Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 14:45

Sura ya An-Naml, aya ya 70-75 (Darsa ya 677)

Sura ya An-Naml, aya ya 70-75 (Darsa ya 677)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 677, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 70 hadi 72 ambazo zinasema:


وَلا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلا تَكُن فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ


Wala usiwahuzunukie wala usiwe katika dhiki kwa sababu ya hila zao wanazo zifanya.


وَيَقُولُونَ مَتَى هَذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ


Na wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa mnasema kweli?


قُلْ عَسَى أَن يَكُونَ رَدِفَ لَكُم بَعْضُ الَّذِي تَسْتَعْجِلُونَ


Sema: Huenda karibu ikakufikieni sehemu ya yale mnayo yahimiza.


Katika darsa iliyopita tuliona kwenye aya ya 69 jinsi Qur'ani ilivyowataka wapinzani wa Bwana Mtume SAW watembee katika pembe mbalimbali za dunia ili waweze kujionea zilivyoangamizwa staarabu na tamaduni zilizopita na kupata ibra kutokana na hatima iliyowafika watu hao. Amma aya hizi tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW kwa kumwambia: Usihuzunike kwa sababu ya hao washirikina kuendelea kufanya inadi na ukaidi na kuamua kila mara kusimama na kuipinga haki; wewe umeshatimiza wajibu wako na wito wa haki umeshawafikishia; na kimsingi ni kwamba Mwenyezi Mungu amewaumba wanadamu na kuwapa hiyari na uhuru wa kuchagua; hakutaka waiamini haki kwa nguvu. Bila ya shaka wao wapinzani wa haki sio tu hawako tayari kuamini, lakini wanapanga na kufanya njama kila mara ili kuzuia wito na ulinganiaji wako; lakini Sisi tutazizima njama na hila zao hizo; kwa hivyo wewe usiwe na wasiwasi kwa hilo. Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria maneno ya washirikina na kueleza kwamba: wao wanamwambia Mtume na waumini kwa shere na stihzai kwamba hii ahadi mnayotoa ya kusema kwamba sisi tutafikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu duniani na akhera, kwa nini hiyo adhabu haitushukii? Sisi tunaingojea. Allah SW akawajibu kwa kuwaambia: msiwe na pupa ya hilo, kwani karibuni hivi itakufikeni hiyo adhabu mnayoifanyia shere na stihzai. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwahurumia na kuwaonea uchungu waliopotea kuna kiwango na mpaka. Inatakiwa mtu ajitahidi kadiri awezavyo kuwaelimisha waliopotoka, lakini kama wataifahamu haki na wakaamua kuendelea kung'ang'ania kufuata batili, hapo tena inabidi awaache kama walivyo na wala asiwasikitikie tena. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa muhula ambao Allah anawapa makafiri na madhalimu usitufanye tukadhani kwamba Yeye Mola amewasahau; bali tujue kuwa kama si leo ni kesho, watapata ikabu na adhabu ya maovu waliyofanya.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 73 hadi 75 ambazo zinasema:


وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لا يَشْكُرُونَ

 

Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye fadhila kwa watu, lakini wengi wao hawashukuru.


وَإِنَّ رَبَّكَ لَيَعْلَمُ مَا تُكِنُّ صُدُورُهُمْ وَمَا يُعْلِنُونَ


Na hakika Mola wako Mlezi anayajua yanayo ficha vifua vyao na wanayo yatangaza.


وَمَا مِنْ غَائِبَةٍ فِي السَّمَاء وَالأَرْضِ إِلاَّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ


Na hakuna siri katika mbingu na ardhi ila imo katika Kitabu kinacho bainisha.


Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia na kueleza kwamba:"Ikiwa Mwenyezi Mungu haharakishi kukuteremshieni adhabu si kwamba Yeye si mweza wa hilo au amesahau au ameghafilika nalo, bali hiyo inatokana na rehma na uraufu wa Allah kwa waja wake, ili kwa kuwapa muhula huo asaa wataweza kutubia kwa makosa na madhambi waliyofanya. Lakini kwa masikitiko ni kwamba wao si washukurivu kwa rehma hizo adhimu za Mola; na badala ya kutubia wanaendelea kufanya maovu na maasi. Yamkini pia madhalimu wakawa wanadhani kwamba Allah SW hawafanyi chochote kwa sababu hana habari za wanayoyafanya wala uwezo wa kuvivunja vitimbi, nia na njama zao hatari. Hali ya kuwa Yeye Allah ni Mjuzi, si wa yale tu yaliyomo kwenye batini zao wao, bali yaliyomo pia kwenye vifua na batini za viumbe na vitu vingine vyote vilivyoko kwenye ulimwengu wa uumbaji, na kwa kweli hakuna chochote kilichofichikana mbele yake Yeye Mola. Na sababu ni kuwa katika mfumo wa ulimwengu wa uumbaji, kuna loho inayohifadhi kila kitu, yaani Lauhul-mahfudh, ambayo ndiyo hiyo elimu mutlaki na isiyo na ukomo ya Mola Muumba; na mambo yote ya ulimwengu yamewekwa na kuhifadhiwa humo. Miongoni mwa mafunzo tuanayopata kutokana na aya hizi ni kwamba muhula wa fursa tunaopewa na Allah tuuthamini sana na kuutumia kwa kutubia na kujirekebisha kwa tuliyoyafanya huko nyuma. Na si kuuchukulia kuwa ni hoja ya kuonyesha kwamba tuyafanyayo ni ya sawa na ndiyo maana hatufikwi na adhabu ya Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwelewa wa ya siri na ya dhahiri. Yeye anayajua mambo ya ghaibu ya mbinguni na ardhini, yafanywayo kwa siri na mwanadamu, wakati wa kutokea Kiyama pamoja na mengine yaliyofichikana. Aidha tujue kwamba ulimwengu mzima uko chini ya uangalizi wake Mola na kila jambo lake linafanyika kwa hisabu na ratiba maalumu. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba sio tu tunahitaji kujirekebisha tabia na matendo yetu, bali kuna ulazima pia wa kurekebisha na kuziweka safi nia na dhamira zetu. Badala ya kuwatakia mabaya wenzetu, tuwatakie mema na ya kheri kwa sababu Allah SW ni Mjuzi wa yaliyomo ndani ya nafsi zetu; na rehma na fadhila zake kwetu zinatokana na nia zetu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 677 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atuwezeshe kuifuata na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)