Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 11:55

Sura ya An-Naml, aya ya 36-40 (Darsa ya 670)

Sura ya An-Naml, aya ya 36-40 (Darsa ya 670)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 670, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 36 na 37 ambazo zinasema:


فَلَمَّا جَاءَ سُلَيْمَانَ قَالَ أَتُمِدُّونَنِ بِمَالٍ فَمَا آتَانِيَ اللَّهُ خَيْرٌ مِّمَّا آتَاكُم بَلْ أَنتُم بِهَدِيَّتِكُمْ تَفْرَحُونَ

Basi alipo fika (mjumbe) kwa Sulaiman, alisema (Sulaiman): Hivyo ndio nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Lakini nyinyi mnafurahia hii zawadi yenu.


ارْجِعْ إِلَيْهِمْ فَلَنَأْتِيَنَّهُمْ بِجُنُودٍ لّا قِبَلَ لَهُم بِهَا وَلَنُخْرِجَنَّهُم مِّنْهَا أَذِلَّةً وَهُمْ صَاغِرُونَ

Rejea kwao! Kwa yakini sisi tutawajia na majeshi wasiyo weza kuyakabili. Na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa katika kujibu wito uliokuwemo kwenye barua aliyopelekewa na Nabii Suleiman (AS), Malkia wa Saba'a Balqis aliamua kutuma wajumbe kwa Mtume huyo wa Allah wakiwa na zawadi na hidaya mbalimbali za kumjaribu na kumpima ili kuelewa kama lengo lake la kumpelekea barua ni kutaka mali, utajiri na mambo ya kidunia au ana lengo jengine ghairi ya hilo. Malkia wa Saba'a aliwataka wajumbe wake wamtizame Nabii Suleiman atafanya nini na ataonyesha hisia gani wakati atakapoziona zawadi alizopelekewa na kisha wakampe habari. Aya tulizosoma zinaeleza kuwa sio tu Nabii Suleiman hakufurahika kwa kuziona zawadi na hidaya hizo, bali alikichukulia kitendo hicho kuwa ni aina fulani ya rushwa ya kutaka kumlaghai; hivyo akasema: Nyinyi mumedhani kwamba ninachokitaka mimi ni mali na utajiri, ndo mkaniletea hidaya na zawadi hizi? Hivi mlivyovileta nyinyi si lolote si chochote kulinganisha na yale niliyopewa na kutunukiwa na Mola wangu. Kusudio langu mimi ni kukutakeni mujisalimishe mbele ya haki. Kama hamtojisalimisha mbele ya haki nitakujieni na jeshi kubwa na kuyatwaa madaraka na utawala wenu kiasi cha kukufanyeni mlazimike kuhama na kuondoka huko katika hali ya unyonge na udhalili. Mimi nilitarajia kwamba kwa kupata barua yangu mtachukua hatua ya kufanya uhakiki na kunitaka nikupeni hoja na burhani za kuthibitisha Utume wangu na si kuniletea zawadi za kutaka kunilaghai na kunihadaa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mawalii wa Allah hawafanyi mambo kwa nia ya kutafuta maslahi ya kimaada na wala hawayafanyii muamala malengo na majukumu waliyopewa na Mola kwa pesa na vitu vya kidunia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa inapasa kutumia mantiki katika kuamiliana na watu, lakini kwa wale ambao hawako tayari kusalimu amri mbele ya haki, baadhi ya wakati hulazimu kuwatunishia misuli pia. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba Jihadi ilikuwepo pia katika zama za Mitume waliotangulia.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 38 ambayo inasema:


قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَن يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ

Akasema: Enyi wahishimiwa! Ni nani kati yenu atakaye niletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.


Kama ilivyoelezwa katika tafsiri za Qur'ani, baada ya wajumbe wa Balqis kukutana na Nabii Suleiman (AS) walirudi kwa malkia huyo wa Saba'a na kumsimulia aliyoyasema Mtume huyo wa Allah wakati walipompelekea zawadi alizowapa pamoja na adhama na mamlaka ya utawala wake. Baada ya kuelezwa hayo malkia wa Saba'a aliamua yeye mwenyewe pamoja na maashrafu na waheshimiwa wa utawala wake kwenda kwa Nabii Suleiman na kumfahamisha kwamba hana dhamira wala nia ya kutaka kukabiliana naye. Kwa elimu aliyojaaliwa na Mola, Nabii Suleiman (AS) aliweza kutambua kuhusu safari hiyo ya malkia wa Saba'a; hivyo ili kumfanya aelewe nguvu za mamlaka aliyojaaliwa na Allah aliwataka watu wa utawala wake wakamletee hapo Sham alipo kiti cha enzi cha malkia Balqis kilichokuwako huko Yemen kabla ya malkia mwenyewe na msafara wake hawajawasili huko. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mitume wa Mwenyezi Mungu wamejaaliwa kuwa na elimu ya ghaibu ambayo huitumia kwa namna inayostahiki kila pale inapolazimu kufanya hivyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa suala la ukataji masafa ya ardhi kwa kuweza kufika mahala pa masafa marefu kwa muda mfupi kabisa linawezekana kufanywa na watu hata wasiokuwa Mitume. Ni kwa sababu hiyo Nabii Suleiman (AS) alimtaka yeyote miongoni mwa watu wa utawala wake aliye na uwezo wa kuifanya kazi hiyo aifanye.
Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya 39 na 40 ambazo zinasema:


قَالَ عِفْريتٌ مِّنَ الْجِنِّ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن تَقُومَ مِن مَّقَامِكَ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ

Akasema: Afriti, katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka pahala pako hapo. Na mimi kwa hakika nina nguvu na muaminifu.


قَالَ الَّذِي عِندَهُ عِلْمٌ مِّنَ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِندَهُ قَالَ هَذَا مِن فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ

Akasema mwenye ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipo kiona kimewekwa mbele yake, akasema (Sulaiman): Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Mkarimu.


Baada ya Nabii Suleiman (AS) kutoa wito wa kutaka kiti cha enzi cha Malkia wa Saba'a kiletwe kutoka Yemen hadi Sham kwa kutumia muda mfupi kabisa, watu wawili walijitokeza na kutangaza kwamba wako tayari kuifanya kazi hiyo; mmoja wao alikuwa ni jini aliyekuwa ndani ya kasri la utawala wa Nabii Suleiman akitekeleza amri zake. Jini huyo alisema anao uwezo wa kukileta kiti hicho cha enzi kabla ya kikao hicho kumalizika na Nabii Suleiman kuinuka kwenye kiti chake cha ufalme. Lakini kinyume na ahadi iliyotolewea jini huyo, mtu mwengine aliyekuwa akiitwa Aasif Ibn Barkhiya, ambaye alikuwa mmoja wa mawaziri wa Nabii Suleiman, na ambaye ndiye aliyeshika nafasi yake baada ya yeye kuaga dunia, yeye alitamka kwamba, anao uwezo wa kukileta kiti cha enzi cha Balqis kutoka Saba'a kwa muda wa kiasi cha kupepesa macho tu. Kwa kuwa muda aliopendekeza yeye ulikuwa mfupi zaidi, Nabii Suleiman alikubali, na akampa Aasif Ibn Barkhiya kazi hiyo ya kukileta kiti cha enzi cha Malkia wa Saba'a. Na yeye akakileta kiti hicho mbele ya Nabii Suleiman na hadhara iliyokuwepo baada ya lahadha ndogo kabisa. Jambo hilo lililofanywa na mmoja wa wanafunzi na watu waliochini ya Nabii Suleiman (AS) lingeweza kumtia ghururi yeye mfanyaji mwenyewe pamoja na watu wengine wa karibu wa ufalme wa Mtume huyo. Kwa hivyo ili kuzuia kutokea jambo hilo, Nabii Suleiman alilitaja jina la Mwenyezi Mungu ili kuwakumbusha watu wake kwamba kuweza kufanya jambo kama hili hakutokani na nguvu na uhodari wetu, bali ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu; hivyo tunapaswa kuwa washukurivu kwake; japokuwa Yeye Mola si mhitaji wa hilo, kwa sababu adhama na utukufu wake ni mkubwa zaidi ya kuhitaji kuhimidiwa na kushukuriwa na waja wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kwa kutumia elimu ya Mwenyezi Mungu, mwanadamu huweza kuutawala ulimwengu wa maumbile na kanuni zinazotawala ndani yake na kuvitumia vitu vya maumbile kwa namna aitakayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kwa kupitia teknolojia inayotumika katika vyombo vya habari na mawasiliano, mwanadamu wa leo anaweza kuonesha ulimwengu mzima na kwa wakati mmoja sauti na picha za vitu na watu. Si jambo lililo muhali kuvikutanisha vitu vyenyewe, bila kujali mahala na wakati, japokuwa elimu ya mwanadamu haijaweza kufikia uwezo huo kwa sasa. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa tusiingiwe na ghururi kwa sababu ya elimu na madaraka tuliyonayo. Neema yoyote tuliyonayo haitokani na sisi wenyewe bali inatokana na fadhila, ukarimu na rehma zisizo na kikomo za Allah SW. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 670 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washurukivu wa neema zake zote, kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)