Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:36

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 105-111 (Darsa ya 604)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 604 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 105 na 106 ambazo zinasema:

أَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَى عَلَيْكُمْ فَكُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ

Je! Hazikuwa Aya zangu mkisomewa, na nyinyi mkizikadhibisha?

قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ

Watasema: Mola wetu Mlezi! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tuliopotea.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoeleza kuwa kipimo kitakachotumiwa kuwalipa thawabu na ikabu waja Siku ya Kiyama kitakuwa ni amali zao njema na mbaya walizofanya hapa duniani na kisha zikaashiria pia adhabu kali watakayopata watu wa motoni. Katika aya hizi tulizosoma Mwenyezi Mungu Mtukufu anawahutubu watu wa motoni kwa kuwauliza: Sikukuleteeni nyinyi aya na ishara za wazi kupitia Mitume wangu na kukuwekeeni njia na suhula za kuufikia uongofu? Kwa nini basi badala ya kuikubali haki mliipinga na kuwa makafiri na wakanushaji? Jibu watakalotoa makafiri kwa Allah ni kwamba nyoyo zetu zilizidiwa na uovu na kuwa ngumu na yabisi kama mawe kiasi kwamba hakuna neno lolote la haki lililoweza kupenya ndani yake na hivyo tukaishia kwenye dhalala na upotovu. Ni wazi kuwa watatoa jibu hilo ili kuhalalisha na kutetea matendo maovu waliyofanya duniani. Kwa sababu ni kutokana na amali zao chafu ndipo nyoyo zao zikakubuhu na kuwa ngumu na yabisi na kutoujali wala kuukubali wito wa haki; na si kwamba tangu walipozaliwa walikuwa na nyoyo hizo ngumu na yabisi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba adhabu na ikabu ya Mola kwa waja inakuja baada ya Mitume na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo kukamilisha hoja na kuondoa dhima kwa watu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Siku ya Kiyama watu waovu wataungama kwa madhambi na makosa yao, lakini watakuwa wamechelewa katika kukiri na kuungama kwao huko kwani hakutowaletea tija wala faida yoyote.

Zifuatazo sasa ni aya za 107 na 108 ambazo zinasema:

رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْهَا فَإِنْ عُدْنَا فَإِنَّا ظَالِمُونَ

Mola wetu Mlezi! Tutoe humu Motoni. Na tutakaporudia, basi kweli sisi ni wenye kudhulumu.

قَالَ اخْسَؤُوا فِيهَا وَلا تُكَلِّمُونِ

Atasema Mwenyezi Mungu: Tokomeeni humo, wala msinisemeshe.

Baada ya waovu na makafiri kuungama makosa na madhambi yao watamwomba Mwenyezi Mungu awatoe motoni; na zaidi ya hilo awarudishe tena duniani ili wakajirekebishe, watengenee na kuyafidia makosa waliyofanya huko nyuma. Watafanya hivyo hali ya kuwa kutekelezwa ombi hilo hakutoyumkinika kwa sababu hakutokuwepo na njia ya kurudi duniani, na Siku ya Kiyama ni siku ya malipo na si ya kufanya tena amali yoyote ile. Katika lahadha hiyo Allah SW atawatimua mbele ya hadhara yake, na kwa kutumia lugha kali inayotumika kumfukuza mbwa atawaambia: Tokomeeni huko, nyinyi hamstahiki kusema chochote. Mahali penu nyinyi ni motoni, na mnachostahiki nyinyi ni huko kuuungua ndani ya moto huo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba madamu tungaliko duniani na fursa ingali imebaki tujipinde kufanya mema na ya kheri ili huzuni na majuto yetu Siku ya Kiyama yawe machache. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kiburi, ukafiri na inadi huishusha hadhi na thamani ya mwanadamu kufikia kiwango cha hayawani na wanyama, na kubadilika huko kwa utambulisho wa mtu kutajidhihirisha Siku ya Kiyama.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 109, 110 na 111 ambazo zinasema:

إِنَّهُ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْ عِبَادِي يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ

Hakika lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini; basi tusamehe na uturehemu, nawe ndiwe Mbora wa wanaorehemu.

فَاتَّخَذْتُمُوهُمْ سِخْرِيًّا حَتَّى أَنسَوْكُمْ ذِكْرِي وَكُنتُم مِّنْهُمْ تَضْحَكُونَ

Lakini nyinyi mliwakejeli hata wakakusahaulisheni kunikumbuka, na mlikuwa mkiwacheka.

إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ

Hakika Mimi leo nimewalipa kwa vile walivyosubiri. Bila ya shaka hao ndio wenye kufuzu.

Katika aya zilizopita ilizungumziwa jinsi watu waovu watakavyofukuzwa na kuwekwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu. Aya hizi tulizosoma zinaitaja sababu ya kupatwa na adhabu na idhilali hiyo kwamba sio tu watu hao hawakuwa wakijuta na wala hawakuyaacha matendo maovu waliyokuwa wakiyafanya bali walikuwa wakiwafanyia shere na stihzai pia waumini ambao ni watu wenye kutubia na kuomba maghufira kwa Mola wao na wakawa wanawacheka kwa nia ya kuwadunisha na kuwadhalilisha. Ni kama kwamba wao walikuwa wakijiona watu wajanja na werevu na kuwaona waumini majuha na watu wenye kuamini haraka kila wanaloambiwa, ambao kila wanapofanya kosa lolote lile hukimbilia kwa Mwenyezi Mungu kuomba toba na maghufira kutokana na hofu ya moto wa Jahanamu. Lakini wale waliokuwa wakifanyiwa shere, kejeli na stihzai leo watakuwa peponi wakineemeka na kila aina ya raha na starehe, na wale waliokuwa wakiwafanyia shere na stihzai watatupwa ndani ya moto wa Jahanamu na wala hawatopata njia na mahala pa kukimbilia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba sharti la imani ya kweli ni kuomba maghufira na msamaha kwa Mola Mwenyezi, kwani muumini huwa muda wote anajihisi kuwa yeye ana makosa na mwenye taksiri mbele ya Mola wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuwafanyia stihzai na kuwadhalilisha waumini hufuta athari ya dhikri na utajo wa Allah ndani ya moyo wa mtu na kumtumbukiza kwenye lindi la hilaki ya moto wa Jahanamu. Aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba uokovu huko akhera unapatikana chini ya kivuli cha subira na istiqama. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 604 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola atughufirie madhambi yetu, atutakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)