Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 14:40

Sura ya An-Naml, aya ya 61-63 (Darsa ya 675)

Sura ya An-Naml, aya ya 61-63 (Darsa ya 675)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 675, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 61 ambayo inasema:


أَمَّن جَعَلَ الأَرْضَ قَرَارًا وَجَعَلَ خِلالَهَا أَنْهَارًا وَجَعَلَ لَهَا رَوَاسِيَ وَجَعَلَ بَيْنَ الْبَحْرَيْنِ حَاجِزًا أَإِلَهٌ مَّعَ اللَّهِ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لا يَعْلَمُونَ


Au ni nani yule aliye ifanya ardhi mahali pa kutua, na akajaalia ndani yake mito, na akaiweka milima? Na akaweka baina ya bahari mbili kizuwizi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali wengi wao hawajui.


Katika darsa iliyopita tuliona katika aya ya 60 ya sura hii jinsi Qur'ani tukufu ilivyovunja hoja za fikra potofu za washirikina na waabudu masanamu kwa kutaja mifano ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu SW, na kuwauliza watu hao: Vitu hivi vya kimaumbile vimeumbwa na miungu yenu au na Mungu mmoja wa haki? Aya hii tuliyosoma pia inaendeleza maudhui hiyo kwa kuashiria mifano mingine ya vitu vya maumbile ambavyo ni madhihirisho ya qudra, uwezo na hekima ya Allah katika uumbaji wa ardhi, mazingira na suhula za kuwezesha kuishi ndani yake na kusema: Mwenyezi Mungu ameifanya ardhi iwe thabiti na tulivu ili nyinyi muweze kupata raha na utulivu. Kama tutakaa na kutafakari juu ya matetemeko ya ardhi yanayotokea kila baada ya muda katika pembe moja au nyengine ya dunia na mitikisiko yake mikubwa inayosababisha maafa na madhara ya kila aina ndipo itakapotubainikia kwamba kutulia kwa ardhi ni moja ya neema kubwa za Allah kwa wakaazi wa sayari hii ya dunia.
Kuwepo kwa milima, mito na bahari za maji baridi na ya chumvi ndivyo vinavyowezesha kuwepo uhai na maisha kwa ajili ya wanadamu. Na ushahidi wa hayo ni kudhihiri kwa tamaduni na staarabu kubwa kubwa za watu kando ya maeneo ya mito na mabonde mbalimbali. Kama ni hivyo, inakuwaje washirikina wanayafanya masanamu yasiyo na uhai kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji au tadbiri na uendeshaji wa masuala ya ulimwengu huu wenye adhama? Kuna sababu nyengine, ghairi ya kushindwa wao kutafakari juu ya jambo hili na kuelewa ukweli wake? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ardhi imekuwa tulivu kwa wakaazi wake kiasi cha kuwafanya wanadamu wadhani kwamba ardhi ni kitu thabiti kisicho na harakati yoyote. Hali ya kuwa sayari hii ya dunia inajizunguka yenyewe na kulizunguka jua pia kwa kasi, lakini kwa kuwa harakati yenyewe inafanyika kwa mwendo thabiti, wa kasi isiyobadilika na yenye nidhamu maalumu, hakuna awezaye kuuhisi mwendo huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa chanzo halisi cha ukafiri na shirki ni kukosa uelewa na utambuzi sahihi wa ukweli na hakika ya mambo ambao baadhi ya wakati hufanywa kwa makusudi au hutokana na ukaidi, kwa mtu kutotaka kuifahamu na kuikubali haki.
Ifuatayo sasa ni aya ya 62 ambayo inasema:

 

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاء الأَرْضِ أَإِلَهٌ مَّعَ اللَّهِ قَلِيلا مَّا تَذَكَّرُونَ


Au ni nani yule anaye mjibu aliye dhikika pale anapo mwomba, na akaiondoa dhiki, na akakufanyeni nyinyi warithi wa ardhi? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayo yazingatia.


Aya hii inaashiria moja ya madhihirisho ya kuwepo Mwenyezi Mugu katika maisha ya wanadamu wote na kueleza kwamba wakati mnapokuwa mmetanzwa na kutingwa na mabalaa, misukosuko na matatizo; na milango yote ya auni na msaada ikawa imefungwa mbele yenu, ni nani mnayemuelekea na kumkimbilia? Katika hali kama hiyo masanamu au wengineo wanaweza kukufaeni kwa lolote? Au ndani ya nafsi zenu mnaihisi nguvu ambayo ndiyo yenye uwezo wa kuyatatua matatizo na masaibu yenu, na ambayo mnaiomba kwa ikhlasi na kutarajia msaada wake?
Katika aya ya 22 ya Suratu Yunus imani hii ya kifitra na kimaumbile ya mwanadamu juu ya Mwenyezi Mungu imeashiriwa kwa kuelezwa kwamba wakati mnapokuwa mumeabiri merikebuni kisha mkakumbwa na dhoruba ya mawimbi makali ya bahari kutoka kila upande, na maisha yenu yakawa hatarini, ni nani ghairi ya Allah mnayemwomba kwa ikhlasi na unyenyekevu, na ni nani mwengine asiyekuwa yeye mnayemtegemea akuokoeni?
Baadhi ya watu wenye itikadi za kimaada na wakadhibishaji wa dini, wanadai kuwa imani ya kuwepo kwa Mungu ni matokeo ya hofu na kutingwa mwanadamu; na kwa kutumia kisingizio hicho wanakana asili ya kuwepo Mola Muumba. Kwa imani yao wao, ni kwamba wakati mwanadamu anapokabiliwa na msiukosuko na matukio mazito, kwa kujihisi ametingwa na hana uwezo wa kuyakabili, woga, hofu na ujinga humfanya akimbilie kuomba msaada, kwa kitu chenye uwezo anachokitasawari akilini mwake. Lakini ukweli ni kwamba waja waumini hawamuelekei na kumtegemea Mwenyezi Mungu wakati wa hatari na hofu tu, bali wanamwamini Allah katika hali zote za maisha yao, na Yeye ndiye tegemeo na marejeo yao. Ile hali ya hofu na kuhisi kutingwa huondoa utandu wa mghafala mbele ya macho ya moyo wa mwanadamu na kumfanya asione chochote mbele yake isipokuwa Yeye Mola na kujihisi ni mhitaji wa auni na msaada wake. Mfano wake ni sawa kabisa na mtoto kwa wazee wake ambao anawakubali katika hali zote kuwa ni wazazi wake, lakini ni pale anapotingwa na kupatwa na shida nzito ndipo huwaendea na kuwaomba msaada. Sasa je tuseme baba na mama ni matokeo ya mahitaji ya mtoto wao au hofu yake inayotokana na hatari zinazomkabili? Au vitu hatarishi vinamfanya mtoto afahamu kwamba katika hali ngumu ya shida na misukosuko ni wazazi wake wawili yaani baba na mama ndio wanaomshika mkono ili kumfaa na kumsaidia? Alaa kulli hal, wakati wanadamu wanapokuwa na yakini kwamba hakuna nguvu yoyote ya kuyaitika mayowe yao ya kuomba msaada, na wakawa wamekata tamaa na kupoteza matumaini kikamilifu, hapo ndipo wanapohisi kutokea ndani kabisa ya nafsi zao kuwa kuna nguvu ya ghaibu isiyoonekana ya kuitegemea, ambayo ndiye Allah SW. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba miongoni mwa njia za kumjua Mwenyezi Mungu ni hisi ya kutegemea nguvu maalumu ya uokozi pale mtu anapotingwa, akadhikika mpaka akawa hana uwezo tena wa kufanya chochote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu amemtawalisha ardhi mwanadamu, akampa uwezo wa kuyamiliki maumbile na kuzitumia kwa faida na manufaa yake suhula zilizomo ndani yake.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 63 ambayo inasema:


أَمَّن يَهْدِيكُمْ فِي ظُلُمَاتِ الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَن يُرْسِلُ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ أَإِلَهٌ مَّعَ اللَّهِ تَعَالَى اللَّهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ


Au ni nani yule anaye kuongozeni katika giza la bara na bahari? Na ni nani yule azipelekaye pepo kuleta bishara kabla ya rehema zake? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ametukuka Mwenyezi Mungu na yale wanayoyashirikisha Naye.


Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyotangulia kwa kutumia tena lugha ya suali na kusema: Mnapokuwa katika safari zenu za nchi kavu na baharini wakati wa usiku, vipi mnaweza kutambua njia ya kufuata? Zile nyota ambazo ndiyo dira ya kukuongozeni wakati wa usiku zimeumbwa na mnavyoviabudu visivyo na uhai wala hisi au zimeumbwa na Allah, Mungu mmoja tu wa haki!?
Pepo, ambazo ni wenzo wa kusukuma mawingu hadi maeneo ya mbali ya ardhi na kusababisha kunyesha mvua, zinavuma na kuifanya kazi hiyo kwa matakwa na irada ya nani mwengine ghairi ya Allah SW? Inakuwaje basi mnayaomba pamoja na Mwenyezi Mungu Mweza na Aliyetukuka masanamu hayo duni yasiyo na thamani na kuitakidi kuwa miungu hiyo bandia ina athari katika majaaliwa yenu na majaaliwa ya ulimwengu? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba vitu vya maumbile vyenye mfungamano wa pamoja na nidhamu maalumu, vilivyoko angani na ardhini ni ushahidi bora na tosha kabisa wa kuthibitisha kuwepo nidhamu na mpangilio maalumu katika mfumo wa ulimwengu wa maumbile; na kazi kubwa kabisa na adhimu kama hiyo haiwezi kufanywa na yeyote ghairi ya Muumba wa ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa hakuna mtu yeyote wala kitu chochote kinachostahiki kuwa na hadhi ya jina lake kuwekwa katika nafasi sawa na jina la Mwenyezi Mungu. Yeye Allah ndiye aliyetukuka na ndiye wa juu zaidi ya vyote vilivyoko katika ulimwengu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 675 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa na maarifa ya yakini ya kumtambua Yeye yatakayozidisha imani ndani ya nyoyo zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)