Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 11:58

Sura ya An-Naml, aya ya 41-44 (Darsa ya 671)

Sura ya An-Naml, aya ya 41-44 (Darsa ya 671)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 671, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 41 hadi 43 ambazo zinasema:


قَالَ نَكِّرُوا لَهَا عَرْشَهَا نَنظُرْ أَتَهْتَدِي أَمْ تَكُونُ مِنَ الَّذِينَ لا يَهْتَدُونَ

Akasema: Kibadilini kiti chake cha enzi hiki, tuone atakitambua, au atakuwa miongoni mwa wasioweza kukitambua.


فَلَمَّا جَاءَتْ قِيلَ أَهَكَذَا عَرْشُكِ قَالَتْ كَأَنَّهُ هُوَ وَأُوتِينَا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهَا وَكُنَّا مُسْلِمِينَ

Basi (Malkia) alipo fika akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hichi. (Malkia na watu wake wakasema): Na sisi tulishapewa ilimu kabla (kuhusu ukweli wa Sulaiman), na tukawa tumeshajisalimisha.


وَصَدَّهَا مَا كَانَت تَّعْبُدُ مِن دُونِ اللَّهِ إِنَّهَا كَانَتْ مِن قَوْمٍ كَافِرِينَ

Na yale aliyo kuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia (kusalimu amri mbele ya haki). Hakika yeye (Malkia) alikuwa katika kaumu ya makafiri.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa malkia wa Saba'a Balqis aliondoka huko Yemen pamoja na watu wa utawala wake na kuanza safari ya kuelekea Sham ili kwenda kutangaza kuwa amesalimu amri mbele ya Nabii Suleiman (AS). Na wakati huohuo tukasema kuwa kutokana na agizo lililotolewa na Mtume huyo wa Allah, kufumba na kufumbua kiti cha enzi cha malkia wa Saba'a kilitolewa kutoka kwenye kasri la ufalme wake hadi kwenye kasri la Nabii Suleiman (AS). Aya tulizosoma zinasema: ili kupima kiwango cha urazini na ufahamu wa malkia wa Saba'a, na vilevile kumuonyesha makarama aliyojaaliwa kuwa nayo, Nabii Suleiman alitoa amri kiti hicho cha enzi kitiwe mapambo yatakayokifanya kiwe tofauti kabisa na hali yake ya awali. Wakati malkia wa Saba'a alipoingia kwenye kasri la Nabii Suleiman alionyeshwa kiti chake cha enzi na kuulizwa: "kiti chako cha enzi kinafanana na hiki?" Alipokiangalia, Balqis alikitambua kiti chake cha enzi licha ya mapambo na mabadiliko yote kiliyofanyiwa; na akasema: "ni kama chenyewe hasa." Baada ya kukitambua kiti chake cha enzi, malkia wa Saba'a alimuelekea Nabii Suleiman (AS) pamoja na watu wa utawala wake na kuwaambia:" kama lengo lenu la kufanya hivi ni kutaka tuelewe nguvu na uwezo wenu na kusalimu amri kwenu, sisi kabla ya kuja hapa tulishaelewa nguvu na uwezo wenu, na tumekuja hapa tukiwa tumesalimu amri. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: kwa vile malkia wa Saba'a alikuwa mmoja wa makafiri wakubwa, imani ya kuabudu jua na masanamu ilikuwa imekithiri na kuenea ndani ya jamii ya watu wake kiasi kwamba hakuruhusu mtu yeyote afikirie imani ya tauhidi au kutaka kumjua Mola Muumba wa haki. Lakini pamoja na hayo wakati alipofikishiwa wito wa haki na akaitambua, aliikubali na kujisalimisha mbele yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kusilimu na kuiamini haki huwa na thamani pale kunapofanyika kutokana na elimu na utambuzi, na si kuiga na kufuata kibubusa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa fikra za khurafa na itikadi potofu zitapenya ndani ya jamii, huwa kizuizi na kikwazo kwa watu kuitambua na kuiamini haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kwa kuwa binadamu ni kiumbe chenye sifa ya kuweza kubadilika, kuwa na rekodi mbaya tu huko nyuma si hoja na sababu ya kumfanya mtu awe na mustakabali mbaya. Bali si hasha watu ambao walikuwa wabaya hapo kabla, baadaye wakaamua kufuata njia sahihi na kujirekebisha nafsi zao.
Darsa ya 671 ya Qur'ani inahitimishwa na aya ya 44 ambayo inasema:


قِيلَ لَهَا ادْخُلِي الصَّرْحَ فَلَمَّا رَأَتْهُ حَسِبَتْهُ لُجَّةً وَكَشَفَتْ عَن سَاقَيْهَا قَالَ إِنَّهُ صَرْحٌ مُّمَرَّدٌ مِّن قَوَارِيرَ قَالَتْ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي وَأَسْلَمْتُ مَعَ سُلَيْمَانَ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

Akaambiwa: Ingia kwenye kasri. Alipoliona alidhani ni lindi la maji, na akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. (Sulaiman) akasema: Hakika hilo ni kasri lilio sakafiwa kwa vioo ving'aravyo! Akasema (Malkia): Mola wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu, na sasa najisalimisha pamoja na Sulaiman kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.


Kama inavyoonekana, kwa mujibu wa aya tuliyosoma, Nabii Suleiman (AS) alikuwa ametoa amri ya kujengwa katika ua mmoja wa makasri yake sakafu ya vigae vilivyong'arishwa na kumeremeta ambayo maji yatakuwa yakipita chini yake. Wakati malkia wa Saba'a alipotaka kupita juu ya sakafu hiyo, alipandisha juu nguu yake ili isiroe kwa kudhani kwamba ulikuwa ni mto. Kwa kuishuhudia mandhari hiyo, Nabii Suleiman (AS) alimwambia Balqis: sakafu hii ya ua imetengenezwa kwa vigae na vioo vinavyong'ara, kwa namna inayowafanya watu wasiione na kuamua kupita juu yake bila ya viatu kwa kudhani kuwa ni mto. Ni wazi kwamba kushuhudia mandhari hiyo, kulimstaajabisha na kumfadhaisha malkia wa Saba'a ambaye alikuwa mtu mwenye kiti cha enzi na kasri la fahari la ufalme wake, na kumfanya ahisi utawala wake na kila ulichonacho ni kitu kidogo na duni kabisa mbele ya kasri lenye adhama la ufalme wa Nabii Suleiman. Na kwa hivyo hakubakiwa na kitu kingine chochote kile cha kutambia na kujigamba kwa nguvu na suhula mbele ya Mtume huyo wa Allah. Kwa maneno mengine, kwa kuonesha nguvu za utawala wake na suhula za kimaada na zisizo za kimaada ulizonazo, Nabii Suleiman alimtanabahisha malkia wa Saba'a kwamba isije ikampitikia akilini mwake kutaka kukabiliana naye na kupigana naye vita, na kufanya jambo litakalosababisha pande hizo mbili kupata hasara kubwa zinazotokana na vita. Baada ya kuvunjwa nguvu na adhama yake ya kimaada, malkia wa Saba'a alinyenyekea na kusalimu amri pia kimaanawi mbele ya dini ya haki ya Nabii Suleiman (AS). Kwa sababu alitambua kwamba nguvu na adhama zote hizo havikumhadaa Suleman (AS) na kumfanya atekwe na kupaparikia mapambo ya kidunia; bali pamoja na kuwa na ufalme anatekeleza kwa uzito kamili kazi yake ya Utume na kuwalingania watu njia ya Mwenyezi Mungu; na wala hakuna mgongano wala mkinzano baina ya mawili hayo. Kwa hivyo Balqis akaomba maghufira kwa Allah na kutangaza kuwa anajisalimisha mbele ya Yeye Mola Muumba kwa kuacha kuabudu jua na kufuata dini ya haki ya tauhidi. Ni jambo la kuvutia kwamba katika kubainisha hayo malkia wa Saba'a hakutamka kuwa: Mimi nimejisalimisha kwa Suleiman, bali alisema: mimi nimejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Suleiman pia amejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu; na sisi sote wawili ni waja wa Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka kusilimu kwa malkia Balqis kuliwezesha watu wake wa ardhi ya Saba'a nao pia waachane na dhalala na imani potofu ya kuabudu jua na badala yake kumwabudu Mola mmoja pekee wa haki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba suhula za kimaada zinapasa zitumike katika tablighi na uenezaji dini, kama ambavyo Nabii Suleiman (AS) aliutumia ufundi na suhula za kimaada kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwaonesha watu njia ya uongofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa ni jambo zuri kabisa kutumia vitu kama sanaa, mapambo, ufundi na teknolojia za kisasa zinazoweza kuwapigisha magoti, kuwafumba midomo na kuwafanya makafiri wauheshimu Uislamu. Kadhalika aya hii inatuelimisha kwamba toba ya kweli ni ile ya mtu kuungama kwa makosa na madhambi aliyofanya huko nyuma, akaomba maghufira na msamaha kwa Allah na akaamua kwa dhati kufuata nuru ya uongofu katika mustakabali wake. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba kiini halisi cha imani ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu Muumba wa ulimwengu, kama ambavyo malkia Balqis wa Saba'a alitamka mwishowe kwamba amejisalimisha kwa Allah, Mola wa ulimwengu wote. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 671 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola ajizaje subira nyoyo zetu, azifanye thabiti imani zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)