Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 14:51

Sura ya An-Naml, aya ya 82-85 (Darsa ya 679)

Sura ya An-Naml, aya ya 82-85 (Darsa ya 679)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 679, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 82 na 83 ambazo zinasema:


وَإِذَا وَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِمْ أَخْرَجْنَا لَهُمْ دَابَّةً مِّنَ الأَرْضِ تُكَلِّمُهُمْ أَنَّ النَّاسَ كَانُوا بِآيَاتِنَا لا يُوقِنُونَ


Na itapo waangukia kauli juu yao, tutawatolea mnyama katika ardhi atakaye wasemeza, ya kuwa watu walikuwa hawana yakini na Ishara zetu.


وَيَوْمَ نَحْشُرُ مِن كُلِّ أُمَّةٍ فَوْجًا مِّمَّن يُكَذِّبُ بِآيَاتِنَا فَهُمْ يُوزَعُونَ


Na Siku tutapo wakusanya watu kutoka kila umma kundi katika wanao kadhibisha Ishara zetu, nao watagawanywa mafungu mafungu.


Aya hizi tulizosoma zinaendelea na maudhui iliyokuja katika darsa iliyopita kwa kuzungumzia tukio la Kiyama na kueleza kwamba: katika zama za mwisho wa dunia na kukaribia tukio la Kiyama, Mwenyezi Mungu SW atawafufua na kuwatoa ardhini baadhi ya watu waliokuwa tayari wameshaondoka duniani. Wakati litakapojiri hilo, mmoja wa watu hao watakaofufuliwa, atazungumza na wakanushaji wa Kiyama, na kuelezea inadi na kuikaidi kwao haki, mpaka kufikia hadi kwamba licha ya kuona ishara zote pamoja na miujiza ya Mwenyezi Mungu wakanushaji hao hawatokuwa tayari kuamini kufufuliwa na kuwa hai tena wafu baada ya kifo.
Kufufuliwa wafu katika dunia hii hii, kwa irada ya Allah SW ni jambo ambalo lilishawahi kutokea hapo kabla, na Qur'ani tukufu pia imeliashiria jambo hilo. Miongoni mwao ni mmoja wa Mitume wa Allah ambaye aliomba aoneshwe mandhari ya Siku ya Kiyama ya jinsi watakavyofufuliwa wafu; na Allah akamfisha kwa muda wa miaka mia moja kisha akamfufua. Tukio hilo limeashiriwa kwenye aya ya 259 ya Suratul Baqarah. Vilevile kuna tukio la mtu aliyeuliwa bila ya kosa miongoni mwa Bani Israil, ambaye kwa irada ya Allah, kilipopigwa kiwiliwili chake kwa kipande cha nyama ya ng'ombe wa dhabihu walioamrishwa watu hao wamchinje, mtu huyo alifufuka na kumtaja aliyemuua. Tukio hili limeashiriwa pia kwenye aya ya 73 ya sura hiyo hiyo ya Al- Baqarah. Lakini pia kwa upande wa Nabii Isa (AS), moja ya miujiza ya Mtume huyo kama inavyosimulia Qur'ani, ulikuwa ni kuwafufua wafu papa hapa duniani. Isitoshe, aya ya 56 na 243 za Suratul Baqarah pia zinaeleza kwa uwazi kabisa habari za kufufuliwa papa hapa duniani baadhi ya wafu wa kaumu zilizopita.
Kwa hiyo aya hizi tulizosoma pia zinaashiria suala la Raj'at la baadhi ya watu katika siku za kukaribia mwisho wa dunia, yaani aakhiruz-zamaan, lakini hazijataja majina wala kubainisha sifa za watu hao. Kulingana na kaida na kanuni za mambo, ili kuweza kufahamu aya sawasawa, inabidi turejee kwenye hadithi zenye itibari na za kuaminika zinazozungumzia suala hili. Japokuwa neno "daabbah" lililokuja katika aya tulizosoma lina maana ya mnyama, na ni mara chache hutumika kuhusiana na mwanadamu, lakini kwa kuchunguza mwahala lilimotumika neno hili ndani ya Qur'ani kwa sura ya umoja na wingi tutabaini kuwa neno hili lina maana pana inayojumuisha wanadamu pia. Mfano ni aya ya 22 ya Suratul Anfal ambayo inasema: «إِنَّ شَرَّ‌ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الصُّمُّ الْبُکْمُ الَّذِینَ لَایَعْقِلُونَ» Hakika vinyama viovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni vile viziwi na bubu visio tumia akili zao. Bila ya shaka madhumuni ya wanyama waliokusudiwa katika aya hii ni watu waliokemewa na kufananishwa na viziwi na mabubu, kwa sababu hawatumii akili wala hawatafakari. Kuhusu tarjumi ya aya 82 tuliyosoma kwamba tutawatolea mnyama katika ardhi atakaye wasemeza, kwa mujibu wa hadithi maana iliyokusudiwa hapa ni mmoja wa mawalii wakubwa wa Allah au shakhsia mmoja muhimu, ambapo katika baadhi ya hadithi tukio hili limehusishwa na Imam Ali Ibn Abu Talib (AS).
Aidha kuhusu makundi ya watu waliozungumziwa katika aya ya 83 kuhusu kufufuliwa kwao, kwa mujibu wa hadithi, baadhi ya waja wema waumini ambao waliishi katika zama mbalimbali za historia na baadaye kuaga dunia, Mwenyezi Mungu atawafufua katika aakhiruz-zamaan ili waje kushuhudia na kujionea utawala wa ulimwengu mzima wa Imam Mahdi (AS) na kuwa miongoni mwa wafuasi na wasaidizi wa mtukufu huyo. Kwa upande mwengine Allah SW atawafufua pia baadhi ya watu waliokuwa vigogo wa ukafiri na dhulma katika zama mbalimbali za historia ili waweze kulipwa adhabu zao za duniani katika utawala huo wa haki na uadilifu wa ulimwengu mzima. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kufufuka waliokufa ni miongoni mwa mambo ambayo hayahusiani na Siku ya Kiyama tu bali yamewahi kutokea pia hapa duniani na yataendelea kutokea; na kuwa na shaka juu ya jambo hilo ni kuutilia shaka uwezo wa Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa mwisho wa dunia utatokea kwa kuwepo viongozi wa waja waumini na vigogo wa dhulma na ukafiri; lakini katika zama hizo waumini watakuwa na izza, hadhi na utukufu; na makafiri na madhalimu watakuwa katika hali ya unyonge na udhalili.
Darsa yetu hii inahatimishwa na aya ya 84 na 85 ambazo zinasema:


حَتَّى إِذَا جَاؤُوا قَالَ أَكَذَّبْتُم بِآيَاتِي وَلَمْ تُحِيطُوا بِهَا عِلْمًا أَمَّاذَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ


Hata watakapo fika, atasema (Mwenyezi Mungu): Je! Nyinyi si mlizikanusha Ishara zangu pasipo kuzijua vyema? Au mlikuwa mkifanya nini?


وَوَقَعَ الْقَوْلُ عَلَيْهِم بِمَا ظَلَمُوا فَهُمْ لا يَنطِقُونَ


Na kauli itawaangukia juu yao kwa vile walivyo dhulumu. Basi wao hawatasema lolote.


Aya zilizotangulia zilizungumzia Raj'at, yaani kurudi tena duniani viongozi wa waumini na makafiri zama za mwisho wa dunia. Kama tulivyoeleza, Raj'at inahusu kufufuliwa baadhi ya watu kabla ya tukio la Kiyama. Na kutokana na Hadithi inadhihirika kwa uwazi kwamba Raj'at ni moja ya hatua za kuelekea Siku ya Kiyama japokuwa kudhihiri kwake hakutoendelea hadi kuifikia Siku ya Kiyama. Wakati huo aya na ishara za Mwenyezi Mungu zitadhihiri kwa maana yake kamili. Watu ambao walikuwa wa mbele katika imani au ukafiri, yaani waliokuwa mawalii au maadui wa Mwenyezi Mungu, watafufuliwa na kurudishwa duniani ili ije ipambanuke baina ya haki na batili.
Aya tulizosoma zinasema: baada ya kufufuliwa viongozi wa shirki na ukafiri Mwenyezi Mungu atawahoji watu hao ilikuwaje mlizikadhibisha aya za vitabu vya mbinguni pamoja na miujiza ya Mitume? Hali ya kuwa elimu yenu haba kabisa mliyokuwa nayo haikuwa na uwezo wa kuzikana aya na ishara hizo. Isitoshe ni kwamba mlikuwa mkifanya mambo mengi maovu ambayo yalitokana na kukufuru na kuzikana kwenu aya za Mwenyezi Mungu. Ni wazi kwamba wakati watu hao watakapoziona ishara na miujiza ya wakati wa Raj'at, hawatokuwa na njia ya kupinga na kukana haki na hawatoweza kutoa udhuru na kisingizio wala kuwa na chochote cha kusema. Matokeo yake watakubali kuwa wanaadhibiwa kutokana na dhulma waliyozifanyia aya na Mitume ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika zama za mwisho wa dunia yatajitokeza madhihirisho ya Kiyama ambapo makundi ya watu wema maalumu na watu wabaya maalumu watasimama mbele ya mahakama ya Mwenyezi Mungu na mmoja wa waja wateule wa Allah atatoa hukumu kwa watu hao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tusikanushe na kukadhibisha kitu chochote bila ya kuwa na uelewa wa kutosha, kwa sababu tuwe na hakika tutasailiwa na kuulizwa kwa kufanya hivyo. Ni kwa sababu hiyo pia tunatakiwa imani na itikadi zetu zitokane na uelewa na msingi wa hoja za wazi na za yakini. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa adhabu kwa madhalimu Siku ya Kiyama ni jambo la hakika na lisilo na chembe ya shaka, na wao hawatokuwa na la kunena. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 679 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atusamehe madhambi yetu, atutakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)