Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 11:48

Sura ya An-Naml, aya ya 23-28 (Darsa ya 668)

Sura ya An-Naml, aya ya 23-28 (Darsa ya 668)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 668, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 23 na 24 ambazo zinasema:


إِنِّي وَجَدتُّ امْرَأَةً تَمْلِكُهُمْ وَأُوتِيَتْ مِن كُلِّ شَيْءٍ وَلَهَا عَرْشٌ عَظِيمٌ

Hakika mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho kiti cha enzi kikubwa.


وَجَدتُّهَا وَقَوْمَهَا يَسْجُدُونَ لِلشَّمْسِ مِن دُونِ اللَّهِ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ فَهُمْ لا يَهْتَدُونَ

Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na Shet'ani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia. Kwa hivyo hawakuongoka,


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa wakati ndege Hud Hud alipotakiwa na Nabii Suleiman (AS) aeleze sababu ya kughibu na kutokuwepo katika hadhara ya jeshi lake alimwambia mtukufu huyo kwamba mimi nilikuwa nimekwenda ardhi ya Saba'a na nimekuja na ripoti muhimu kutoka huko. Hivyo aya tulizosoma zinabainisha yale yaliyokuwemo kwenye ripoti hiyo ya ndege Hud Hud kwa kueleza kwamba katika ardhi hiyo ya Saba'a, kinyume na ilivyo katika maeneo mengine, mwanamke ndiye mtawala, tena mwenye suhula nyingi mno pamoja na kasri lenye adhama na la kifahari. Nabii Suleiman alistaajabishwa na habari hiyo ya kuelewa kuwepo kwa utawala na mtawala wa aina hiyo; lakini baada ya maelezo hayo ya utangulizi, Hud Hud alibainisha kiini hasa cha ripoti yake kwa kusema: la muhimu, si taji na kiti cha enzi cha ufalme wa mwanamke huyo, bali kile ambacho wewe ukiwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu unapaswa kukijua ni kwamba watu wote wa ardhi ya Saba'a wanaabudu jua na wameghariki kwenye lindi la anuai za maasi na madhambi. Na sababu ni kwamba shetani amewazaini kwa kuwafanya wayaone maovu wayatendayo ni mema na mazuri. Kwa hivyo ni jambo gumu na lililo mbali kwa watu hao kuufikia uongofu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kujaaliwa kuwa na neema na Allah, sio kigezo na kipimo pekee cha kuonyesha uzuri na ubaya wa watu. Nabii Suleiman na Balqis, wote wawili walijaaliwa kuwa na neema nyingi mno, lakini mmoja alikuwa Mtume wa Allah na mwengine alikuwa mtawala kafiri. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa aghalabu ya watu hufuata na kuamini itikadi na dini inayokubaliwa na kufuatwa na viongozi wao. Na ni kwa sababu hiyo tawala huwa na nafasi na mchango wenye taathira katika muelekeo wa dini na itikadi wanazofuata watu wao.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 25 na 26 ambazo zinasema:


أَلاَّ يَسْجُدُوا لِلَّهِ الَّذِي يُخْرِجُ الْخَبْءَ فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُخْفُونَ وَمَا تُعْلِنُونَ

(Shetani amewaghilibu) kwamba wasimsujudie Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyo fichikana katika mbingu na ardhi, na anayajua mnayo yaficha na mnayo yadhihirisha.


اللَّهُ لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ

Mwenyezi Mungu - hapana Mola ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi tukufu.


Baada ya Hud Hud kutoa ripoti yake kuhusu upotofu wa kuabudu jua wa watu wa Saba'a, kwa maastajabu na mshangao alisema: mimi nashindwa kuelewa ni kwa nini wao wameamua kuliabudu jua badala ya kumwabudu Mwenyezi Mungu avitoaye vilivyofichika vya mbinguni na ardhini na Mjuzi wa yafanywayo na wanadamu kwa siri na kwa dhahiri! Inafaa kuashiria kuwa moja ya misdaqi na mifano hai ya utoaji vilivyofichika mbinguni na ardhini, ni mvua zinyeshazo na mimea iotayo kutokana na maji ya mvua hiyo. Sisi sote tunajua kwamba awali kicha cha mmea huwa kimefichika ndani ya mbegu, lakini kwa nguvu na tadbiri yake Mola, huchomoza kicha hicho ndani ya mbegu hiyo katika sura ya mche mzuri wenye kuvutia. Kwa mtazamo wa Hud Hud, hata Nabii Suleiman (AS) ambaye ni Mtume wa Allah na mfalme mkubwa pia, hawezi kuwa na hadhi ya kuabudiwa. Kwa sababu elimu yake ina mpaka maalumu na wala hana habari ni nini kinachotokea katika ardhi ya Saba'a. Mungu pekee anayestahiki kuabudiwa ni yule mwenye elimu na ujuzi wa mambo yote, hata yaliyofichika katika ulimwengu wa maumbile na ya siri yafanywayo na wanadamu, na ambaye wakati wowote ule atakapo ni mweza wa kuyadhihirisha yote ya siri na yaliyofichika. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuabudu ni jambo la kimaumbile; na katika kila zama za historia yao, wanadamu wamekuwa wakivitukuza, kuvichukulia kuwa na taathira na kuviabudu viumbe wenzao mbalimbali vikiwemo vitu visivyo na uhai, wanyama na hata wanadamu wenzao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa vitu vya kimaumbile kama jua vina taathira kubwa katika uotaji wa mimea na kwa maisha ya viumbe hai; lakini vitu hivyo si waumbaji wa nafsi zao wenyewe na wala sifa maalumu vilizonazo hazitokani na wao wenyewe. Anayepasa kuabudiwa na kusujudiwa ni Muumba wa jua, na si jua lenyewe ambalo ni mojawapo ya viumbe wa Allah. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba lengo la shetani la kuvifanya vibaya vionekane vizuri na vya kuvutia mbele ya watu ni kuwafanya wasimsujudie Muumba wa ulimwengu; ilhali kumsujudia Allah SW, Mola pekee wa ulimwengu ni dhihirisho la kumwabudu Mungu wa haki. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba ulimwengu ni hadhara ya Mwenyezi Mungu Jalla jalaaluh, na hakuna chochote, kifanywacho na yeyote kinachoweza kufichika mbele yake.
Aya za 27 na 28 ndizo zinazotuhatimisha darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:


قَالَ سَنَنظُرُ أَصَدَقْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْكَاذِبِينَ

Akasema (Sulaiman): Karibuni tutaona (kama) umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.

اذْهَب بِّكِتَابِي هَذَا فَأَلْقِهْ إِلَيْهِمْ ثُمَّ تَوَلَّ عَنْهُمْ فَانظُرْ مَاذَا يَرْجِعُونَ

Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.


Baada ya Nabii Suleiman kusikiliza ripoti ya Hud Hud, alikubali kwamba udhuru wake ulikuwa unakubalika na kwa hivyo hakumchukulia hatua yoyote. Lakini kwa kuwa ripoti hiyo ilikuwa muhimu na ya kuzingatiwa, bila ya kutaka kuitolea maoni yoyote, alihisi kuna ulazima wa kuifanyia uchunguzi kwanza. Kwa hivyo akaamua yeye mwenyewe kuandika barua na kumtaka Hud Hud aipeleke kwa malkia wa Saba'a na kungojea huko huko ili kuona ni jawabu gani atakalotoa. Tab'an kuandika barua kwa lengo la kuwalingania watu uongofu na tauhidi, yaani kumwabudu Mola mmoja tu wa haki ni mojawapo ya sira na mwenendo wa Mitume. Historia inaeleza kuwa Bwana Mtume Muhammad SAW aliwaandikia barua wafalme wa Rumi na Iran za kuwalingania wito wa kuifuata dini ya haki ya Uislamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kuwalingania na kuwaita watu kwenye dini ya haki inapasa kutumia nyenzo tofauti kwa kuzingatia mazingira na mahitaji. Kuna wakati huhitajika hotuba, wakati mwengine huwa ni aula kuandika barua na kuna wakati huhitaji kutuma mjumbe pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa madai na propaganda zinazotolewa na watu juu ya jambo zisituzuie sisi kulifanyia uchunguzi na uhakiki jambo hilo. Japokuwa Hud Hud alidai kwamba habari aliyokuja nayo ni ya uhakika lakini Nabii Suleiman alimwambia: itabidi tuchunguze usahihi na ukweli wake. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kabla ya kuchukua uamuzi wowote kuhusu wapinzani, inapasa kwanza kuwaelewesha na kuwaelimisha, kisha baada ya jibu lao ndipo kuchukua hatua zinazofaa. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 668 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waumini wa kweli, wanaothibitisha imani zako kwa maneno na vitendo vyao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)