bakora 80 ya mwenye kuwasingizia uchafu wa zinaa watu wasafi na wenye kujistahi haipishani sana na ya mtu aliyefanya tendo hilo, ya bakora 100. Na aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa heshima za watu zina thamani mbele ya Allah SW kiasi kwamba ikiwa watu wanne hawatotoa ushahidi dhidi ya mtu wa kufanya uchafu, Allah SW haruhusu watu watatu wengine wamkashifu na kuifichua dhambi aliyofanya, la sivyo watu hao watapewa adhabu. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na kila aina ya machafu, ya siri na ya dhahiri. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)