Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 03 Oktoba 2015 11:30

Sura ya An-Naml, aya ya 12-16 (Darsa ya 666)

Sura ya An-Naml, aya ya 12-16 (Darsa ya 666)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 666, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 12 ambayo inasema:


وَأَدْخِلْ يَدَكَ فِي جَيْبِكَ تَخْرُجْ بَيْضَاء مِنْ غَيْرِ سُوءٍ فِي تِسْعِ آيَاتٍ إِلَى فِرْعَوْنَ وَقَوْمِهِ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ

Na ingiza mkono wako katika mfuko wako, utatoka mweupe bila ya kuwa na dosari. Ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na watu wake. Hakika wao walikuwa watu mafasiki.


Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Nabii Musa (AS), akiwa amefuatana na aila yake, alikuwa akielekea Misri wakati alipobaathiwa na Mola na kupewa Utume; na muujiza wake wa kwanza aliopewa ulikuwa ni wa fimbo kwa kuambiwa: Itupe fimbo yako. Alipofanya hivyo, fimbo hiyo iligeuka nyoka mdogo na kumfanya Nabii Musa aingiwe na hofu. Ikiendelea na maudhui hiyo, aya tuliyosoma inaashiria muujiza wa pili wa Musa (AS). Allah SW alimwambia Mtume wake: utie mkono wako kwapani mwako; utakapoutoa utakuwa mweupe na ung'arao pasina weupe huo kuwa wenye kutokana na ugonjwa wa mabalanga. Kisha Allah akamwambia Mtume wake: muujiza wako si vitu viwili hivi tu bali tumekuwekea miujiza mingine saba ambayo unaweza kuitumia wakati utakapo walingania Firauni na kaumu ya Bani Israil wito wa tauhidi; na kwa miujiza hiyo hawatokuwa na kisingizio chochote cha kutoa. Miongoni mwa miujiza hiyo ni kupasuka mto Nile na kuchomoza njia kavu ya kupita ndani yake na vile vile kutoka ndani ya jabali chemchemi 12 za maji. Kama ilivyosimuliwa katika aya nyengine za Qur'ani tukufu, wakati Firauni na jeshi lake walipomwandama Nabii Musa na watu wake wa Bani Israil walipokuwa wakihama Misri, kwa amri ya Allah, Musa (AS) alipiga fimbo yake kwenye maji ya Mto Nile, tahamaki mpasuko ukatokea na kufunguka njia kavu ya kupita Bani Israil. Aidha katika tukio jengine, Nabii Musa aliipiga fimbo yake kwenye jabali, na zikatokeza ndani ya jabali hilo chemchemi 12 za maji. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mfumo wa maumbile ni mahuluku na muumbwa wa Allah, hivyo lolote lile atakalo Yeye Mola linakuwa hata kama ni jambo lisilo la kawaida na lenye kutofautiana na utaratibu wa kawaida wa maumbile. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa baadhi ya kaumu na watu huchachamaa na kunga'ng'ania njia batili na ya upotofu kiasi kwamba muujiza mmoja tu huwa hautoshi kuwafanya waikubali haki bali huhitaji kuonyeshwa miujiza kadhaa ndipo labda nyoyo zao zitalainika na kuikubali haki.
Zifuatazo sasa ni aya za 13 na 14 ambazo zinasema:


فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ آيَاتُنَا مُبْصِرَةً قَالُوا هَذَا سِحْرٌ مُّبِينٌ

Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zionyeshazo, wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri.


وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ

Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!


Nabii Musa (AS) alianza kutekeleza jukumu alilopewa na Mola wake la Utume kwa kumwendea Firauni na watu wake na kuwafikishia wito wa tauhidi na kumwabudu Mungu mmoja tu wa haki. Lakini wakati taghuti huyo alipoiona miujiza ya Nabii Musa, badala ya kumwamini, alimtuhumu Mtume huyo wa Allah
kuwa ni mchawi. Aya zinaendelea kuzungumzia nukta hiyo kwa kusema: si kwamba tuhuma hizo zilitokana na shaka waliyokuwa nayo juu ya yale aliyowaonyesha Musa, bali ukweli ni kwamba waliyafahamu vyema maneno ya Mtume huyo na walitambua kwamba maneno hayo ni ya haki na ya kweli. Lakini kujikweza na kupenda kwao jaha ndiko kulikowafanya wakadhibishe maneno ya haki ya Musa (AS). Ilikuwa ni vigumu na uzito kwa wao kumtii na kumfuata mtu ambaye kijamii, alikuwa na hadhi ya chini kulinganisha na wao. Kwa sababu hiyo Firauni akaamua kutenda dhulma kubwa kwa kumtuhumu Mtume wa Mwenyezi Mungu Musa (AS) kuwa ni mchawi ili tu kuukataa ubora na utukufu wake juu yao. Tab'an dhulma hiyo aliyomfanyia Nabii Musa na dini ya haki aliyokuja nayo ilikuwa ni sawa na kuzidhulumu nafsi zao wenyewe kwa sababu hatima na mwisho wao ulikuwa mbaya na wa kutisha wa kugharikishwa kwenye maji ya Mto Nile. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba daraja ya imani ni ya juu zaidi kuliko elimu na yakini. Si hasha mtu akawa anaukubali ukweli ndani ya moyo wake na kuutambua kuwa ni haki, lakini pamoja na hayo akaukanusha na kutokuwa tayari kujisalimisha mbele ya haki. Imani ni kusalimu amri mbele ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa moja ya vizuizi vinavyomfanya mtu asiikubali haki, ni kibri na kujikweza, ambavyo humfanya mtu awadogoshe na kuwadunisha watu wengine kulinganisha na nafsi yake na kutoyathamini wala kuyajali wayasemayo. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa hatima ya wafanyao uharibifu na ufisadi ni kuporomoka na kuangamia. Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 15 na 16 ambazo zinasema:


وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ عِلْمًا وَقَالا الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي فَضَّلَنَا عَلَى كَثِيرٍ مِّنْ عِبَادِهِ الْمُؤْمِنِينَ

Na hakika tuliwapa Daudi na Sulaiman ilimu, na wakasema: Alhamdu Lillahi, Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu ambaye ametufadhilisha kuliko wengi katika waja wake Waumini.


وَوَرِثَ سُلَيْمَانُ دَاوُودَ وَقَالَ يَا أَيُّهَا النَّاسُ عُلِّمْنَا مَنطِقَ الطَّيْرِ وَأُوتِينَا مِن كُلِّ شَيْءٍ إِنَّ هَذَا لَهُوَ الْفَضْلُ الْمُبِينُ

Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri.


Baada ya kuzungumziwa yaliyojiri katika maisha ya Nabii Musa (AS), aya tulizosoma zinaelezea yale yaliyotokea katika maisha ya Manabii Daud na Suleiman (AS), ambao nao pia ni miongoni mwa Mitume wa Bani Israil. Mitume ambao hali na mazingira yao yalikuwa tofauti kabisa kulinganisha na Mitume wengine. Na miongoni mwa hali maalumu ya Mitume hao ni kwamba waliunda tawala kwa ajili ya kuendesha masuala ya jamii zao. Ikiwa Mitume wengine walikuwa wakiudhiwa na kutaabishwa na watu wao na hata kubaidishwa na kutolewa nje ya miji yao, Manabii Daud na Suleiman walifikia kilele cha nguvu, mamlaka na madaraka kiasi kwamba si wanaadamu pekee bali hata majini pia walikuwa wakitii amri zao. Aya hizi tulizosoma zinasema siri ya kuwa na nguvu za mamlaka na utawala Mitume hao wa Allah ilikuwa ni elimu na ujuzi maalumu ambao Mola aliwapa Manabii Daud na Suleiman (AS). Na kutokana na elimu hiyo wakaweza kuasisi utawala mkubwa na mpana. Elimu ambayo Mitume hao waliijua na kuienzi thamani yake, na wakamshukuru Allah SW kwa kuwajaalia elimu hiyo ambayo iliwafanya wawe na fadhila, utukufu na ubora kuliko watu wengine. Kisha aya zinaendelea kwa kuitaja moja ya elimu hizo za kujaaliwa na Mola ambayo ni kuweza kufahamu lugha za ndege na kuwa na uwezo wa kuzitumia suhula na neema zote za kimaada, na kuzielezea elimu hizo kuwa ni miongoni mwa mifano wadhiha na vielelezo vya wazi kabisa vya rehma na fadhila za Allah. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba elimu za Mitume ni za kuwa nazo ndani ya nafsi zao kupitia ilhamu tu wanayopewa na Mola, si za kujifunza. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dini na siasa hazitenganiki bali zimeshikamana kama chanda na pete. Ikiwa Utume na utawala vinajumuika pamoja, ni jambo linalokubalika kwa waumini kuingia kwenye masuala ya kisiasa kwa nia ya kuunda utawala wa kidini, au angalau kupambana na madola dhalimu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba uendeshaji nchi unapasa ufanyike kwa misingi ya elimu na ujuzi, si utashi binafsi wa mtu au wa kichama wa watawala. Na pia tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa elimu na neema nyengine zote tulizonazo tumezipata kwa rehma na fadhila zake Mola, si kwa ustahiki na uhodari wetu; hivyo kila mara tuwe tunamshukuru Allah, na si kuingiwa na ghururi na majivuno na kumsahau Yeye Mola. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 666 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake washukurivu kwa kauli na vitendo kutokana na kila neema aliyotupa. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)