Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:33

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 99-104 (Darsa ya 603)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 603 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 99 na 100 ambazo zinasema:

حَتَّى إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ

Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe.

لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلاَّ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَى يَوْمِ يُبْعَثُونَ

Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyoyaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.

Aya hizi zinaelezea hali ya washirikina, makafiri na watu wenye madhambi wakati wanapofikwa na mauti na kueleza kuwa katika lahadha hiyo ambapo watu hao hujihisi kuwa sasa wanatengana na dunia hii na kuelekea kwenye ulimwengu mwengine hapo ndipo pazia la mghafala waliokuwa nao linapowaondokea mbele ya macho yao na kuiona hatima chungu na ya kutisha iliyoko mbele yao. Wakati huo watatambua jinsi walivyopoteza umri na rasilimali ya uhai waliyopewa na kuuona mwisho mbaya wa madhambi waliyoyafanya. Na hapo ndipo watakapoanza kumwomba na kumsikitikia Mwenyezi Mungu awape fursa tena ya kurudi duniani ili waweze kwenda kuyatekeleza na kuyafidia yale waliyokuwa wameamrishwa kuyafanya lakini wakayapuuza na vilevile wakazitumie kwa mambo mema na ya kheri mali na utajiri waliokuwa wamejirundikia. Lakini hayo ni matarajio ya kutamani tu yanayodhihirishwa kwa maneno matupu, kwani hata kama watarejeshwa tena duniani hawatoyafanyia kazi hayo wanayoyasema kwa sababu Allah SW aliwapa fursa kubwa na muda wa kutosha wa kutubia na kufuata uongofu lakini walipuuza badala ya kuitumia fursa na muda huo waliopewa. Kisha aya zinaendelea kuashiria ulimwengu wa barzakhi, ambao ni ulimwengu wa baina ya dunia hii na akhera. Kwa mujibu wa Qur'ani na hadithi, baada ya kifo roho hutengana na kiwiliwili na kuelekea kwenye ulimwengu wa barzakhi. Siku ya Kiyama, wakati wafu watakapofufuliwa roho hiyo itaungana na kiwiliwili chake. Katika ulimwengu wa barzakhi waumini wameandaliwa mazingira ya raha za peponi kama ambavyo makafiri watayaonja machungu na adhabu za motoni. Katika hadithi za viongozi wa dini imeelezwa kuwa kaburi ama ni bustani kati ya mabustani ya peponi au shimo kati ya mashimo ya motoni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tuzitumie fursa tunazopewa, kwani majuto hapo baadaye hayatokuwa na faida au tija yoyote na wala zama hazitarudishwa nyuma tena. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kuupoteza na kuuharibu mtu umri wake humletea majuto wakati wa mauti; na zawadi bora ya kubeba mtu katika ulimwengu wa baada ya kifo ni amali njema.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 101 ambayo inasema:

فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ فَلا أَنسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلا يَتَسَاءَلُونَ

Basi litakapopulizwa baragumu hapo hautakuwapo ujamaa baina yao siku hiyo, wala hawataulizana.

Kwa mujibu wa aya na hadithi baragumu litapulizwa mara mbili; mara ya kwanza ni wakati wa kumalizika umri wa dunia hii na kupelekea kufariki viumbe hai wote; na mara ya pili ni wakati kitakaposimama Kiyama na kupelekea kufufuliwa wafu na hapo wanadamu watarejea kwenye maisha mapya katika ulimwengu wa akhera. Kwa kuzingatia aya iliyotangulia ambayo ilizungumzia mauti na kuingia kwenye ulimwengu wa barzakhi, hivyo madhumuni ya baragumu katika aya hii, ni lile baragumu la pili litakalofuatiwa na kufufuliwa viumbe. Katika mfumo wa kidunia wanadamu huzaliwa na mama, na mahusiano baina ya watu wa jamaa na familia hutokana na njia ya nasasba na ndoa. Lakini Siku ya Kiyama ambapo wanadamu watatolewa kutokea ardhini na kuwa hai tena, uhusiano wa kidunia utakatika baina yao na kila mtu atafufuliwa peke yake na  kwa hivyo hatokuwa na wa kumsaidia. Kwa hakika hofu na kitisho cha Siku ya Kiyama ni kikubwa kiasi kwamba hakuna mtu atakayetaka kuuliza na kujua kuhusu hali ya mwenzake na wala hatoshughulika kutafuta msaada wa mtu mwengine kwa sababu anajua kwamba ombi hilo halitokuwa na tija wala faida yoyote na wala hakuna mtu atakayekuwa na uwezo wa kumsaidia mwenzake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba tunatakiwa tufadhilishe kupata radhi za Mwenyezi Mungu kuliko radhi za wengine hata kama watakuwa ni jamaa na watu wetu wa karibu. Kwa sababu Siku ya Kiyama hakuna mwengine ghairi ya Yeye Mola atakayekuwa na uwezo wa kufanya chochote kile. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kujinasibu na kujifakharisha kwa majina ya kifamilia na ya kikabila huenda kukamletea tija mtu katika baadhi ya mambo hapa duniani, lakini Siku ya Kiyama hakutokuwa na faida yoyote.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 102, 103 na 104 ambazo zinasema:

فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

Basi wale ambao mizani zao zitakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu.

وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ

Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio waliozitia khasarani nafsi zao, na katika Jahannamu watadumu.

تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ

Moto utababua nyuso zao, nao watakuwa na nyuso zilizokunjana.

Kufufuka na kuwa hai tena wafu Siku ya Kiyama kutafanyika ili watu wasimamishwe mbele ya mahakama ya uadilifu ya Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla. Lakini kigezo na kipimo atakachokitumia Yeye Mola kulipa malipo ya thawabu au ikabu ni amali alizofanya mtu hapa duniani ambazo baada ya kupimwa ndizo zitakazoainisha hatima ya kila mtu. Amali njema na zenye thamani za mtu zitatenganishwa na zile ovu na chafu na hivyo ndivyo atakavyokabidhiwa kila mtu daftari la amali zake. Ni wazi kwamba yule ambaye aliupoteza uhai wake na kuuharibu umri wake kwa maovu na madhambi daftari lake la amali halitokuwa na thawabu na mema ya kumfanya aingizwe peponi; na badala yake ni kwamba madhambi na maovu aliyofanya yatakuwa sababu ya kutupwa ndani ya moto wa Jahanamu. Na kwa sababu ya machungu makubwa ya adhabu kali atakayopata uso wake utasinyaa na kukunjana. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba matendo yetu hapa duniani yana tija na athari inayobaki hadi Siku ya Kiyama na ndiyo yatakayoainisha hatima ya maisha yetu ya milele huko akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hasara kubwa kabisa ni mtu kupoteza rasilimali ya uhai wake na neema za kiutu alizopewa na si hasara ya mali na uchumi anayopata katika maisha yake. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 603 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye mizani za amali zetu njema Siku ya Kiyama ziwe nzito na atujaalie kuwa miongoni wa watakaopata rehma ya kuingizwa katika Pepo yake ya milele, amin.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)