Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 12:04

Sura ya An-Naml, aya ya 45-49 (Darsa ya 672)

Sura ya An-Naml, aya ya 45-49 (Darsa ya 672)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 672, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 45 hadi 47 ambazo zinasema:


وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَى ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّهَ فَإِذَا هُمْ فَرِيقَانِ يَخْتَصِمُونَ

Na hakika tuliwapelekea kina Thamud ndugu yao Saleh kuwaambia: Muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi mara yakawa makundi mawili yanayo hasimiana.


قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلُونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ لَوْلا تَسْتَغْفِرُونَ اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mpate kurehemewa?


قَالُوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَ قَالَ طَائِرُكُمْ عِندَ اللَّهِ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تُفْتَنُونَ

Wakasema: Tuna mkosi nawe na wale walio pamoja nawe. Yeye akasema: Uaguzi wa mkosi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni watu mnao jaribiwa.


Tangu mwanzo wa sura hii ya An-Naml hadi aya yake ya 44 zimesimuliwa kwa muhtasari habari za maisha ya Manabii Musa, Daud na Suleiman (AS). Katika aya tulizosoma unazungumziwa ujumbe na wito wa Utume wa Nabii Saleh (AS) kwa watu wa kaumu yake ya Thamud, ambapo kutokana na kuwaonea uchungu mno watu wake hao Mtume huyo wa Allah aliwalingania kwa mapenzi ya kidugu wito wa tauhidi wa kumwabudu Mola mmoja wa haki. Kundi moja lilimwamini na kumfuata na kundi jengine lilimkadhibisha na kuikufuru haki. Ni jambo la kawaida kwamba hasama na makabiliano hujitokeza baina ya waumini na makafiri. Uhasama ambao baadhi ya wakati huwa ni wa baina ya mtu na mtu, na wakati mwengine huwa na sura ya kijamii. Nabii Saleh (AS) alikuwa akiwaonya na kuwapa indhari wale makafiri wakaidi kwamba mwisho na hatima yenu itakuwa ni kuishia kwenye adhabu ya moto. Kwa nini hamuachi madhambi na vitendo viovu, na kwa nini mnamwasi Mwenyezi Mungu? Hata hivyo badala ya watu hao kuzinduka na kutubia, walikuwa wakimjibu Mtume wao kwa kumwambia:"kama uyasemayo ni kweli kwa nini Mungu wako hatuteremshii adhabu ili likajulikana moja kati ya sisi na wewe? Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba: Nabii Saleh aliwaambia watu wake: kwa nini nyinyi badala ya kuomba maghufira kwa mliyoyafanya huko nyuma na kumuomba Allah msamaha ili akurehemuni, mnaharakisha kuteremshiwa adhabu? Na badala ya toba mnaomba adhabu? Kwa nini badala ya kujitahidi kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, ambazo ndizo zitakazokupatieni kheri na saada, mnaharakisha kuteremshiwa adhabu ambayo itakuleteeni hilaki na maangamizi? Tajiriba inaonesha kuwa katika zama zote za historia wakanushaji na maadui wa haki, badala ya kuyakubali maonyo na indhari za Mitume waliamua kukabiliana nao kwa kutaka kuwatoa katika miji yao. Katika kisa cha Nabii Saleh (AS) kwa kuwa njaa na ukame vilikuwa vimeukumba mji huo, watu hao walimwambia Mtume huyo wa Allah:"mazonge na masaibu yote haya yanatokana na maneno yako na wafuasi wako, kiasi cha kuyafanya maumbile yatususie na kutugomea; na ndio maana tumefikwa na matatizo haya. Nyinyi ni watu wenye mkosi na kisirani, ambao mumeiletea nuhusi kaumu hii. Lakini Nabii Saleh aliwajibu watu wake kwa kuwaambia: "hatima na majaaliwa yenu kuwa mema au mabaya yako kwenye elimu na mamlaka ya Mwenyezi Mungu. Nyinyi mmefanyiwa majaribu; na huu ukame ni namna moja ya mtihani wa Mwenyezi Mungu, na si kwamba hili ni jambo la nuhusi ambalo limekufikeni kutokana na mtu fulani mkataka kumnasibisha nalo. Bali si hasha maovu yenu na madhambi yenu yakawa ndiyo sababu ya njaa na ukame uliopo." Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kulingania tauhidi na kumwabudu Mola pekee wa haki ndio mhimili mkuu wa wito wa Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika zama zote za historia siku zote kumekuwepo na utesi, hasama na uadui baina ya haki na batili. Hivyo tusitarajie kama watu wote wataikubali mantiki ya haki, na kuwa waumini na watenda mema. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba sambamba na kuwapa wafanya madhambi maonyo na indhari, tuwaonyeshe pia njia ya toba ili kuwaandalia mazingira ya kubadilika na kurejea kwenye njia ya haki. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba baada ya kuemewa na kushindwa kukabiliana na mantiki na hoja za wazi za Mitume, makafiri hukimbilia kwenye mambo ya khurafa yakiwemo ya imani ya uaguzi wa bahati njema au mkosi na nuhusi.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 48 na 49 ambazo zinasema:


وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الأَرْضِ وَلا يُصْلِحُونَ

Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi wala hawafanyi la maslaha.


قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ

Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli.


Aya hizi zinaashiria njama ya kutaka kumuua Nabii Saleh (AS) na wafuasi wake na kueleza kwamba: katika watu wa kaumu ya Thamud yalikuwapo makundi ya watu waliokuwa wamezama kwenye maovu na ufisadi. Watu hao hawakuwa na nia ya kufanya mambo mema, na kujirekebisha kwa kuacha vitendo vyao viovu. Watu hao waliwekeana ahadi wamuue Nabii Saleh, ahli zake pamoja na wafuasi wake, na kisha baada ya kufanya hivyo ikiwa atatokea mtu kuwatuhumu kwamba wameua watasema:"Sisi hatukuwa na habari kabisaa ya jambo hili, labda ni watu wengine ndio waliofanya hayo". Ajabu ni kwamba katika kuwekeana ahadi yao waliapishana kwa jina la Mwenyezi Mungu ili kuonesha kuwa walikuwa wakimjua na kumkubali Yeye kuwa ni Muumba, lakini katika imani yao, wakiitakidi kwamba masanamu ndiyo yanayoathiri majaaliwa yao na ndiyo wanayoyaabudu. Watu hao walikuwa wakisema:" Mwenyezi Mungu ametuumba lakini ametuachia kila kitu wenyewe, kwa hivyo lolote lile tutakalo na tunalohisi lina maslaha na sisi tunafanya na wala hakuna haja ya kutuletea Mitume. Itikadi yao hiyo ni sawa kabisa na waliyonayo watu wanaojifanya wanafikra wataalamika katika zama zetu hizi, ambao hawaukanushi uumbaji wa Mwenyezi Mungu lakini wanaitakidi kuwa mwanadamu ana mamlaka ya kujifanyia mambo yake; na kwa hivyo wanampa haki ya kufanya lolote apendalo kwa sharti tu asiwasababishie madhara watu wengine. Njama ya kutaka kumuua Nabii Saleh inakumbusha pia njama ya washirikina wa Makka dhidi ya Bwana Mtume Muhammad (SAW) walipotaka kumuua mtukufu huyo katika pingapinga la usiku wakati amelala kitandani pake. Washirikina kutoka kila kabila walichagua mtu wao mmoja ili makabila yote yawe yameshiriki katika mauaji ya Bwana Mtume, na wakati watu wake watakapodai kisasi cha damu yake wasiweze kulituhumu na kuliandama kabila maalumu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wapinzani wa Mitume hawakuwa watu wa hoja na mantiki. Walikuwa wakifanya vitimbi mbalimbali ili kuzuia kuenea wito wa Mitume na hata kupanga njama za kutaka kuwaua. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika historia kuna matukio mengi ya ibra na mazingatio. Kuna watu waliofikia hadi ya kula kiapo kwa jina la Mwenyezi Mungu kwa lengo la kuwaua Mitume wake, ambalo ni dhihirisho la upeo wa ujahili na upotovu. Ni kama ilivyokuwa kwa tapo la Khawarij, ambao kwa kudhani wanajikurubisha kwa Allah, walimuua shahidi kwa dharba ya upanga mja mteule wa Allah, Imam Ali (AS) ndani ya nyumba ya Allah na katika mwezi mtukufu wa Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 672 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atuoneshe haki na kutupa taufiki ya kuifuata na atuoneshe batili na kutuwezesha kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)