Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 11:52

Sura ya An-Naml, aya ya 29-35 (Darsa ya 669)

Sura ya An-Naml, aya ya 29-35 (Darsa ya 669)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 669, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 29 hadi 31 ambazo zinasema:


قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ إِنِّي أُلْقِيَ إِلَيَّ كِتَابٌ كَرِيمٌ

(Malkia) akasema: Enyi wahishimiwa! Hakika nimeletewa barua tukufu.


إِنَّهُ مِن سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Imetoka kwa Sulaiman nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.


أَلاَّ تَعْلُوا عَلَيَّ وَأْتُونِي مُسْلِمِينَ

(Kwamba) msinifanyie jeuri, na fikeni kwangu nanyi mmekwisha kuwa wenye kusalimu amri.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa baada ya Nabii Suleiman (AS) kupata habari kuhusu yale yaliyokuwa yakijiri katika ardhi ya Saba'a ya watu wa ardhi hiyo kuabudu jua aliamua kuandika barua na kumpa ndege Hud hud kazi ya kuipeleka barua hiyo kwa watu hao. Hud hud alielekea hadi kwenye kasri la malkia wa Sheba na kuidondosha barua aliyopewa na Nabii Suleiman kwa malkia huyo. Aya tulizosoma zinasimulia yaliyojiri baada ya hapo kwa kueleza kwamba wakati malkia wa Saba'a alipoiona barua hiyo alibaini kwamba ndege huyo mzuri na wa kupendeza ni mfikishaji barua; na barua aliyomletea inatoka kwa shakhsia mkubwa. Malkia huyo alikuwa na washauri na watu wake wa karibu ambao alikuwa akiwapa taarifa na habari za matukio yaliyokuwa yakijiri. Aliwaita watu hao na kuwasomea yeye mwenyewe barua aliyoletewa. Barua hiyo ilikuwa imeanza kwa jina la Allah, na muhtawa na yaliyokuwemo ndani yake ni vitu viwili. Kimoja ni kusalimu amri mbele ya haki, na kingine ni kutofanya uasi na ukaidi wowote mbele ya utawala wa Nabii Suleiman (AS). Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mambo yetu yote tuyafanyayo, tuyaanze kwa jina la Allah, mwingi wa rehma, mwenye kurehemu. Hata tunapowaandikia barua watu ambao ni makafiri tusilisahau tamko la Bismillahir Rahmanir Rahiim. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kujikweza na kujifanya bora kunamkosesha mtu fursa ya kuisalimisha nafsi yake mbele ya haki.
Zifuatazo sasa ni aya za 32 na 33 ambazo zinasema:


قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَفْتُونِي فِي أَمْرِي مَا كُنتُ قَاطِعَةً أَمْرًا حَتَّى تَشْهَدُونِ

Akasema: Enyi wahishimiwa! Nipeni ushauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri yoyote mpaka mhudhurie.


قَالُوا نَحْنُ أُوْلُوا قُوَّةٍ وَأُوْلُوا بَأْسٍ شَدِيدٍ وَالأَمْرُ إِلَيْكِ فَانظُرِي مَاذَا تَأْمُرِينَ

Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali kwa vita; na amri iko kwako, basi tazama ni nini unaamrisha.


Baada ya kuisoma barua ya Nabii Suleiman, malkia wa Saba'a, ambaye alikuwa mwanasiasa mjuzi na mwenye uono wa mbali aliwaita maafisa wake wa mamlaka ya ufalme na wa jeshi lake na kuwataka wamshauri ni jawabu gani atoe kwa barua aliyoletewa. Ni wazi kuwa ushauri huo ungemsaidia kuelewa, watu wake wana utayarifu wa kiwango gani wa kukabiliana na Suleiman na hivyo kutumia njia na mbinu bora na mwafaka. Washauri wa malkia Balqis pamoja na majemedari wa jeshi lake walijigamba mbele yake kwa wapiganaji shupavu na wenye nguvu walionao na zana nyingi na imara za vita walizonazo; na wakatangaza kuwa wako tayari wakati wowote kukabiliana na shambulio lolote litakalofanywa na Suleiman. Ukweli ni kwamba wao waliyafasiri madhumuni ya barua hiyo kuwa Nabii Suleiman (AS) alikuwa ametangaza vita, na kwa hivyo kama walivyo makamanda wa jeshi wa aghalabu ya nchi, badala ya kukubali kusalimu amri wakapendekeza waingie vitani kupambana naye. Lakini baada ya kutangaza kuwa tayari kwao kwa vita wakamwachia malkia mwenyewe atoe uamuzi wa mwisho; kwamba lolote atakaloamuru yeye ndilo watakalolifanya na wala hawatokwenda kinyume na amri yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuna ulazima wa kuwa na vikosi vya askari, nguvu za kijeshi, zana na suhula mbalimbali kwa ajili ya uendeshaji nchi, lakini kwa sharti kwamba vitu hivyo visiwe sababu ya kuwatia watu ghururi, wakataka kuanzisha ubeberu dhidi ya wenzao na kuwafanya wasiwe tayari kuikubali haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ni jambo muhimu sana kutaka ushauri katika mambo hasa ya kufanya tadbiri kuhusiana na utawala, lakini uamuzi wa mwisho unapasa uchukuliwe na mtu mmoja ili usitokee mparaganyiko na mvurugiko katika uendeshaji mambo.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 34 na 35 ambazo zinasema:


قَالَتْ إِنَّ الْمُلُوكَ إِذَا دَخَلُوا قَرْيَةً أَفْسَدُوهَا وَجَعَلُوا أَعِزَّةَ أَهْلِهَا أَذِلَّةً وَكَذَلِكَ يَفْعَلُونَ

Akasema: Hakika wafalme wanapo uingia mji wanauharibu, na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge. Na hivyo ndivyo watendavyo.


وَإِنِّي مُرْسِلَةٌ إِلَيْهِم بِهَدِيَّةٍ فَنَاظِرَةٌ بِمَ يَرْجِعُ الْمُرْسَلُونَ

Lakini mimi nitawapelekea zawadi, nami nitangoja watakayo rudi nayo wajumbe.


Baada ya malkia Balqis wa Saba'a kusikiliza maoni ya maashrafu, washauri na majemedari wa jeshi la utawala wake na kuelewa utayarifu wao kwa vita na mapambano alitangaza uamuzi wake kwa kusema: ikiwa tutaamua kuingia vitani hakuna kitakachopatikana zaidi ya uharibifu na ufisadi. Kwa sababu watawala wapenda ulua wanapoingia katika mji wowote ule hufanya uharibifu wa kubomoa nyumba na kuwaua au kuwafanya mateka watu wenye izza katika mji huo na kuwaweka watu katika hali ya udunifu na udhalilifu. Kwa hivyo badala ya kutangaza vita ni bora kwanza tutafute taarifa na habari zaidi kuhusu upande wa pili ili tujue ni nini lengo la kutuma barua hii? Hivyo Malkia wa Saba'a akaamua kumpelekea Nabii Suleiman zawadi na hidaya za tunu na zenye thamani kubwa ili kuona atafanya nini. Yaani kwa kupelekewa zawadi hizo ambazo ni alama ya kutokuwa na azma ya kupigana vita, je suala hilo litamalizika, au lengo hasa la Suleiman ni kuivamia na kuiteka ardhi hiyo. Hivyo akawaambia watu wake: baada ya kuona hatua atakayoonyesha Suleiman ndipo tutakapoweza kuchukua uamuzi unaofaa, kama tuingie vitani au tufikirie uamuzi mwengine wa kuchukua. Yamkini kwa hatua yake ya kutuma zawadi, malkia Balqis wa Saba'a alitaka kumjaribu Nabii Suleiman (AS) ili kujua kama ni kweli Mtume wa Mwenyezi Mungu au ni mfalme tu aliyelewa madaraka ambaye anataka kuzihodhi na kuzitawala nchi nyengine. Kwa sababu alikuwa akijua kwamba Mitume huwa hawaghilibiki kwa mali za dunia na wala hawaachi kufanya kazi yao ya tablighi na kuwapa watu miongozo ya uongofu. Ni wafalme wanaopenda dunia ndio huwa tayari kufanya lolote lile alimuradi wafanikishe malengo yao binafsi na kuweza kujipatia mali na madaraka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kueneza ufisadi na uharibifu, na kuchochea vita na umwagaji damu kwa ajili ya kuwatawala watu ndio mbinu ya tawala ovu zisizofuata muongozo wa Allah. Aidha aya hizi zinatutaka tuwe na hadhari na zawadi na hidaya tunazopewa na watu; kwani baadhi ya wakati huwa ni aina ya hongo ya kutughilibu au kutaka kuififilisha haki. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 669 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aupe nguvu na izza Uislamu na Waislamu, na awafanye madhalili wale wote wenye uadui na dini hiyo ya haki. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)