Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 15:37

Sura ya An-Naml, aya ya 86-88 (Darsa ya 680)

Sura ya An-Naml, aya ya 86-88 (Darsa ya 680)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 680, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 86 ambayo inasema:


أَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا اللَّيْلَ لِيَسْكُنُوا فِيهِ وَالنَّهَارَ مُبْصِرًا إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ


Je! Hawaoni kwamba sisi tumeufanya usiku ili watulie, na mchana wa kuangaza. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao amini.


Katika aya tulizosoma kwenye darsa iliyopita zilizungumziwa nukta kadhaa kuhusu Siku ya Kiyama ili kuwataka wakanushaji waachane na dhana na fikra hizo za ukadhibishaji, na wala wasione kujiri kwa tukio hilo la mwisho wa ulimwengu huu kuwa ni jambo muhali. Baada ya maelezo hayo, aya hii ya 86 inaashiria dhihirisho jengine la nguvu na uwezo wa Allah SW na kueleza kwa kuuliza: je hadi sasa mumefikiria jambo hili, kwamba lau kama sayari ya ardhi ingekuwa muda wote katika hali ya mwanga, ikawa inaangaziwa na mwangaza na joto la jua mtawalia, vipi mngeliweza kupumzika na kupata utulivu? Au je, kama sayari ya dunia ingekuwa muda wote katika giza totoro kama ulivyo usiku, vipi mngeliweza kushughulika na kufanya kazi? Na katika hali hiyo mimea na miti ingewezaje kukua na kustawi? Hivi kweli mzunguko wa dunia wa kujizunguka yenyewe katika muda wa saa 24 ambao umekuwezesheni nyinyi kupanga ratiba za kazi na shughuli zenu za kila siku kulingana na wakati wenu wa kupumzika na kulala wakati wa usiku, umetokea kwa sadfa tu? Leo hii imethibitishwa kwa mtazamo wa kisayansi kuwa giza la usiku lina nafasi kubwa zaidi na ya msingi katika kuipa utulivu mishipa ya fahamu na akili ya mtu; na mwangaza wa mchana katika kumwezesha kufanya shughuli zake katika nyanja tofauti. Qur'ani tukufu imezikariri aya kama hizi mara kadhaa ili kuwazindua wale walio na kiu ya kuijua haki na walio tayari kuikubali, kwamba watupie jicho mazingira yaliyowazunguka ili waweze kubaini na kuamini elimu, nguvu na hekima za Muumba wa ulimwengu na kuacha kukanusha Kiyama bila ya hoja wala sababu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuingia na kutoka usiku na mchana ni alama na ishara ya elimu na tadbiri ya Muumba wa ulimwengu. Inapasa tuviangalie vitu hivi kwa makini na mazingatio, na wala masuala yetu ya kila siku ya kimaisha yasitufanye tukaacha kutafakari juu ya uumbaji. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuzungumziwa kulala na kuamka kuwa ni miongoni mwa ishara za Kiyama, ni kwa sababu kila siku, sisi katika dunia hii tunaipitia tajiriba ya kufa na kufufuka kutokana na kulala kwetu na kuamka kwetu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ratiba ya maisha ya mtu inapasa ifuatane na nidhamu ya mfumo wa maumbile: usiku uwe ni kwa ajili ya kupumzika na mchana kwa ajili ya kufanya kazi. Na ndiyo kusema kwamba kubaki macho hadi usiku wa manane na kuendelea kulala hadi mchana ni kinyume na mfumo wa kimaumbile wa uumbaji.
Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya ya 87 ambayo inasema:


وَيَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَفَزِعَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الأَرْضِ إِلاَّ مَن شَاء اللَّهُ وَكُلٌّ أَتَوْهُ دَاخِرِينَ


Na Siku litapo pulizwa baragumu, watafazaika waliomo mbinguni na waliomo ardhini, ila amtakaye Mwenyezi Mungu. Na wote watamfikia nao ni wanyonge.


Aya hii inarejea tena kwenye maudhui ya kufufuliwa viumbe na kuashiria utangulizi wake ambao ni kupulizwa baragumu. Kwa mujibu wa aya za Qur'ani baragumu litapulizwa mara mbili: ya kwanza ni wakati wa mwisho wa dunia ambao ndio unaoashiriwa katika aya hii; na kwa kulisikia baragumu hilo viumbe vyote vitataharuki na kufa kutokana na hofu, kihoro na mshtuko. Mara ya pili ni wakati wa kusimama Kiyama, ambapo viumbe vyote vitafufuka na kusimama mbele ya uwanja wa kufufuliwa. Kama inavyoeleza aya ni kwamba wakati litakapopulizwa baragumu wanadamu wote watapatwa na hofu, lakini waja wema na waliotakasika na vile vile malaika hawatokuwa miongoni mwa hao kama itakavyoelezwa katika aya zitakazofuatia, hususan aya ya 89 kwamba watakuwa katika amani na utulivu. Tab'an wakati litakapopulizwa baragumu la kwanza, waja wote, wema na wabaya pamoja na malaika, watakufa na kusalimu amri mbele ya irada hiyo ya Allah kwa khushuu na unyenyekevu. Na wakati litakapopulizwa baragumu la pili watafufuka na kusimama mbele ya Mola wao Muumba. Kwa mujibu wa hadithi, malaika mwenye mas-ulia na kazi ya kupuliza baragumu la kufa na kufufuka viumbe Siku ya Kiyama anaitwa Israfil na ni mmoja wa malaika waliokurubishwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kwa mujibu wa Qur'ani, kusambaratika na kutoweka kwa mfumo mzima wa ulimwengu wa maumbile na kufa kwa viumbe wote wa ardhini na wa mbinguni kutatokea kwa wakati mmoja kwa mlio wa sauti kubwa na ya kutisha. Funzo jengine tunalolipata kutokana na aya hii ni kuwa mbinguni pia kuna viumbe hai. Na wao pia kama walivyo viumbe wa ardhini watafufuliwa na kusimamishwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mauti hawakuumbiwa wanadamu peke yao, bali viumbe wengine pia wakiwemo malaika, kuna siku nao pia watakufa.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 88 ambayo inasema:


وَتَرَى الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ صُنْعَ اللَّهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا تَفْعَلُونَ


Na unaiona milima unaidhania imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za myatendayo.


Aya hii pia inaashiria muujiza mwengine katika miujiza ya uumbaji na kueleza kwamba kwa mnavyoona nyinyi milima iko thabiti na imetulia, ilhali kama yalivyo mawingu, milima nayo iko katika mwendo wa polepole, wa taratibu na wa kimyakimya. Hii ni katika ishara za adhama ya Muumba, ambaye ameufanya mwendo wa kasi wa sayari ya dunia kujizunguka yenyewe uwe ni kitu kisichohisika na mwanadamu na kumfanya kiumbe huyo adhani kwamba vitu vyote viko thabiti na vimetulia, kiasi kwamba hata katika zama mbalimbali za historia watu na hata wanasayansi walikuwa wakidhani kuwa dunia iko thabiti na imetulia na kwamba jua na mwezi ndivyo vilivyoko kwenye harakati na mwendo wa kuizunguka sayari ya dunia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba harakati ya milima haitenganiki na harakati ya sayari ya dunia; kwa hivyo dunia nayo iko katika mwendo na harakati. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ni kitu cha kustaajabia kwamba zaidi ya miaka elfu moja nyuma na kabla ya Galileo na wanasayansi wengine, Qur'ani tukufu ilizungumzia habari ya kuzunguka kwa dunia; na huu ni mmoja wa miujiza ya kielimu ya Kitabu hicho cha Allah. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba harakati na mwendo wa milima ni wa kasi kama ulivyo wa mawingu. Kutulia kwa sayari ya dunia licha ya mwendo wake wa kasi ni moja ya ishara za kustaajabisha za Mwenyezi Mungu. Wa aidha aya hii inatuelimisha kuwa katika mtazamo wa Qur'ani viumbe vyote vya Mwenyezi Mungu vimeumbwa vikiwa imara na thabiti, na hakuna kasoro wala nakisi yoyote katika uumbaji. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 680 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)