Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 12:05

Sura ya An-Naml, aya ya 50-56 (Darsa ya 673)

Sura ya An-Naml, aya ya 50-56 (Darsa ya 673)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 673, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 50 hadi 53 za sura hiyo ambazo zinasema:


وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ

Basi wakapanga hila, na Sisi tukapanga mipango yetu, na wao hawatambui.


فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهُمْ وَقَوْمَهُمْ أَجْمَعِينَ

Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa hila yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote.


فَتِلْكَ بُيُوتُهُمْ خَاوِيَةً بِمَا ظَلَمُوا إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ

Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo dhulumu. Hakika katika hayo kuna Ishara kwa watu wanao jua.


وَأَنجَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

Na tukawaokoa wale walio amini na walio kuwa wanamchamngu.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa baadhi ya wapinzani wa Nabii Saleh (AS) walikula njama ya kumuua Mtume huyo. Wakalishana kiapo kwamba wachague watu kutoka makundi tisa tofauti watakaoshirikiana kufanya uovu huo ili hatia ya mauaji ya Nabii Saleh isije ikampata mtu au kundi moja tu la wauaji hao. Walikuwa wakitaka wakati Nabii Saleh atakapokuwa yuko mbali na familia yake na wafuasi wake, akiwa amejitenga milimani peke yake na kushughulika na munajati na kunong'ona na Mola wake, ndipo wamshambulie na kumuua. Lakini kwa irada ya Allah mawe yaliporomoka kutoka juu mlimani alikokuweko Nabii Saleh (AS) na kuwaangamiza watu hao waliokuwa wamejibanza chini ya mlima ili kumvizia na kumdhuru Mtume huyo wa Allah. Aya zinaendelea kueleza kwamba wao walikuwa wakidhani kuwa njama waliyopanga itakuwa na tija na wataweza kumuua Nabii Saleh, lakini hawakujua kwamba Mola wa Saleh ni Mwenye nguvu zaidi yao na ni Mjuzi wa yote waliyoyapanga katika njama yao. Na si wale tu waliopanga njama hiyo waliangamizwa lakini kaumu yenyewe ya Thamud, ambayo iliridhia njama hiyo ya kumuua Mtume wa Allah, nayo pia ilishukiwa na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu na kuangamia. Tab'an mbele yake Yeye Mola, hesabu ya wenye hatia na wasio na hatia haziko sawa, hivyo kwa irada ya Allah SW wale waliokuwa wamemwamini Nabii Saleh walisalimika na kuokoka na adhabu hiyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ikiwa waumini watatekeleza wajibu wao, Mwenyezi Mungu ataizima kwa wakati njama ya makafiri dhidi yao na hatoruhusu makafiri wawe na nguvu juu yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kaida na utaratibu aliouweka Allah ni haki kushinda dhidi ya batili. Tab'an batili ina mapambo na marembo; na yamkini ikafanikiwa kidhahiri katika baadhi ya mambo, lakini mafanikio hayo si ya kudumu, kwa sababu batili ni kitu dhaifu na kisicho na mashiko ambacho mwisho wake ni kutoweka tu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba inapasa kuzihifadhi athari za kale zilizosalia kutoka kwa kaumu zilizopita ili ziwe funzo, ibra na mazingatio kwa wanaokuja. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa athari na faida za imani na taqwa hazihusiani na akhera tu; bali hata hapa duniani pia, watu wamchao Mwenyezi Mungu huona matunda ya amali zao, kama ambavyo malipo ya adhabu na ikabu kwa waovu na madhalimu hayatalipwa huko akhera tu. Bali wakati mwengine malipo ya maovu yao hulipwa hata hapa duniani pia.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 54 na 55 ambazo zinasema:


وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ وَأَنتُمْ تُبْصِرُونَ

Na Lut'i alipo waambia watu wake: Je! Mnafanya uchafu nanyi mnaona?


أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ شَهْوَةً مِّن دُونِ النِّسَاء بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ

Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio badala ya wanawake? Bali nyinyi ni watu mnao fanya ujinga!


Baada ya aya zilizopita kuzungumzia habari za Nabii Saleh (AS), aya tulizosoma zinaelezea kwa muhtasari yaliyojiri baina ya Nabii Lut (AS) na watu wa kaumu yake. Kabla ya sura hii ya An-Naml, habari za kaumu ya Nabii Lut zilisha zungumziwa katika sura kadhaa zilizotangulia, lakini kwa kuzingatia kuwa vitendo vichafu vya maingiliano ya kimwili ikiwemo liwati vimekuwepo katika zama mbalimbali za historia, Qur'ani tukufu imeashiria katika sehemu mbalimbali habari za kaumu ya Nabii Lut (AS) na kuwatanabahisha watu na mwisho mbaya wa kaumu hiyo ili uwe onyo na mazingatio kwa watakaofuatia. Aya hizi tulizosoma zinasema: Nabii Lut alikemea vikali mwenendo muovu na mchafu wa liwati uliokuwa umeozoeleka na kuenea baina ya wanaume wa kaumu yake na kuwaambia:"Wakati nyinyi mnaujua uovu wa mwenendo huu vipi mnafanyiana kitendo kichafu kama hiki? Nyinyi mnao wake zenu; sasa inakuwaje mnawaacha wao na kuwaendea wanaume wenzenu?" Ni wazi kwamba wakati waume wanapowaacha wake zao na kuwaendea wanaume wenzao, wake pia hutokwa na hamu na raghba ya waume zao, na wao pia kuamua kuwaendea wanawake wenzao. Na hali hii hudhoofisha na hatimaye kusambaratisha ndoa na familia na kusababisha talaka na kuachana vishamiri na kuzagaa katika jamii. Inasikitisha kuona kwamba katika dunia yetu ya leo inayojigamba kuwa ni ulimwengu ulioendelea na uliostaarabika maingiliano ya kimwili ya watu wa jinsia moja yanazidi kuenea. Na baya zaidi ni kwamba katika baadhi ya nchi za Magharibi, vitendo hivyo vichafu na vyenye kukinzana na fitra na maumbile ya mwanadamu vinatambuliwa rasmi na kuhalalishwa kisheria. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kupambana na maovu na matendo machafu yaliyoenea na kuzoeleka katika jamii ni miongoni mwa majukumu ya Mitume na warekebishaji wa jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hitajio la kukidhi matamanio ya kijinsia ni miongoni mwa mahitaji ya kimaumbile ya mwanadamu, lakini yanapasa yakidhiwe kwa njia halali na ya kisheria iliyoainishwa na Muumba mwenyewe wa ulimwengu, na si kwa njia zinazokengeuka njia ya maumbile ambazo husababisha matatizo na madhara chungu nzima kwa mtu binafsi na jamii kwa jumla. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba mwenendo potofu wa kukidhi matamanio ya kijinsia ukiwemo wa kungiliana kimwili watu wa jinsia moja ni alama ya ujinga, upumbavu na kutokuwa na akili, hata kama mambo hayo yatafanywa na watu watamaduni na waliotaalamika.
Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 673 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 56 ambayo inasema:


فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلاَّ أَن قَالُوا أَخْرِجُوا آلَ لُوطٍ مِّن قَرْيَتِكُمْ إِنَّهُمْ أُنَاسٌ يَتَطَهَّرُونَ


Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Wafukuzeni wafwasi wa Lut'i katika mji wenu. Maana hao ni watu wanao jitakasa.


Baada ya watu wafanya maovu wa kaumu ya Nabii Lut (AS) kuelezwa maneno ya mantiki na ya hoja madhubuti na Mtume wao huyo, ya kuwaonya na kuwapa indhari juu ya maovu wanayoyafanya, badala ya kuyakubali maneno yake ya haki walimhamakia Mtume wao, na kwa utovu mkubwa wa staha na heshima wakasema: Lazima Luti, ahli zake na wafuasi wake wasiokubaliana na sisi na wanaotulaumu na kutukosoa kila mara wafukuzwe katika mji huu ili asije akatokea tena mtu wa kutubughudhi na kutukemea katika mambo yetu. Naam, wakati madhambi yanapokithiri na kuzagaa, usafi na uchaji Mungu huonekana kuwa ni kosa; na adhabu yake ikawa ni kufukuzwa na kufungwa. Ni kama ilivyokuwa kwa ujana safi wa ucha Mungu wa Nabii Yusuf (AS), ambaye wakati alipokataa kuridhia matakwa ya watu waliotekwa na matamanio ya nafsi zao aliishia jela na kupitisha humo miaka mingi ya umri wake kwa kosa la kuwa mja msafi mwenye kumcha na kumuogopa Mola wake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba haijuzu kuyanyamazia madhambi na maovu. Inabidi yakemewe ili wafanya madhambi wasiweze kujifaragua. Ni lazima maovu yakatazwe hadharani hata kama haitopatikana tija na kumfanya mtu afukuzwe na kubaidishwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kaulimbiu za uhuru wa maingiliano ya kimwili yakiwemo ya watu wa jinsia moja ni aina ya fikra iliyokuwa nayo kaumu ya Nabii Luti, ambao walikuwa ni watu majahili na waliopotoka. Uhuru wa aina hiyo hauwezi katu kuwa alama ya ustaarabu na maendeleo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba mazingira hayamlazimishi mtu kufanya dhambi, kwa sababu walipo watu waovu na mafasiki wanaishi pia watu safi na wema ambao wanazilinda nafsi zao na machafu na maovu. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atulinde na kila aina ya maovu, makubwa na madogo, ya siri na ya dhahiri. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)