Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 02 Oktoba 2015 19:06

Sura ya An-Naml, aya ya 6-11 (Darsa ya 665)

Sura ya An-Naml, aya ya 6-11 (Darsa ya 665)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 665, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 27 ya An-Naml. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya 6 ambayo inasema:


وَإِنَّكَ لَتُلَقَّى الْقُرْآنَ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ عَلِيمٍ

Na kwa hakika wewe unapewa Qur'ani kutoka Kwake Mwenye hikima Mwenye kujua.


Sura hii ya An Naml imeanza kwa kuelezea adhama ya Qur'ani na nafasi yake katika kupata waumini uongofu na saada. Kisha ikaendelea kwa kuzungumzia sifa maalumu za waumini na vilevile hatima na mwisho wa watu wasioamini Siku ya Kiyama. Ikiendelea na maudhui hiyo na kabla ya kuanza kusimulia visa vya Mitume, aya ya sita tuliyosoma inasema: maarifa na mafunzo ya kitabu hiki cha mbinguni yanatokana na elimu na hikma ya Allah SW. Madhumuni ya elimu iliyokusudiwa hapa ni elimu isiyo na kikomo ya Mwenyezi Mungu Mwenye ujuzi mutlaki wa yale yenye kheri na yenye madhara kwa wanadamu; na hikma yake katika kupanga na kubainisha wajibu na sheria ambazo humkaribisha mtu kwenye lengo la kuumbwa kwake. Na baada ya hayo, katika aya zitakazofuatia tutaona baadhi ya mifano ya elimu na hikma hiyo ya Allah SW katika matukio ya kubaathiwa na kupewa Utume Manabii mbalimbali. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Qur'ani ni dhihirisho la elimu na hikma ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Elimu ya Bwana Mtume pia, ambaye ni mpokezi wa wahyi, ni elimu ya kupewa na Allah si ya kujifunza. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa hukumu na maamrisho ya dini chimbuko lake ni elimu mutlaki ya Mola Muumba, na kila moja kati ya hukumu za dini ina hikma iliyojifcha ndani yake japokuwa sisi hatuijui na wala hatuna njia ya kutuwezesha kuibaini.
Ifuatayo sasa ni aya ya 7 hadi ya 9 za sura yetu ya An-Naml ambazo zinasema:


إِذْ قَالَ مُوسَى لِأَهْلِهِ إِنِّي آنَسْتُ نَارًا سَآتِيكُم مِّنْهَا بِخَبَرٍ أَوْ آتِيكُم بِشِهَابٍ قَبَسٍ لَّعَلَّكُمْ تَصْطَلُونَ

(Kumbuka) Musa alipo waambia ahli zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili mpate kuota moto.


فَلَمَّا جَاءَهَا نُودِيَ أَن بُورِكَ مَن فِي النَّارِ وَمَنْ حَوْلَهَا وَسُبْحَانَ اللَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.


يَا مُوسَى إِنَّهُ أَنَا اللَّهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ

Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.


Katika sura hii yamezungumziwa matukio yaliyojiri katika maisha ya Mitume wakubwa watano wa Mwenyezi Mungu na kaumu zao ikianza kusimuliwa jinsi alivyopewa Utume Nabii Musa (AS). Kwa mujibu wa ilivyopokewa katika hadithi ni kwamba wakati Nabii Musa na ahli zake alipokuwa akitoka kwa Nabii Shuaib na kuelekea Misri, ulipoingia usiku walipotea njia na kupigwa na baridi, tufani na upepo mkali. Musa (AS) alikuwa akifikiria mahali pa kupata hifadhi na njia ya kuwaokoa ahli zake, mara akaona moto kutokea mbali. Akajisemea moyoni mwake: Bila ya shaka kule kutakuweko na watu waliowasha moto ule, ambao wataweza kutusaidia au angalau kutuelekeza njia. Lakini kwa upande mwengine hakuweza kwenda huko akiandamana na ahli zake kwa sababu yamkini pia watu hao wangekuwa ni maharamia na wanyang'anyi. Kwa hivyo akawaambia ahli zake: bakini hapa hapa mnisubiri hadi nirudi; ima nitakuja na habari ya kutuongoza kuitambua njia au kwa uchache nitapata kijinga cha moto cha kuchukua na kuja nacho hapa kituondolee mzizimo wa baridi. Lakini wakati alipofika kulipokuwa na moto hakumwona mtu yeyote, bali aliona mandhari ya kustaajabisha mno. Moto ulikuwa ukitoka kwenye miti iliyonawiri kwa kijani kibichi na kusambaa kuelekea kila upande. Moja ya macheche ya moto huo yalimuelekea yeye na kumfanya ashtuke na kurudi nyuma. Hapo alisikia sauti ikinadi kwa kumwambia: "Ewe Musa usiogope! Mimi ni Mwenyezi Mungu Mwenye Nguvu na Mwenye Hikima; nimekuteua wewe uwe Mtume. Moto huu ni dhihirisho la nguvu zangu; hautokuunguza wewe wala ile miti ya kijani; na kila aliyemo ndani yake na kandokando yake yuko katika amani yangu." Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume walikuwa na maisha ya kawaida kabisa, na wakiishi kama walivyokuwa wakiishi watu wengine. Nabii Musa alihangaika ili kuweza kukidhi mahitaji ya ahli zake. Lakini akiwa katika hali hiyo akabaathiwa na Mola wake kuwa Mtume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa Allah atataka, basi moto pia utapoteza muunguzo wake na kutokuwa na hatari yoyote, kama ambavyo Nabii Ibrahim (AS) alipotiwa ndani yake, badala ya kumuunguza ulikuwa baridi na salama kwake.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 10 na 11 ambazo zinasema:


وَأَلْقِ عَصَاكَ فَلَمَّا رَآهَا تَهْتَزُّ كَأَنَّهَا جَانٌّ وَلَّى مُدْبِرًا وَلَمْ يُعَقِّبْ يَا مُوسَى لا تَخَفْ إِنِّي لا يَخَافُ لَدَيَّ الْمُرْسَلُونَ

Na itupe fimbo yako! Alipo iona ikitikisika kama nyoka, aligeuka nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu! Hakika hawakhofu mbele yangu Mitume.


إِلاَّ مَن ظَلَمَ ثُمَّ بَدَّلَ حُسْنًا بَعْدَ سُوءٍ فَإِنِّي غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Ila (yule) aliye dhulumu, kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi Mimi ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.


Ni wazi kwamba wakati aliposikia sauti ile ikimnadi pamoja na moto usio na madhara, Nabii Musa aliingiwa na shaka, kwamba atajuaje kama hayo anayoyasikia ni maneno ya Mwenyezi Mungu na hayo anayoyaona yanafanywa na Yeye. Ndipo Allah SW akamwamuru aitupe chini fimbo yake. Naye Musa (AS) akafanya hivyo. Mara ghafla ikageuka nyoka mdogo ambaye alianza kumwendea yeye. Nabii Musa alianza kukimbia kwa hofu, kwa sababu hakutarajia kuona mandhari ya ajabu kama hiyo. Hapo sauti ikanadi tena, kwamba "Ewe Musa hii ni alama ya Utume wako. Wewe sasa umefikia daraja ya Utume na risala; na hayo uliyoyaona ni muujiza wa kukupa hakikisho kwamba wito unaousikia unatoka kwa Mwenyezi Mungu wala hautokani na ilhamu za shetani. Na kwa kuwaonyesha watu muujiza huu, watakuwa na hakika kwamba wewe ni Mtume uliyetumwa na Mwenyezi Mungu, wala si mchawi na mfanya mazingaombwe. Ewe Musa mbele ya Mola wako ni mahala pa amani na utulivu, si pa kumtia mtu hofu na hamaniko. Mtu anayepasa kuwa na hofu ni yule aliyewadhulumu wenzake. Na tab'an yeye pia kama atatubia na kuacha dhulma na madhambi atapata rehma zetu." Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba muujiza huthibiti kwa irada na amri ya Allah SW japokuwa Mitume ndio wanaoionyesha kwa watu. Kwa hivyo kabla ya mambo hayo yasiyo ya kawaida kuwa ni muujiza kwa watu, huwa ni muujiza kwanza kwa Mitume wenyewe na kitulizo cha nyoyo zao kiimani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika mtazamo wa mafundisho ya dini dhalimu inapasa daima awe katika hali ya hofu na kiwewe, si katika amani, raha na utulivu. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba msamaha wa Allah unakuja baada ya mtu kufanya amali njema na kufidia madhambi aliyoyatanguliza. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 665 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atusamehe madhambi yetu, atutakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)