Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 14:35

Sura ya An-Naml, aya ya 57-60 (Darsa ya 674)

Sura ya An-Naml, aya ya 57-60 (Darsa ya 674)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 674, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 57 na 58 ambazo zinasema:


فَأَنجَيْنَاهُ وَأَهْلَهُ إِلاَّ امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَاهَا مِنَ الْغَابِرِينَ


Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe; tukamkadiria katika walio baki nyuma.


وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِم مَّطَرًا فَسَاء مَطَرُ الْمُنذَرِينَ


Na tukawanyeshea mvua. Ni mbaya kweli kweli hiyo mvua ya walio kwisha onywa.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa badala ya watu wa kaumu ya Nabii Lut kutafakari na kuzingatia maneno ya Mtume wao huyo, na kuacha amali chafu ya liwati waliyokuwa nayo, walitoa vitisho dhidi yake na kumwambia, madamu hutaki kusikilizana na sisi bali unatuudhi na kutubughudhi tutakufukuza katika mji wetu huu. Lakini pia wakimwambia kwa kejeli na istihzai kwamba: Kama unataka kuwa mtakasifu ondoka nje ya mji wetu usije ukapatwa na adhabu itakayotusibu sisi. Aya tulizosoma zinasema: baada ya Mwenyezi Mungu kutimiza dhima kwa kaumu ya watu hao wakaidi na mafasiki aliwateremshia adhabu yake, baada ya kumueleza Mtume wake Lut (AS) kwamba kabla ya kuteremka adhabu ondoka mjini hapo pamoja na waliokuamini ili msije mkapatwa na adhabu hiyo. Tab'an kwa kuwa mke wa Nabii Lut alikuwa akitumiwa na wapinzani wa haki kuwapelekea habari za nyumbani kwa Mtume huyo, na yeye pia aliingia kwenye kundi la walioshukiwa na adhabu na akaangamia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuridhia dhambi inayofanywa na watu na kutoa ushirikiano kwa waovu, kunahesabika kuwa ni dhambi na kunamstahikisha mtu adhabu mbele ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika dini ya Mwenyezi Mungu amali za mtu ndio kipimo si ujamaa na nasaba yake. Mke wa Nabii Lut (AS) na mtoto wa Nabii Nuh (AS) walikuwa watu wa karibu mno na Mitume hao wa Allah lakini walifikwa na adhabu. Kinyume chake, mke wa taghuti Firauni akawa mja wa peponi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba taqwa na uchamungu hapa duniani humuokoa mtu na adhabu ya Mola.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 59 ambayo inasema:


قُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ وَسَلامٌ عَلَى عِبَادِهِ الَّذِينَ اصْطَفَى آللَّهُ خَيْرٌ أَمَّا يُشْرِكُونَ


Sema: Alhamdu Lillahi! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu! Na amani ishuke juu ya waja wake alio wateuwa. Je! Mwenyezi Mungu ni bora, au wale wanao washirikisha Naye?


Baada ya kuzungumzia habari za Mitume watano wa Allah aya hii ya 59 ya Suratun Naml inamhutubu Bwana Mtume SAW na kumwambia: Inapasa kumshukuru na kumhimidi Mwenyezi Mungu ambaye amewaondoa waovu na waharibifu katika ardhi na kuisafisha ardhi kwa kuliondoa doa la uchafu wa uwepo wa viumbe hao. Aidha inatakiwa tuwatakie rehma na amani Mitume na mawalii wa Allah, kwa sababu wao ni waja wateule wa Mwenyezi Mungu na walifanya jitihada na hima kubwa kwa ajili ya kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Kisha aya inaendelea kwa kuuliza: Je masanamu waliyokuwa wanayaabudu washirikina au utajiri na nguvu za mamlaka waliyokuwa nayo viliweza kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu? Kwa nini badala ya wao kumtegemea Allah wanaiendea miungu bandia na ya kubuni? Kwani hawakuona hatima na yaliyowapata watu wa kaumu zilizopita jinsi walivyoangamizwa papa hapa duniani? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba pamoja na kushukuru neema za Allah inapasa kuwaenzi na kuwatakia rehma waja wake wema, kwa sababu kuwaenzi na kuwatukuza waja hao wateule kuna taathira njema na chanya kwa mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mawalii wa Allah wako hai na zinawafikia na wanazipokea sala na salamu tunazowafikishia.
Tunaihatimisha darsa hii ya 674 kwa aya ya 60 ambayo inasema:


أَمَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ وَأَنزَلَ لَكُم مِّنَ السَّمَاء مَاء فَأَنبَتْنَا بِهِ حَدَائِقَ ذَاتَ بَهْجَةٍ مَّا كَانَ لَكُمْ أَن تُنبِتُوا شَجَرَهَا أَإِلَهٌ مَّعَ اللَّهِ بَلْ هُمْ قَوْمٌ يَعْدِلُونَ


AU NI NANI yule aliye ziumba mbingu na ardhi, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, na kwayo tukaziotesha bustani zenye kupendeza? Nyinyi hamna uwezo wa kuiotesha miti yake. Je! Yuko mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Bali hao ni watu walio potoka.


Sehemu ya mwisho ya aya iliyopita ilihoji kwa kuuliza: je Mwenyezi Mungu aliye Mweza ni bora au hao mnaowaitakidi kuwa ni washirika wake? Baada ya maelezo hayo, aya hii tuliyosoma inataja baadhi ya madhihirisho ya elimu, nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu ambao ndio sababu ya kupatikana neema mbalimbali katika ardhi na kuhoji: Je hao mnaowaabudu ndio walioumba mbingu na ardhi na ndio wanaokuteremshieni mvua? Je miungu yenu mnayoiabudu ndiyo iliyoleta bustani, konde na mashamba haya yaliyonawiri? Kwa nini mnaikengeuka haki na kufuata batili?
Aya hii wapenzi wasikilizaji na nyengine zinazofuatia zinawataka wanadamu watafakari juu ya uumbaji ambao ndio njia bora zaidi kwa watu wote ya kumtambua Mwenyezi Mungu. Kwa sababu mtu yeyote mwenye akili timamu anaelewa kwamba ulimwengu huu wenye adhama hauwezi kuwa umeumbwa na umetokana na sisi wanadamu, na wala hauwezi kuwa unaendeshwa kwa irada na matakwa yetu. Hivyo kama tutatafakari kidogo tu tutakiri kwamba kuna Muumba Muweza mutlaki ambaye ameuumba ulimwengu huu kwa elimu na hekima na kuuwekea mfumo wake nidhamu na utaratibu maalumu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kutafakari juu ya uumbaji ndio njia bora ya kumtambua Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tunaweza kuutambua uwezo mutlaki wa Allah katika uumbaji wa ulimwengu pale tutakapobaini kuwa sisi hatuna uwezo hata wa kuotesha mmea mmoja. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba uendeshaji wa kila kitu cha ulimwengu wa maumbile uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu SW, lakini hayo hufanyika kwa njia ya wasita na visababishi, kama ambavyo kuota na kuchipua kwa mimea hufanyika kwa kunyesha mvua. Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, ajizaje subira nyoyo zetu na aufanye mwema mwisho wetu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)