Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:26

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 91-98 (Darsa ya 602)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 602 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu hii kwa aya za 91 na 92 ambazo zinasema:

مَا اتَّخَذَ اللَّهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَهٍ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلا بَعْضُهُمْ عَلَى بَعْضٍ سُبْحَانَ اللَّهِ عَمَّا يَصِفُونَ

Mwenyezi Mungu hakujifanyia mwana, wala hakuwa pamoja naye mungu mwengine. Ingekuwa hivyo basi kila mungu angelichukua alivyoumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine. Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazomsifu.

عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ

Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, na ametukuka juu ya hayo wanayomshirikisha nayo.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia mamlaka na utawala mutlaki wa Allah SW juu ya ulimwengu wa maumbile. Aya hizi tulizosoma zinaashiria baadhi ya imani na itikadi za khurafa na uzushi zilizopo juu ya Mwenyezi Mungu na kueleza kwamba imani na itikadi hizo ni batili na potofu. Kati ya wafuasi wa dini zilizopita kumekuwepo na imani ya kumuitakidia kuwa na mwana Mola Muumba aliyetakasika na kila kasoro. Wakristo wana imani kuwa Nabii Issa Masih (AS) ni mwana wa Mungu. Washirikina wa Makka, wao walikuwa na fikra kwamba malaika ni mabanati wa Mwenyezi Mungu. Mbali na hao, katika zama zote za historia na kati ya kaumu na mataifa mbalimbali zilienea pia imani na itikadi za kuwepo miungu kadha wa kadha ambao kila mmoja kati yao ana mamlaka ya uendeshaji sehemu fulani ya masuala ya ulimwengu. Aya hizi tulizosoma zinatoa jibu kwa itikadi zote hizo kwa kusema: Kuna mfumo mmoja tu unaotawala juu ya mbingu na ardhi na viumbe vyote vya ulimwengu, ambao ni dhihirisho la kuwepo tadbiri moja tu na uthabiti wa kanuni zinazotawala viumbe vyote hivyo. Laiti kama tutachukulia kwamba ulimwengu huu una miungu kadhaa bila shaka utazuka mchanganyiko katika uendeshaji wa masuala ya ulimwengu ambao utasababisha hali ya mparaganyiko na mvurugiko katika masuala ya ulimwengu. Isitoshe ni kwamba yumkini wakati wowote ule mmoja wa miungu hao anaweza kwa sababu fulani, akaamua kuingilia eneo la mamlaka ya miungu wengine ili kupanua eneo la satua na mamlaka yake. Na hata kama tutajaalia kwamba miungu hao ni waola wenye hekima na uelewa, lakini kwa kukubali tu kuwa wao ni miungu kadhaa basi lazima watatafautiana tu kwa sababu kama waungu hao watalingana na kuwa na hali sawa na za namna moja katika mambo yote, hawatokuwa tena miungu kadhaa. Na kimsingi ni kwamba kila penye hitilafu na tofauti, tutake tusitake, hitilafu hizo zitaathiri uendeshaji na utendaji na kusababisha hali ya shaghalabaghala katika mfumo mzima wa ulimwengu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa na mwana na mshirika ni ishara ya kuwa mhitaji na kuwa na uwezo wenye mpaka maalumu. Hali ya kuwa Allah SW si mhitaji wa yeyote au chochote kile na wala uwezo na mamlaka yake mutlaki hayana ukomo au mpaka wowote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuitakidi na kuamini kwamba Mwenyezi Mungu jalla fii ulaahu, ametakasika na kila fikra potofu na ya khurafa inayompitikia mja akilini mwake ni miongoni mwa mafunzo ya Qur'ani tukufu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 93, 94 na 95 ambazo zinasema:

قُل رَّبِّ إِمَّا تُرِيَنِّي مَا يُوعَدُونَ

Sema: Mola wangu Mlezi! Ukinionyesha (adhabu) waliyoahidiwa,

رَبِّ فَلا تَجْعَلْنِي فِي الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

Mola wangu Mlezi! Usinijaalie katika watu madhaalimu.

وَإِنَّا عَلَى أَن نُّرِيَكَ مَا نَعِدُهُمْ لَقَادِرُونَ

Na hakika Sisi ni waweza wa kukuonyesha tuliyowaahidi.

Baada ya aya zilizotangulia kuvunja hoja za mtazamo potofu wa washirikina, aya hizi zinaashiria adhabu kali itakayowapata watu hao na kueleza kwamba yeye Mtume mwenyewe anajilinda na anaomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu amlinde na hatari ya kuandamana na kuwa pamoja na washirikina, kwa sababu yeye anajua kwamba hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kuvumilia ghadhabu na onjo la adhabu ya Allah ya hapa duniani seuze tena adhabu halisi ya huko Akhera.

Kushindwa washirikina na Waislamu katika vita vya Badr ulikuwa mfano mmojawapo wa ghadhabu hizo za Mwenyezi Mungu, ambapo kundi dogo, lakini la watu waumini, liliweza kulisambaratisha na kulishinda kundi kubwa la watu, lakini wasio na imani, na tukio hilo kuwa ibra na mazingatio katika historia. Tab'an kaida na utaratibu aliouweka Allah SW ni kutoa muhula wa fursa kwa makafiri na washirikina, ili kwa upande mmoja kuondoa dhima na kwa upande mwengine kuwafungulia na kuwawekea wazi mlango wa toba na kurejea kwake kwa madhambi waliyofanya endapo wao wenyewe watakhitari kufanya hivyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuhudhuria vikao vya watu madhalimu na kuchanganyika nao kuna hatari ya kumfanya mtu afikwe na yale yatakayowapata watu hao kwa sababu ya dhulma waliyofanya. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kutoshuhudia kwa macho yetu mwisho mbaya wa makafiri kusitufanye kuwa na shaka juu ya nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 602 inahatimishwa na aya za 96, 97 na 98 ambazo zinasema:

ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ

Kinga maovu kwa (kutenda) yaliyo mema zaidi. Sisi tunajua wayasemayo.

وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ

Na sema: Mola wangu Mlezi! Najikinga kwako na wasiwasi wa mashet'ani.

وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ

Na najikinga kwako, Mola wangu Mlezi, wasinikaribie.

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinamfahamisha Bwana Mtume Muhammad SAW jinsi ya kuamiliana na washirikina na makafiri na kumweleza kwamba: wao wanatumia ndimi zao kuvurumiza tuhuma mbalimbali dhidi yako ikiwemo kudai kuwa wewe ni mshairi na mwendawazimu. Katika muamala pia wanakufanyia maudhi na kukuwekea vizuizi usiweze kutekeleza kazi yako; lakini wewe wachukulie, na badala ya kuwalipizia kwa kutumia lugha chafu na mwenendo muovu kama wao, amiliana nao kwa wema na upole na kuandaa mazingira ya wao kuukubali wito wa haki na kufuata uongofu. Wewe wasamehe kwa mabaya wanayokutendea; na tumia lugha ya mantiki na hoja za wazi kabisa kukabiliana na maneno yao ya batili, na wala usiwe na pupa na haraka ya kutaka wao waamini, kwa sababu sisi tuna habari na utambuzi wa mambo yote ya ubaya na maovu wanayokutendea na subira na uvumilivu wako wewe. Wewe tahadhari tu usije ukatekwa na wasiwasi wa shetani na wala usiamiliane nao kama wao wanavyoamiliana na wewe. Tab'an kabla ya wao kusilimu na kuwa waumini wasiwe na nafasi yoyote mbele yako na wala wasichanganyike na kuwa pamoja na wewe. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba njia bora zaidi ya kuwalingania wapinzani wito wa haki ni kutumia maneno ya mantiki na mwenendo mwema na wa upole mkabala na maneno yao machafu na muamala wao mbaya. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa ikiwa Mitume walio maasumu wanajilinda kwa Mwenyezi Mungu na hatari ya wasiwasi wa shetani, vipi inapasa kuwa hali yetu sisi watu wa kawaida tunaoweza kufanya makosa na madhambi wakati wowote. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 602 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaowafanya watu wavutiwe na Uislamu kutokana na maneno yao mazuri na tabia na akhlaqi zao njema.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)