Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 11:42

Sura ya An-Naml, aya ya 17-22 (Darsa ya 667)

Sura ya An-Naml, aya ya 17-22 (Darsa ya 667)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 667, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:


وَحُشِرَ لِسُلَيْمَانَ جُنُودُهُ مِنَ الْجِنِّ وَالإِنسِ وَالطَّيْرِ فَهُمْ يُوزَعُونَ

Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na watu, na ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu.


حَتَّى إِذَا أَتَوْا عَلَى وَادِي النَّمْلِ قَالَتْ نَمْلَةٌ يَا أَيُّهَا النَّمْلُ ادْخُلُوا مَسَاكِنَكُمْ لا يَحْطِمَنَّكُمْ سُلَيْمَانُ وَجُنُودُهُ وَهُمْ لا يَشْعُرُونَ

Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake na hali wao hawatambui.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwapa Manabii Daud na Suleiman (AS) elimu na nguvu za mamlaka ambavyo viliwawezesha kuunda utawala katika zama zao. Tawala hizo zilikuwa katika ardhi ya Sham ya wakati na maeneo mengine yaliyoizunguka. Aya hizi tulizosoma zinaashiria moja ya vitu muhimu kwa utawala, yaani kuwa na vikosi vya wanajeshi na kueleza kuwa kundi moja la watu, kundi moja la majini na kundi moja la ndege yalikuwa sehemu ya jeshi lililokuwa chini ya mamlaka ya Nabii Suleiman bin Daud (AS). Jeshi hilo lilikuwa limejiweka tayari kukabiliana na maadui kila pale Mtume huyo wa Allah alipolitaka kufanya hivyo. Siku moja Nabii Suleiman aliliita jeshi lake hilo, na askari wake wote walifika mbele yake wakajipanga kwa nidhamu maalumu na kuanza safari. Wakati walipokuwa njiani walifika kwenye jangwa moja ambalo lilikuwa na wadudu chungu wengi. Kwa irada ya Allah SW, Nabii Suleiman aliyasikia maneno ya wadudu chungu waliokuwa wakiambiana: 'jihadharini msije mkakanyagwa na askari na farasi wa jeshi la Suleiman. Kwa sababu wao hawana habari ya kuwepo kwenu na hivyo watakuangamizeni bila ya kukusudia.' Ilikuwa ni kama kwamba wadudu chungu wa jangwani, nao pia walikuwa wakijua kuwa haifai kwa Nabii Suleiman aliye mtawala kumdhuru mdudu chungu yeyote na vilevile askari wake hawapaswi kumtendea dhulma mdudu huyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mwanadamu anao uwezo wa kumtiisha jini na kumtumia amsaidie katika kazi na mambo tofauti. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa nidhamu, uwezo wa kijeshi na kutumia vikosi imara kwa ajili ya kukabiliana na maadui ni miongoni mwa sifa za utawala wa Mitume. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wanyama, ndege na wadudu wana uwezo wa kuitambua hatari na kutahadharishana nayo. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa waja wateule wa Allah huwa hawamdhuru kwa makusudi na kwa kujua hata kiumbe mdogo kama mdudu chungu.
Ifuatayo sasa ni aya ya 19 ambayo inasema:


فَتَبَسَّمَ ضَاحِكًا مِّن قَوْلِهَا وَقَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَى وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَدْخِلْنِي بِرَحْمَتِكَ فِي عِبَادِكَ الصَّالِحِينَ

Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa kauli yake (mdudu chungu), na akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema unayoyaridhia, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema.


Maneno aliyoyasema mduduchungu kuwaambia wenzake kwamba jihadharani msije mkakanyagwa na kupondwa na askari wa Suleiman, kwa upande mmoja yalimfanya Nabii huyo wa Allah atabasamu huku akistaajabu ni vipi mdudu chungu anafikiria hali za waduduchungu wenzake?! Lakini kwa upande mwengine yalimfanya awaze na kutafakari kwamba isije ikawa katika zama za utawala na ufalme wake kuna watu wa chini na wanyonge wanaoonewa na kutendewa dhulma hata kama ni bila ya kujua wala kukusudia. Kwa sababu hiyo akainua mikono yake juu kuomba dua kwa Mwenyezi Mungu amsaidie na kumwezesha kutekeleza majukumu yake. Yawe ni majukumu yake ya binafsi na ya kifamilia kwa kufikiria na kuzingatia neema mbalimbali ambazo Allah amempa yeye, pamoja na baba na mama yake; au yawe ni majukumu ya kijamii na kiutawala, kwamba asifanye jambo ila lililo la sawa, na tena ni kwa ajili ya kupata radhi zake Mola; na hatima yake iwe ya mwisho mwema na wa kheri na kufufuliwa na waja wema wa Allah. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba moja ya sifa za uongozi na uendeshaji wa jamii ni kuwa na kifua kipana cha subira cha kuweza kusikiliza maneno ya ukosoaji; na badala ya kuwa mkali na kugombana, kuupokea ukosoaji huo kwa tabasamu na bashasha. Kama ambavyo Nabii Suleiman AS pia alitabasamu na kuyakubali maneno yaliyosemwa na mduduchungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, ushukurivu wa neema za Mwenyezi Mungu si wa kufanywa kwa maneno tu. Utumiaji sahihi wa neema hizo, kwa kuzifanyia mambo mema yakiwemo ya kuwahudumia waja wa Mwenyezi Mungu nako pia ni kushukuru neema zake Mola. Na vile vile aya hii inatutaka tuelewe kwamba jambo jema huwa na thamani pale linapofanywa kwa nia ya kupata radhi za Allah, si kutaka kuwa mashuhuri na kupata umaarufu mbele za watu.
Darsa yetu hii inahatimishwa na aya ya 20, 21 na 22 ambazo zinasema:


وَتَفَقَّدَ الطَّيْرَ فَقَالَ مَا لِيَ لا أَرَى الْهُدْهُدَ أَمْ كَانَ مِنَ الْغَائِبِينَ

Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona simwoni Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu?


لَأُعَذِّبَنَّهُ عَذَابًا شَدِيدًا أَوْ لَأَذْبَحَنَّهُ أَوْ لَيَأْتِيَنِّي بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ

Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au nitamchinja, au aniletee hoja ya kutosha.


فَمَكَثَ غَيْرَ بَعِيدٍ فَقَالَ أَحَطتُ بِمَا لَمْ تُحِطْ بِهِ وَجِئْتُكَ مِن سَبَإٍ بِنَبَإٍ يَقِينٍ

Basi (Hud-hud) hakukaa sana (akaja) na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na nimekujia hivi kutoka (nchi ya) Sabai, na khabari za yakini.


Katika aya zilizotangulia tulisema kuwa mbali na viumbe wengine, ndege pia walikuwa wakitiishwa na kumtumikia Nabii Suleiman (AS). Ndege hao walikuwa wakimpa ripoti Mtume huyo wa Allah juu ya yale yaliyokuwa yakijiri katika ardhi ya Sham na kando kando yake katika maeneo yaliyoizunguka. Katika aya hizi tulizosoma inaelezwa kwamba siku moja wakati Nabii Suleiman alipowakagua ndege wa utawala wake, alibaini kuwa ndege wote wapo isipokuwa Hud Hud; na ambaye inavyoonekana alishawahi huko nyuma kufanya hivyo pia. Kwa hivyo kwa lugha kali na nzito inayolazimu kutumiwa katika uendeshaji utawala, Nabii Suleiman akasema:" Ikiwa Hud Hud ameshindwa kuwepo hapa anapotakiwa kuhudumu kwa sababu ya uvivu na uzembe nitamchukulia hatua kali, pengine hata ya kumchinja, au aniletee hoja ya kuridhisha iliyomfanya asiwepo hapa. Lakini kutokuwepo kwa Hud Hud hakukudumu kwa muda mrefu mara akafika kwa Nabii Suleiman na kumwambia: mimi nilikuwa nimefanya safari kuelekea ardhi ya Saba'a. Na huko nimeona mambo ambayo wewe huna taarifa nayo; hivyo nitakueleza habari za yale niliyoyakuta huko. Kwa maelezo hayo Hud Hud akaweza kutoa sababu ya kumridhisha Nabii Suleiman juu ya kutokuwepo kwake na kusalimika na adhabu ambayo angeipata. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kufuatilia mtu habari za waliochini yake na kutaka kujua hali zao ni katika sira na mwenendo wa mawalii wa Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwa na akili hodari, umakini na udhibiti imara wa mambo ni masharti ya lazima kwa ajili ya uongozi wa jamii; kama ambavyo Nabii Suleiman (AS) alikuwa na umakini wa kufuatilia mambo yote katika utawala wake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba katika mfumo na taasisi ya utawala upuuzaji na kuyachukulia mambo kwa wepesi hakukubaliki. Hatua kali inapasa wachukuliwe wanaokhalifu kutekeleza majukumu yao ili liwe funzo kwa wengine wasijaribu kufanya hivyo. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa kutumia mantiki na kukubali udhuru na sababu yenye kukubalika sambamba na kuwa thabiti na bila kufanya mzaha katika maamuzi ni mambo ya lazima katika uongozi na utawala wa Kiislamu. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 667 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aupe nguvu Uislamu na Waislamu, na awape nusra na ushindi dhidi ya maadui zao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)