Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 14:42

Sura ya An-Naml, aya ya 64-69 (Darsa ya 676)

Sura ya An-Naml, aya ya 64-69 (Darsa ya 676)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 676, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 64 ambayo inasema:


أَمَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَمَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاء وَالأَرْضِ أَإِلَهٌ مَّعَ اللَّهِ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ


Au ni nani anaye uanzisha uumbaji, kisha akaurejesha? Na nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Je! Yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Sema: Leteni hoja zenu kama nyinyi ni wakweli.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Qur'ani tukufu iliwageukia washirikina na kuwauliza: maabudu na miungu mnayoiabudu nyinyi ndio bora au Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumba wa viumbe na anayeziendesha kwa hekima na tadbiri yake mbingu na ardhi pamoja na viumbe vingine vyote vikubwa na vidogo? Aya tuliyoisoma inaendelea na maudhui hiyo kwa kuuliza suali jengine, nalo ni kwamba, je hawa maabudu na miungu wenu ndio bora au Mwenyezi Mungu mmoja ambaye sio tu ndiye chimbuko la uumbaji lakini Siku ya Kiyama atavifufua tena viumbe hivyo na marejeo yao wote ni kwake Yeye? Na ni Yeye Mola huyo ndiye anayedhamini mahitaji ya viumbe na akakiwekea kila kiumbe njia ya kupatia riziki yake. Pamoja na hayo kama mnadhani kuwa ghairi ya Mungu mmoja wa haki, kuna miungu wengine wanaomsaidia Yeye katika uumbaji au katika tadbiri na uendeshaji masuala ya ulimwengu, mtajeni basi na toeni hoja zenu juu ya hilo kwa njia wadhiha na ya kimantiki. Moja ya sifa maalumu za Qur'ani katika kukabiliana na wapinzani ni kuwataka watoe hoja na burhani, suala ambalo limeashiriwa katika aya kadhaa za kitabu hicho kitukufu. Qur'ani, kama ambavyo hubainisha mafundisho yake kuhusiana na asili ya uumbaji na ufufuo wa viumbe kwa uwazi na kwa mantiki, inatarajia wapinzani nao watoe hoja zao kwa mantiki na kuacha kuzungumza mambo kwa dhana na kujiepusha na utumiaji lugha ya istihzai, udunishaji na utoaji vitisho dhidi ya waumini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba tuwe na insafu katika kuamiliana na wapinzani, na kama watatoa hoja na burhani za kimantiki tuzikubali. Na isiwe kwamba kwa kuwa aliyesema jambo fulani ni adui, basi tusilikubali. Kwa sababu Uislamu ni dini ya mantiki na burhani; na inawataka wapinzani wake, nao pia watoe burhani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu ametukadiria na kutupangia riziki na yote tunayoyahitajia sisi viumbe wake wote. Hitajio la hewa, mwangaza na mvua linakidhiwa kutokea angani na mahitaji ya anuai za vilaji, vyakula, matunda na vinywaji vinapatikana kutokea ardhini.
Zifuatazo sasa ni aya za 65 na 66 ambazo zinasema:


قُل لّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ الْغَيْبَ إِلاَّ اللَّهُ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ


Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Wala wao hawajui lini watafufuliwa.


بَلِ ادَّارَكَ عِلْمُهُمْ فِي الآخِرَةِ بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ مِّنْهَا بَلْ هُم مِّنْهَا عَمُونَ


Bali ujuzi wao wa kuijua Akhera umefikia kikomo. Bali wao wamo katika shaka nayo. Bali wao ni vipofu nayo.


Washirikina, kwa sababu ya kukanusha kwao Kiyama na kutoamini kufufuliwa viumbe baada ya kufa, kila mara walikuwa wakiwauliza Mitume wao suali hili, kwamba Kiyama kitatokea lini? Na kwa kuwa hawakuwa wakiwapa jawabu ya suali hili, walikuwa wakiwaambia: Basi nyinyi wenyewe pia hamna uhakika wa kutokea kwake. Aya hizi tulizosoma zinatoa jawabu ya suali hilo na utata uliokuwa ukizushwa na wapinzani kwa kusema: baadhi ya mambo yanamhusu Mwenyezi Mungu tu; hata malaika na Mitume hawajui habari zake. Lakini kutojua wakati wa kutokea tukio si hoja na sababu ya kuonesha kuwa halitojiri. Ni kama ambavyo hakuna mtu yeyote anayejijua lini ataondoka duniani, lakini watu wote wanajua kuwa iko siku watakufa na hakuna njia ya kuyakwepa mauti.
Kwa hivyo kujiri kwa Kiyama kuko vivyo hivyo pia. Kiyama ni jambo la hakika kabisa ambalo hakuna ajuaye wakati wa kujiri kwake; lakini hiyo si sababu ya kulikana au kuwa na shaka nalo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutia shaka juu ya imani na itikadi za dini ni moja ya mbinu za wakanushaji wa itikadi za dini ikiwemo Kiyama. Kwa hivyo Waislamu wanatakiwa watoe hoja za mantiki kukabiliana na mbinu hizo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa imani juu ya maadi na kufufuliwa, kama ilivyo imani juu ya asili ya uumbwaji ni miongoni mwa mambo ya ghaibu ambayo hayawezi kufahamika kwa kutegemea hisi tano za mwanadamu, bali ni akili tu ndiyo inayoweza kulithibitisha hilo kwa hoja na burhani za kimantiki.
Aya za 67 hadi 69 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:


وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَئِذَا كُنَّا تُرَابًا وَآبَاؤُنَا أَئِنَّا لَمُخْرَجُونَ


Na wakasema walio kufuru: Tutakapo kuwa mchanga, sisi na baba zetu, hivyo kweli tutakuja tolewa?


لَقَدْ وُعِدْنَا هَذَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا مِن قَبْلُ إِنْ هَذَا إِلاَّ أَسَاطِيرُ الأَوَّلِينَ


Haya haya tuliahidiwa sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni ngano za watu wa kale.

 

قُلْ سِيرُوا فِي الأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُجْرِمِينَ

 

Sema: Nendeni katika ardhi, na tazameni ulikuwaje mwisho wa waovu.


Zikiendeleza maudhui iliyoashiriwa na aya zilizotangulia ambazo zilieleza kwamba moja ya sababu zinazowafanya wapinzani wa haki wawe na shaka na kujiri kwa Kiyama ni kutotangazwa na Mitume wakati wa kujiri tukio hilo adhimu, aya hizi tulizosoma zinasema: katika kutoa hoja ya kuthibitisha sababu ya shaka yao hiyo, watu hao wanaashiria nukta hii, kwamba katika zama zote za historia, Mitume wote wamekuwa wakiahidi kwamba Siku ya Kiyama itajiri, hali ya kuwa wazee wetu waliotangulia, wote wameshageuka mchanga, na kila sehemu ya viwiliwili vyao imeshaparaganyika na kutawanyika, lakini ahadi hiyo haijathibiti hadi leo. Kwa hivyo hata na sisi pia tutakapokufa tutageuka mchanga na hakuna kitakachosalia katika viwiliwili vyetu hata tuje kuwa hai tena. Jibu la Qur'ani tukufu kwa watu hao liko wazi kabisa, nalo ni kwamba: Kwanza nyinyi nyote asili yenu mlikuwa udongo na mmeumbwa kutokana na udongo, kwa hivyo hakuna kizuizi chochote cha kukufanyeni msiwe hai tena katika ulimwengu mwengine baada ya kugeuka udongo. Lakini pili, ubishi na ukaidi wenu dhidi ya maneno ya haki ya Mitume utakufanyeni mfikwe na adhabu ya papa hapa duniani kama iliyozipata kaumu nyingi zilizopita. Kaumu ambazo baadhi yao ziko karibu na nyinyi kwa zama na mahala, kiasi kwamba kwa kuipitia historia kidogo tu mtaweza kujua nini ulikuwa mwisho wa watu wa kaumu hizo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuvielezea vitabu vya mbinguni kuwa ni ngano za kale ni mwenendo wa wapinzani wa haki katika zama zote za historia. Kwa masikitiko ni kwamba hata leo hii pia kuna baadhi ya watu, kutokana na ujinga na kutoelewa, na kuna baadhi yao kwa uelewa kamili, wanayatuhumu mafundisho matukufu ya mbinguni kuwa ni ngano za kale. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Qur'ani imewataka watu waipitie historia ya waliotangulia kwa kufanya safari za kutalii sehemu mbalimbali za dunia ili kujionea hatima na mwisho wa madhalimu. Kwa sababu kutalii athari zilizobaki za watu madhalimu, kwenyewe kunamjenga na kumpanua mawazo mtu. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba kuna ulazima wa kuhifadhi athari za waliotangulia kwa ajili ya ibra na mazingatio kwa wanaofuatia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 676 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atusamehe madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)