Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 02 Oktoba 2015 19:05

Sura ya An-Naml, aya ya 1-5 (Darsa ya 664)

Sura ya An-Naml, aya ya 1-5 (Darsa ya 664)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 664 ambapo baada ya kuhatimisha tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 26 ya Ash-Shua'raa katika darsa hii ya leo tutaanza kuzungumzia sura ya 27 ya An-Naml. Majina ya baadhi ya sura za Qur'ani tukufu yanatokana na vitu vya kimaumbile pamoja na wanyama. Sura hii, ambayo ni miongoni mwa sura hizo imepewa jina la Naml, yenye ya mdudu chungu, ambalo limetokana na aya ya 18 ya sura hii inayosimulia mazungumzo yaliyokuwa yakijiri baina ya wadudu chungu wakati lilipokuwa likipita jeshi la Nabii Suleiman (AS). Baada ya maelezo haya mafupi tunaianza darsa yetu ya leo kwa tarjumi na maelezo ya aya ya kwanza na ya pili ya sura hii ya An-Naml ambazo zinasema:

 

طس تِلْكَ آيَاتُ الْقُرْآنِ وَكِتَابٍ مُّبِينٍ

T'aa Siin. (T'.S.), Hizi ni Aya za Qur'ani na Kitabu kinacho bainisha;

هُدًى وَبُشْرَى لِلْمُؤْمِنِينَ

Uwongofu na bishara kwa Waumini,


Sura hii, kama zilivyo sura nyengine 28 za Qur'ani imeanza kwa herufi za mkato; na kama zilivyo sura nyengine ikimaanisha adhama ya Kitabu hicho tukufu. Yaani Qur'ani, ni kitabu kilichotumia herufi na alfabeti hizi hizi za kawaida zinazotumiwa na watu wote, lakini hakuna mwanadamu yeyote mwenye uwezo wa kuleta hata sura moja iliyo mfano wa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Aya za kitabu hiki ziko wazi, na zenyewe zinaweka wazi kwa kudhihirisha na kupambanua baina ya haki na batili. Qur'ani imekuja ili kuwa mwongozo wa uongofu kwa ajili ya watu wote, lakini bila ya shaka watakaonufaika na kufaidika nayo na kufikia kwenye saada ni wale watakaoiamini na kuukubali ukweli wake. Na aya zake ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Aya alizoteremshiwa Bwana Mtume Muhammad SAW zina majina mawili. Moja ni "Qur'ani" kwa kuwa mtukufu hiyo alikuwa akiwasomea watu aya hizo; na jina jengine ni "kitabu", kwa sababu baada ya kusomewa watu, aya hizo zilikuwa zikiandikwa pia na baadhi ya masahaba wa Bwana Mtume SAW. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba harakati ya Mitume katika jamii ni harakati ya kitamaduni iliyoambatana na usomaji na uandikaji na kwa msingi wa kubainisha haki na batili. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kati ya sifa maalumu za Qur'ani ni kuwa kwake kitabu kilichoandikwa, chenye kupambanua, chenye mwongozo wa uongofu na kutoa bishara njema. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba bishara njema na ya kweli kwa watu inapatikana kwa wao kufuata njia ya haki na ukweli.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 3 hadi ya 5 ambazo zinasema:


الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ

Ambao wanasimamisha Sala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini nayo.


إِنَّ الَّذِينَ لا يُؤْمِنُونَ بِالآخِرَةِ زَيَّنَّا لَهُمْ أَعْمَالَهُمْ فَهُمْ يَعْمَهُونَ

Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo vyao, kwa hivyo wanatangatanga ovyo.


أُوْلَئِكَ الَّذِينَ لَهُمْ سُوءُ الْعَذَابِ وَهُمْ فِي الآخِرَةِ هُمُ الأَخْسَرُونَ

Hao ndio watakaopata adhabu mbaya, na wao katika Akhera ndio watakaopata khasara zaidi.


Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyoanzia katika aya zilizotangulia ambapo kwanza zinabainisha sifa maalumu za waumini. Mbili ni za tabia na mwenendo wao na moja ni sifa yao ya kifikra. Kusimamisha Sala na kutoa Zaka ni sifa mbili za wazi kabisa za waumini; na mtu yeyote yule asiye na sifa hizi, basi si mkweli katika kudai kwake kwamba yeye ni muumini. Amma la muhimu zaidi ya Sala na Zaka ni kuamini juu ya kuwepo ulimwengu wa baada ya kifo; kwani kama mtu hatoliamini hilo, atatekwa na dunia na mapambo yake, mpaka kufikia hadi ya mapenzi ya mali na vyeo vya kidunia kumfanya aikanushe akhera na kutofanya chochote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ni wazi kuwa mtu asiye na imani juu ya akhera, kwake yeye mambo maovu na machafu huonekana mazuri na yenye thamani na huamua kuyaendea. Mambo ambayo Siku ya Kiyama yatamfanya mtu huyo afikwe na adhabu kali. Katika aya mbalimbali za Qur'ani imeelezwa kwamba shetani ana sifa ya kuyafanya mambo maovu na machafu yaonekane mazuri na safi mbele ya macho ya watu, lakini ni katika aya hii tu tuliyosoma na aya nyengine moja ya Qur'ani ambapo kumenasibishwa na Allah SW kuyafanya mambo maovu yaonekane mazuri mbele ya macho ya watu. Huenda sababu yake ikawa ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia hulka hii kuwemo ndani ya nafsi ya mtu; na kikawaida kurudia tena na tena kufanya jambo lolote lile huathiri nafsi na hulka ya mtu na baada ya muda kuibadilisha kabisa shakhsia yake. Wakati mtu anapofanya tendo ovu, hisia ya kuhisi uovu wa tendo hilo huanza kufutika kidogo kidogo ndani ya nafsi yake na kulihisi kuwa jambo la kawaida, mpaka anafikia hadi ya kutoa hoja za kuhalalisha tendo au matendo maovu anayofanya; na kama ataendelea hivyo hivyo, hufikia mahala akaliona tendo ovu analofanya ni jema na hata kuwashajiisha wengine walifanye. Mtu kama huyo, kwa kudhani kuwa analolifanya ni zuri na jema, huwa kwa kweli anajiongezea mzigo wa amali zake mbaya. Na bila ya shaka kadiri anavyozidi kufanya mambo hayo ndivyo anavyozidi pia kukengeuka njia ya haki na kutumbukia kwenye lindi la dhalala na upotofu. Mwisho wake huwa ni kupotea rasilimali adhimu ya umri na uhai wake, na Siku ya Kiyama kujiona ni miongoni mwa watu waliopata hasara kubwa zaidi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mojawapo ya ubora wa dini tukufu ya Uislamu ni kwamba umeyafungamanisha mahusiano ya mja na Allah na mahusiano ya mja na wanadamu wenzake walio wanyonge na wasio na kitu katika jamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuzoea matendo mema au mabaya ni matokeo ya maumbile aliyojaaliwa nayo mwanadamu; hivyo kama kanuni na kaida hiyo ya kimaumbile haitotumiwa katika njia sahihi, mtu hufikwa na madhara na hasara zisizoweza kufidika. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kama tutakuwa na imani ya kweli juu ya Kiyama tutajiepusha kuyafanya mambo mengi ambayo mbele ya macho yetu yanaonekana mazuri na yenye kuvutia. Na hapo tutakuwa tumefuata muongozo wa mafundisho ya dini na kuzikataa thamani na mambo yasiyokuwa ya dini. Na katika hali hiyo kutembea uchi hakutoonekana tena mbele ya akili na macho yetu kuwa ni alama ya ustaarabu; kufanya mambo ya fahari na israfu hakitokuwa tena kipimo cha mtu kujihisi kuwa shakhsia mtajika; na wala kipimo cha haki na batili katika mtazamo wetu hakitokuwa tena maslahi yetu binafsi au hata utaifa wetu. Vile vile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba kuikufuru na kuikanusha Siku ya Kiyama kutamletea mtu hasara kubwa isiyo na mfano. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah azijaze nyoyo zetu imani ya yakini juu ya Kiyama itakayotuwezesha kuitumia neema ya maisha haya ya kupita kwa ajili ya maisha ya milele huko akhera. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)