Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 14:48

Sura ya An-Naml, aya ya 76-81 (Darsa ya 678)

Sura ya An-Naml, aya ya 76-81 (Darsa ya 678)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 678, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 76 hadi 79 ambazo zinasema:


إِنَّ هَذَا الْقُرْآنَ يَقُصُّ عَلَى بَنِي إِسْرَائِيلَ أَكْثَرَ الَّذِي هُمْ فِيهِ يَخْتَلِفُونَ


Hakika hii Qur'ani inawasimulia Wana wa Israili mengi wanayo khitalifiana.


وَإِنَّهُ لَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ


Nayo hakika ni Uwongofu na Rehema kwa Waumini.


إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُم بِحُكْمِهِ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ

Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao kwa hukumu yake, naye ni Mwenye nguvu, Mjuzi.


فَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ إِنَّكَ عَلَى الْحَقِّ الْمُبِينِ

Basi mtegemee Mwenyezi Mungu; hakika wewe uko kwenye Haki iliyo wazi.


Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowahutubu washirikina ambao walikuwa wakikadhibisha kujiri kwa Kiayama; na kwa kutoa visingizio mbalimbali wakawa wanaifanyia shere na stihzai imani juu ya kufufuliwa wafu na kulipwa thawabu au adhabu huko akhera. Aya hizi tulizosoma zinawazungumzia Mayahudi waliokuwa wakiishi eneo la Bara Arabu, ambao hawakuwa tayari kuiamini Qur'ani na Uislamu. Mayahudi hao walikuwa wakihitilafiana kuhusu Masihi na muokozi wa Aakhiru-Zzaman ambaye alikuwa ametajwa kwenye Kitabu chao cha Taurati, kama ambavyo wakitofautiana pia kuhusu baadhi ya hukumu za dini. Hivyo aya tulizosoma zinasema: Laiti kama wangekuwa wanaiamini Qur'ani kuwa ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu hitilafu zote hizo zingeondoka na yale mambo yote ya khurafa, uzushi na bid'a ambayo yalitiwa ndani ya dini za Uyahudi baada ya Nabii Musa (AS) na Ukristo baada ya Nabii Isa (AS) yangemalizika; na matokeo yake ni kwamba wangekuwa na dini safi ya kufuata na isiyo na ufanyaji wowote mambo kiutashi wala imani na itikadi yoyote potofu.
Kisha aya zinaendelea kwa kumhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW pamoja na waumini kwa kuwaambia: Katika kukabiliana na upinzani wa Ahlul Kitab nyinyi tawakalini kwa Mwenyezi Mungu na endeleeni kushikamana na njia mnayoifuata kwa kuifanya egemeo na tegemeo lenu elimu na nguvu zisizo na kikomo za Allah SW huku mkijua kwamba nyinyi mko katika haki; na haki ni yenye kudumu kwa kubakia imara na thabiti. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba miongoni mwa baraka za Qur'ani ni kutatua hitilafu za kifikra na za msingi za asili ya jambo. Qur'ani ni chachu ya umoja; na si baina ya Waislamu pekee, bali hata kwa Ahlul Kitab pia, ambao kama wataikubali na kuzifanya aya za kitabu hicho kitukufu kuwa marejeo yao wataweza kutatua hitilafu na tofauti zilizopo baina yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa uongofu ni neema kubwa kabisa ya kimaanawi ambayo Allah SW amewatunuku waja wake kutokana na rehma na uraufu wake kwao. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu ni moja ya masharti ya kufanikiwa mtu. Lakini pia kutawakali kwa Allah kunakuwa na maana iliyokusudiwa, kwa kufanya hivyo katika njia na jambo la haki tu, na si katika njia au jambo la batili.
Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 80 na 81 ambazo zinasema:


إِنَّكَ لا تُسْمِعُ الْمَوْتَى وَلا تُسْمِعُ الصُّمَّ الدُّعَاء إِذَا وَلَّوْا مُدْبِرِينَ


Kwa hakika wewe huwezi kuwasikilizisha wafu, wala kuwasikilizisha viziwi, wanapo kwisha geuka kwenda zao.


وَمَا أَنتَ بِهَادِي الْعُمْيِ عَن ضَلالَتِهِمْ إِن تُسْمِعُ إِلاَّ مَن يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا فَهُم مُّسْلِمُونَ


Wala huwezi kuwaongoa vipofu waache upotovu wao. Huwezi kuwasikilizisha ila wale wanao ziamini Ishara zetu; na hao ndio wat'iifu.


Baada ya aya zilizotangulia kueleza kuwa Qur'ani ni haki iliyo dhahiri kabisa, aya tulizosoma hivi punde zinasema, kuipinga kwao Qur'ani hao wapinzani na kukataa kuikubali haki kunatokana na upofu wa nyoyo zao, na si kwamba Qur'ani ni kitabu kisichoweza kukubalika. Mtu ambaye amejawa na inadi, ukaidi, taasubi na ufuataji mambo kibubusa huwa mithili ya mfu ambaye maneno yoyote yale hayawezi kuwa na athari kwake; au huwa mfano wa mtu hai lakini kiziwi, ambaye hasikii chochote aambiwacho bali huendelea na safari zake. Ni kawaida kwamba kama mtu atamwita mtu asiyeona aliyempa kisogo na akiwa mbali huwa hamsikii. Ni masikitiko kwamba makafiri wengi wako mithili ya viziwi na vipofu kwa sababu wanajifungia wenyewe njia zote za kuweza kuitambua haki na ukweli na hivyo kuzikosesha nafsi zao kuusikia na kuuona wito wa haki wanaofikishiwa. Ni wazi kwamba watu watakaoweza kunufaika na uongofu wa Qur'ani na wito wa haki wa Bwana Mtume Muhammad SAW ni wale ambao, kwanza, ni wanyenyekevu mbele ya haki; na pili wawe na imani ya kweli kwamba aya za Mwenyezi Mungu ni maneno ya kweli na ya haki. Kwa maneno mengine, mtu anaweza kunufaika na uongofu wa Qur'ani ikiwa hakutakuwepo na vizuizi vya utambuzi vya kumzuia asiikubali haki. Mara nyingi, vizuizi hivyo huwa vinahusiana na fikra na nafsi za watu ambapo kutokana na misimamo wanayokuwa nayo tokea hapo kabla, iliyojengeka juu ya msingi wa kuiga na kufuata mambo waliyoyarithi kwa waliowatangulia, au kwa sababu ya taasubi za kikaumu na kikabila huwa hawako tayari kusikiliza maneno ya haki; na au kama watayasikiliza, basi huyatolea tafsiri nyengine kutokana na ufahamu potofu walionao. Kwa maana hiyo basi, tatizo haliko katika asili ya ujumbe wa Mitume au kutowezekana kukubalika ujumbe huo; bali tatizo la msingi ni taasubi, inadi na ukaidi wa wale wanaoukanusha ujumbe huo. Ikiwa moyo wa mtu utakuwa umekufa, ukawa hauko tayari kuikubali haki, neno lolote lile la haki halitokuwa na taathira kwa mtu huyo. Ni sawa na kuuunganisha umeme na tungi la taa lililoungua; kwani tungi hilo halitoweza kuwaka abadan! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mafunzo ya Qur'ani, uhai na umauti vina hali ya uhai na mauti ya kimaumbile na kimaada, na pia uhai na mauti ya kimaanawi. Kwa mtazamo wa Qur'ani, watu ambao hawataki kuyasikiliza maneno ya haki; au hata kama watayasikia hawaathiriwi nayo, hao ni wafu na wasio na uhai japokuwa kidhahiri ni watu wanaoishi. Kinyume na watu hao, kwa mujibu wa Qur'ani, watu walioikubali haki, wakaamua kujitoa mhanga nafsi zao na kufa shahidi katika njia ya haki, hao ni watu waliohai na wanaendelea kuruzukiwa na Mwenyezi Mungu ijapokuwa kidhahiri hawako tena pamoja na watu walio hai duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na masikio, macho na akili tu hakutoshi. Muhimu zaidi ni kuwa na moyo wa kuikubali haki; kwani bila ya kuwa na moyo huo mtu huyakanusha hata yale anayoyasikia na kuyaona kwa macho yake, au huyafasiri kwa namna potofu na isiyo sahihi. Mtu aliyelala, wakati anaposikia sauti ya kumwamsha huamka; lakini yule ajifanyaye tu amelala, hata tukimpigia makelele yoyote ya kumwamsha hatoamka. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 678 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutuwezesha kuifuata, na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)