Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:41

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 112-118 (Darsa ya 605)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 605 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 112, 113 na 114 ambazo zinasema:

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ

Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa idadi ya miaka?

قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلْ الْعَادِّينَ

Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanaoweka hisabu.

قَالَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلاَّ قَلِيلا لَّوْ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

Atasema: Nyinyi hamkukaa (huko duniani) ila kidogo, laiti ingelikuwa mnajua.

Aya tulizosoma katika darsa iliyopita ziliashiria mazungumzo yaliyojiri baina ya Allah SW na watu wa motoni, mazungumzo ambayo yanaendelea kunukuliwa na aya tulizosoma kwa kueleza kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atawauliza watu hao kuhusu umri walioishi duniani kuwa waliishi kwa muda wa miaka mingapi hapa ardhini? Watu hao watajibu kwa kusema: ewe Mola! Kama unataka kujua kuhusu idadi halisi ya siku na miaka tuliyoishi, bora uwaulize malaika wako waliokuwa na jukumu la kuweka rekodi na hisabu za umri wetu na yote tuliyokuwa tukiyafanya. Sisi tumo katika adhabu na kwa hivyo hatuwezi kukumbuka chochote. Tuonavyo sisi, muda wote wa uhai wetu duniani haukutimia hata kutwa na kucha moja seuze wiki, mwezi na mwaka. Allah SW atathibitisha kuungama kwao kwamba umri na uhai wa duniani ni mfupi mno na kuwaeleza watu hao kuwa: Nyinyi mumelimaizi na kulitambua hilo sasa baada ya kufikishwa hapa kwenye Siku ya Kiyama. Laiti mlipokuwako duniani mkawa mnashupalia kufanya madhambi na maasi mngalijua kwamba kuna siku hii inakuja, na dunia haina thamani yoyote kulinganisha na siku hii. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Siku ya Kiyama kuna watu ambao watapata majuto makubwa kwa sababu itawabainikia kuwa wamekhitari adhabu ya milele ya akhera kwa sababu ya raha na starehe za siku chache hapa duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa dunia ni mithili ya daraja ambalo tunalivuka kwa kupita juu yake kwa muda wa siku moja au muda fulani tu wa siku. Kwa hivyo tutahadhari mandhari zenye mvuto za kandokando ya daraja hilo zisije zikatufanya tukaacha kuupa umuhimu upande wa pili wa daraja hilo, ambao ni kwenye maisha ya milele ya akhera.

Ifuatayo sasa ni aya ya 115 ambayo inasema:

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لا تُرْجَعُونَ

Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?

Aya hii inaashiria falsafa ya kuwepo akhera na kueleza kuwa kama hakutokuwepo na Siku ya Kiyama maisha ya dunia hayatokuwa na maana na yatakuwa ni kitu cha upuuzi tu. Na sababu ni kwamba kwa ajili ya maisha ya kimaada ya duniani kusingekuwepo  na haja ya kuandaliwa suhula na nyenzo zote hizi ambazo Allah SW amewawekea wanadamu, bali wanadamu, kama walivyo wanyama wengi, wangeweza kutumia na kuneemeka na neema na starehe za dunia bila ya kuhitajia akili, kufikiri wala hiyari ya kufanya mambo.

Ikiwa Mwenyezi Mungu ametoa upendeleo maalumu kwa wanadamu na kuwataka wachague kwa hiyari yao na kutumia akili na uelewa katika mambo na matendo wayafanyayo, basi lazima wakaone natija na matunda ya amali na matendo yao. Vinginevyo, matendo mema na mabaya yatakuwa na hali sawa na dhulma na maovu yataenea kila mahala. Hebu na tujiulize, ni jambo linaloingia akilini kweli, kwamba ulimwengu huu wenye adhama, na mwanadamu huyu aliyetunukiwa chungu ya vipawa na uwezo vimeumbwa na Muumba mjuzi na mwenye hekima, kisha maisha ya mwanadamu yafikie kikomo na yeye kutoweka moja kwa moja pasina kuulizwa, kuhesabiwa na kulipwa kwa aliyoyatenda? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kuumbwa kwa mwanadamu ambaye ni sehemu ya ulimwengu huu mpana hakuwezi kuwe kumefanyika bure bure na bila ya lengo lolote, labda tusiwe tunaamini kuweko kwa Mwenyezi Mungu au tusiwe tunaamini pia kwamba Yeye Mola ni mwenye hekima. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa ghaya na lengo kuu la kuumbwa mwanadamu litadhihirika katika Ulimwengu wa Akhera, na kufikiria kuwepo ulimwengu wa dunia bila ya kuwepo ulimwengu wa akhera ni tafakuri na taswira pungufu na yenye utata juu ya mwanadamu.

Tunaiendeleza darsa yetu hii kwa aya za 116 na 117 ambazo zinasema:

فَتَعَالَى اللَّهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ

Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu.

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ لا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ إِنَّهُ لا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

Na anayemuomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwengine hana ushahidi wa hili; basi bila ya shaka hisabu yake iko kwa Mola wake Mlezi. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi.

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinatilia mkazo suala kwamba mfumo wa ulimwengu na uumbwaji wa mwanadamu si mambo yaliyofanywa vivi hivi tu bila ya sababu, na kueleza kwamba, Allah SW ni Muumba na pia ni Mola; ni Mfalme Mmiliki wa kila kitu na vilevile ni mtawala wa kila jambo. Kama ni hivyo inawezekenaje kwa Mola kama huyu kufanya jambo burebure na lisilo na maana? Ikiwa Yeye Mola ambaye hana sifa yoyote ya kasoro kama ya kutokuwa mjuzi na kutokuwa mweza wa kufanya jambo, na Yeye ambaye ndiye chimbuko la elimu na hekima amemkataza kiumbe wake mwanadamu kufanya mambo ya upuuzi na yasiyo na maana, itawezekanaje kukubali kwamba Yeye mwenyewe Mola Mweza, Mwenye hekima na aliyetakasika afanye jambo la upuuzi na lisilo na maana? Kama katika uumbaji na uendeshaji wa ulimwengu, Yeye Allah SW angekuwa na mshirika ingeyumkinika kutokea mparaganyiko katika mfumo wa ulimwengu na katika lengo la kuumbwa kwa mwanadamu. Lakini ni wazi kwamba ni muhali kuthibiti kwa dhana kama hiyo na hakuna akili timamu inayoweza kukubali kuwepo Mola mwengine mfano wa Allah SW seuze kumfanya yeyote yule kuwa ni mshirika wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu ametukuka na yuko juu ya kila kitu kinachoweza kutupitikia akilini mwetu. Kwani chochote kile zitakachozitasawari akili zetu ni kitu pungufu na chenye kasoro. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa ulimwengu wa maumbile muda wote uko chini ya tadbiri na uendeshaji wa Mwenyezi Mungu, na si kwamba Yeye Mola ameuumba tu kisha akauacha kama ulivyo.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 118, na ambayo pia ndiyo aya ya mwisho ya sura yetu hii ya al Muuminun ambayo inasema:

وَقُل رَّبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ

Nawe sema: Mola wangu Mlezi! Ghufiria na urehemu nawe ni Mbora wa wanaorehemu.

Katika aya hii ya mwisho ya Suratul Muuminun, Mwenyezi Mungu SW anamfunza Mtume wake na waumini kwamba muda wote wawe wanamuelekea Yeye na kuomba fadhila na rehma zake zisizo na ukomo. Na wajue kwamba rehma na mapenzi yake Yeye Mola Muumba kwa waja wake ni makubwa zaidi ya mwengine yeyote yule. Wengineo huwa na mapenzi na sisi kama tutakuwa tanawafanyia mazuri, lakini endapo tutaleza na kuwakosea, mahaba na mapenzi yao kwetu hupungua, bali hata baadhi ya wakati huvunja kabisa uhusiano baina yao na sisi. Lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma na huruma hayuko hivyo. Yeye anawapenda hata waja wake wanaomkosea, na anawaita kwa kuwaambia: Njooni kwangu ili nikusameheni na kukuteremshieni rehma zangu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hakuna mtu yeyote, hata Mitume, asiyehitajia fadhila, uraufu na rehma za Mola Muumba wa ulimwengu, na wao wote wanapaswa kudhihirisha ujao wao kwake na kutaradhia shida na haja zao. Kadhalika aya hii inatuelimisha kuwa daima tujione kuwa sisi ni wenye makosa na taksiri mbele ya Allah SW, na kumwomba maghufira na msamaha kwa sababu ya taksiri na makosa tunayoyafanya. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 605 ya Qur'ani imefikia tamati na ambayo imetuhitimishia pia tarjumi na maelezo ya sura ya 23 ya al Muuminun. Tunamwomba Mola atupe taufiki ya kuyatekeleza na kuyafanyia kazi yale yote tuliyojifunza katika sura hii, amin.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)