Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 15:39

Sura ya An-Naml, aya ya 89-93 (Darsa ya 681)

Sura ya An-Naml, aya ya 89-93 (Darsa ya 681)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 681, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 89 na 90 ambazo zinasema:


مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَهُم مِّن فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ


Watakao kuja na mema, watapata bora kuliko hayo. Nao watasalimika na mfazaiko wa Siku hiyo.


وَمَن جَاءَ بِالسَّيِّئَةِ فَكُبَّتْ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ هَلْ تُجْزَوْنَ إِلاَّ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ


Na watakao kuja na uovu, basi zitasunukishwa nyuso zao Motoni. Je! Kwani mnalipwa isipo kuwa mliyo kuwa mkiyatenda?


Katika darsa iliyopita mazungumzo yetu yaliishia katika kuelezea mwisho wa dunia na kusimama kwa Kiyama. Baada ya kuzungumziwa hayo, aya tulizosoma zinaashiria utaratibu wa ulipaji jaza na thawabu kwa wema, na adhabu na ikabu kwa wabaya na kueleza kwamba: elimu na hekima ya Allah SW inahukumu kwamba wanadamu wanapaswa kuwajibika na kubeba dhima na mas-ulia ya matendo yao. Kwa sababu Yeye Mola amewapa akili na irada, na hiyari ya kuchagua jambo na kuchukua uamuzi wa kulifanya. Ukweli ni kwamba wanadamu wanapata sehemu tu ya matokeo na matunda ya amali na matendo yao hapa duniani; kwa sababu dunia hii haina utoshelezi wa kulipa kikamilifu jaza na malipo ya thawabu au adhabu za matendo ya watu. Lakini katika ulimwengu wa akhera ambao haufungwi na mipaka ya mahala na zama kila mtu atayaona matokeo kamili ya matendo yake pamoja na athari zake na atalipwa malipo yake kulingana na amali zake hizo. Kwa mujibu wa aya tulizosoma, kila mtu atakayefanya jema atapata jaza na malipo bora ya thawabu kupita jema alilofanya, tab'an kwa sharti kwamba tendo hilo jema lifike salama huko lilikokusudiwa pasina kuharibiwa na mambo yanayoharibu malipo yake kama vile ria, yaani kujionyesha, ghururi n.k. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba lililo muhimu zaidi ya kufanya amali njema ni kuilinda na kuitunza amali hiyo na mambo yanayoiharibu, kama vile ria, kuridhika mtu na mema yake na kufanya madhambi ambavyo huyafuta mema na kuyafanya yasifike akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa malipo ya thawabu anayolipa Mwenyezi Mungu ni makubwa na ya juu zaidi kulinganisha na mema wayafanyayo watu, lakini kiwango cha malipo ya adhabu kinalingana na mabaya waliyofanya watu waovu.
Zifuatazo sasa ni aya za 91 na 92 ambazo zinasema:


إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ رَبَّ هَذِهِ الْبَلْدَةِ الَّذِي حَرَّمَهَا وَلَهُ كُلُّ شَيْءٍ وَأُمِرْتُ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْمُسْلِمِينَ


Hakika mimi nimeamrishwa nimuabudu Mola Mlezi wa mji huu ambaye ameufanya ni mtakatifu; na ni vyake Yeye tu vitu vyote. Na nimeamrishwa niwe miongoni mwa Waislamu, wenye kunyenyekea.


وَأَنْ أَتْلُوَ الْقُرْآنَ فَمَنِ اهْتَدَى فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَقُلْ إِنَّمَا أَنَا مِنَ الْمُنذِرِينَ


Na niisome Qur'ani. Na mwenye kuongoka, basi ameongoka kwa faida ya nafsi yake; na aliye potea - basi sema: Hakika mimi ni miongoni mwa waonyaji tu.


Aya hizi na ile inayofuatia ambayo ni aya ya mwisho ya Suratul Naml zinabainisha maneno ya mwisho ya Bwana Mtume SAW kwa washirikina wa Makka kwamba ikiwa hamtoacha kuabudu masanamu jueni kwamba mimi nimetimiza wajibu wangu kikamilifu ambao ni kufikisha aya za Mwenyezi Mungu, kuonya na kutoa indhari. Sasa ni nyinyi wenyewe, ambao inapasa muamue kwa hiyari yenu kuchagua moja kati ya mawili. Ima kuyakubali maneno ya Mwenyezi Mungu na kuufikia uongofu au msimame kukabiliana na haki na kujitafutia wenyewe sababu za kuishia kwenye dhalala na upotofu. Bila ya shaka, lolote mtakalochagua baina ya mawili hayo faida na hasara yake zitakurudieni nyinyi wenyewe. Msidhani kwamba kuamini kwenu haki kutaninufaisha mimi au kukufuru na kukadhibisha kwenu kutanisababishia mimi madhara. Mimi ninatekeleza wajibu wangu mbele ya Mwenyezi Mungu, ninatii amri yake Yeye, na badala ya masanamu ya mawe na miti mliyoyapanga ndani ya Nyumba ya Al-Kaaba, ninamwabudu Mola wa Al-Kaaba na wa mji huu ambaye si Nyumba hii tu, bali ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake ni milki yake Yeye.
Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaashiria mas-ulia tofauti ya Bwana Mtume SAW: Ya kwanza ni ya binafsi ambayo ni ya kumwabudu Allah na kutekeleza maamrisho yake, ambapo kwa upande wa hili, Bwana Mtume SAW yuko sawa na Waislamu wengine. Lakini mas-ulia ya pili ni ya Utume, yaani kufikisha aya za Mwenyezi Mungu kwa watu na kuwapa bishara njema, indhari na maonyo. Mtume hayuko kama walivyo watawala na wafalme, ambao wao wanakuwa ni watoaji amri tu kwa watu, ambao wana wajibu wa kutii na kutekeleza amri hizo. Kile ambacho Bwana Mtume Muhammad SAW anawaamrisha watu kukifanya, yeye mwenyewe huwa wa kwanza na wa mbele kukitekeleza; na kama alivyo Muislamu mwengine yeyote, naye pia anapaswa kutekeleza hukumu na mafundisho ya dini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume ni waja wenye utii kamili na mutlaki kwa amri za Allah SW. Chochote wakisemacho hakitokani na wao wenyewe, na wala hawafanyi lolote kwa utashi wao wenyewe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa jukumu la Mitume na wafanya tablighi ya dini ni kuwafikishia watu aya za Mwenyezi Mungu kwa uwazi kabisa; kukubali au kutokubali; na kuamini au kukufuru, hayo yanawahusu watu wenyewe. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wanadamu huwa muda wote wanakabiliwa na hatari ya mghafala na usahaulifu wa kumdhukuru na kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo jukumu la viongozi wa dini ni kuwapa indhari watu na kuwatahadharisha na mwisho mbaya wa matendo yao maovu.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 93 ya sura hii ya An-Naml ambayo inasema:


وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ سَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ فَتَعْرِفُونَهَا وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ


Na sema: Alhamdu Lillahi, (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu) Yeye atakuonyesheni Ishara zake, na mtazijua. Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.


Aya hii ambayo ndiyo aya ya mwisho ya Suratun Naml inahatimisha sura yetu hii kwa kumhimidi na kumshukuru Mwenyezi Mungu SW. Ni shukrani kutokana na neema kubwa ya Qur'ani ambayo ni wenzo wa uongofu wa kumuelekeza mja kwa Mwenyezi Mungu; na shukrani kwa neema ya Mtume ambaye kama alivyo mwalimu mwenye huruma anamfikiria mwanadamu ili aweze kuifikia saada ya duniani na akhera. Kisha aya inaendelea kwa kueleza kwamba: Watakaofuatia katika zama za baadaye watakuja kuona ishara nyingi za elimu, uwezo na hikima ya Mwenyezi Mungu. Ishara ambazo zinaonekana kuanzia kwenye viumbe wadogo kabisa wanaojulikana duniani, mpaka viumbe na maumbo makubwa kabisa ya sayari za mbali kabisa zilizoko angani. Hakuna shaka kuwa namna ya utazamaji wa watu inatofautiana. Mwalimu wa utabibu aliyemo kwenye chumba cha upasuaji hulipasua figo ili kuweza kuwaelezea wanafunzi wake sehemu mbalimbali za kiungo hicho. Na muuza mishkaki ya maini, naye pia hutumia kisu ili kupasua na kukata kiungo hicho. Japokuwa kidhahiri wawili hao wanafanya kitendo kimoja, lakini mitazamo na malengo yao huwa ni tofauti.
Ikiwa tunautambua mfumo mzima wa ulimwengu kuwa ni muumbwa, basi kila tukionacho ni alama na ishara ya Muumba wa ulimwengu; la kama tutauitakidi mfumo mzima wa maumbile kuwa ni kitu kisicho na lengo lolote, basi tutakuwa tumeghafilika na kumtambua Muumba wake. Na kughafilika huko na Muumba kuna taathira kubwa kwa fikra na mwenendo wa mtu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuteremshwa Qur'ani na kubaathiwa Bwana Mtume Muhammad SAW ni neema mbili kubwa ambazo inapasa kila mara tuoneshe ushukurivu kwa kujaaliwa neema hizo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kila tulichoona hadi sasa katika ishara za Allah ni sehemu tu ya ishara hizo. Kadiri wanadamu wanavyopiga hatua na kuendelea zaidi kielimu ndivyo ishara na alama mpya za uwezo na adhama ya Allah katika ulimwengu wa maumbile zitakavyozidi kudhihirika. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa muhula anaotupa Allah tusiuchukulie kuwa ni ishara ya Yeye Mola kughafilika nasi; la hasha, Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyaangalia matendo yetu, na uangalizi huo ni wa kudumu unaotokana na sifa ya Yeye kuwa Mola mlezi wa viumbe. Wapenzi wasikilizaji, tunamshukuru Allah kwa kutupa taufiki ya kuihitimisha tarjumi na maelezo ya Suratun Naml. Na hadi sasa tumekamilisha tarjumi na maelezo ya juzuu 20 za Qur'ani tukufu. Inshallah katika darsa yetu ijayo tutaanza kuzungumzia sura ya 28 ya Al Qsas. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuifuata Qur'ani kikamilifu na kuifanya kuwa ndio katiba na mwongozo wetu katika maisha yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)