Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:17

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 81-90 (Darsa ya 601)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 601 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 81, 82 na 83 ambazo zinasema:

بَلْ قَالُوا مِثْلَ مَا قَالَ الأَوَّلُونَ

Bali walisema kama walivyosema wa mwanzo.

قَالُوا أَئِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَئِنَّا لَمَبْعُوثُونَ

Walisema: Je! Tukishakufa tukawa udongo na mifupa ndio tutafufuliwa?

لَقَدْ وُعِدْنَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا هَذَا مِن قَبْلُ إِنْ هَذَا إِلاَّ أَسَاطِيرُ الأَوَّلِينَ

Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni ngano za watu wa zamani.

Katika aya tulizosoma katika darsa iliyopita, Qur'ani tukufu imeashiria marejeo ya wanadamu kwa Mola wao Allah SW Siku ya Kiyama. Aya hizi tulizosoma zinazungumzia radiamali na mtazamo wa makafiri na washirikina juu ya imani ya waumini kuhusu Kiyama. Wakanushaji hao wa haki wanauchukulia ulimwengu wa baada kifo kuwa ni jambo la khurafa, uzushi na ngano za kale ambazo kwa mawazo yao hata Mitume waliotangulia walikuwa wakizizungumzia lakini wengi wa watu wa zama zao walikuwa hawazikubali. Katika kukanusha kwao kujiri kwa Kiyama, makafiri hawana hoja wala burhani yoyote ya kuthibitishia madai yao isipokuwa kuhoji tu kwa kusema iweje baada ya kufa, viungo vya mwanadamu vilivyosagika na kutawanyika huku na kule viweze kukusanywa tena pamoja na kumfanya yeye awe hai tena? Bila ya shaka yoyote ni kwamba kama tutataka kulipima na kuliweka kwenye mizani ya elimu na uwezo wa mwanadamu suala la Kiyama na kuwa hai tena kiumbe huyo katika ulimwengu wa akhera hilo litaonekana ni jambo lisilowezekana, lakini kwa Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, ambaye ni Muumba wa mwanadamu na mjuzi kamili wa kila kiungo na kila chembe ya ujudi wa kiumbe huyo, kazi hiyo ni sahali na nyepesi mno. Na ndiyo maana sehemu ya mwisho ya aya hizi inawataka watu wote watafakari na kutaamali juu ya mfumo wa ulimwengu wa maumbile ili waweze kuitambua na kuielewa vizuri zaidi elimu isiyo na ukomo na uwezo mutlaki wa Allah SW. Lakini kwa masikitiko ni kwamba akthari ya watu hawatumii akili zao katika kutafakari juu ya ulimwengu wa maumbile, bali wanawafuata kibubusa wazee wao waliowatangulia na kuendelea kukariri yale yale yaliyokuwa yakisemwa na wazee wao hao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba makafiri hawana hoja wala maneno yenye mantiki ya kukanusha maadi na kufufuliwa viumbe na wala hawako tayari kutumia akili zao na kuyatafakari maneno ya kimantiki ya Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa tuhuma za wapinzani kwa Mitume ni kudai kwamba maneno ya watukufu hao ni ngano ili kutaka watu wajiweke mbali nao.

Zifuatazo sasa ni aya za 84, 85, 86 na 87 ambazo zinasema:

قُل لِّمَنِ الأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

Sema: Ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?

سَيَقُولُونَ لِلَّهِ قُلْ أَفَلا تَذَكَّرُونَ

Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu! Sema: Basi, je, hamkumbuki?

قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ

Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi wa A'rshi Tukufu?

سَيَقُولُونَ لِلَّهِ قُلْ أَفَلا تَتَّقُونَ

Watasema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, hamwogopi?

Aya hizi zinawaelekezea masuali wakanushaji na kuzitaka akili na dhamiri zao zisimame katika nafasi ya hakimu mwadilifu wa kujibu masuali haya: Ni nani aliyeziinua na kuzitandaza mbingu hizi zenye adhama isiyo na kifani na kuuendesha ulimwengu huu usiojulikana mpaka wake? Bila ya shaka dhamiri za makafiri na washirikina hazitowaelekeza watu hao kutoa jibu jengine ghairi ya kulitaja jina la Allah SW. Na kama ni hivyo ndipo wanapoulizwa, inakuwaje basi mnatilia shaka qudra, nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu na kukuona kufufuliwa na kuumbwa tena mwanadamu katika ulimwengu wa akhera kuwa ni jambo la muhali? Kwa hakika mushkili wa watu wanaokanusha maadi na kufufuliwa viumbe chanzo chake hakihusiani na uelewa na utambuzi wao juu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, bali zaidi kinatokana na hawaa, matashi na matamanio yao ya nafsi. Wanachotaka wao ni kuweza kufanya lolote watakalo katika masuala yao ya binafsi na ya kijamii kulingana na matamanio ya nafsi zao pasina kuwekewa mipaka wala masharti yoyote, na hilo ni jambo linalokinzana na imani juu ya kufufuliwa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika kujadiliana na makafiri na wakanushaji wa haki tutumie yale wanayoyakiri na kuyakubali wao wenyewe kwa ajili ya kujengea hoja na kuthibitisha ukweli wa maneno yetu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kutambua adhama ya ulimwengu pamoja na Mola na Muumba wake kunapasa kuwe na taathira katika fikra, tabia na mwenendo wa mtu kwa kumfanya mtu mchaji Mungu na mwenye kumkumbuka daima Mola wake, vinginevyo utambuzi na uelewa huo hautokuwa na faida yoyote.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya za 88, 89 na 90 ambazo zinasema:

قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

Sema: Ni nani mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu, naye ndiye anayelinda, wala hakilindwi chochote kinyume naye, kama mnajua?

سَيَقُولُونَ لِلَّهِ قُلْ فَأَنَّى تُسْحَرُونَ

Watasema: (Ufalme huo) ni wa Mwenyezi Mungu. Sema: Basi vipi mnadanganyika?

بَلْ أَتَيْنَاهُم بِالْحَقِّ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ

Bali tumewaletea Haki, na kwa hakika wao ni waongo.

Aya hizi zinaendelea kuzungumzia yale yaliyoelezwa katika aya zilizotangulia kwa kuashiria mamlaka na utawala mutlaki wa Mwenyezi Mungu SW kwa ulimwengu wa maumbile na hitajio la viumbe vyote kwa mwongozo, auni na msaada wake Mola na kueleza kwamba kila dhamiri safi na akili timamu inakiri kwamba mfumo wa ulimwengu wa maumbile unaendeshwa kwa kufuata tadbiri moja ya Mola mmoja tu wa haki, na hakuna chochote kinachoweza kuathiri au kuathiriwa na kingine katika ulimwengu bila ya irada na kutaka Yeye Mola mwenye tadbiri hiyo. Viumbe vyote viko chini ya hifadhi yake Yeye, na Yeye hahitajii hifadhi ya yeyote, na hakuna mtu anayeweza kupata kimbilio lolote la kumlinda na kumhifadhi na ghadhabu zake Yeye Mola.

Kwa kuzingatia kuwa uchawi na mazingaombwe vinatumika kupindua ukweli na hakika ya jambo, Qur'ani tukufu inawahutubu wapinzani kwa kuwauliza: Kwani nyinyi mmerogwa mpaka haki mnaiona batili, na batili mnaiona kuwa ndio haki? Kama mnakubali kwamba ulimwengu uko chini ya mamlaka ya Mwenyezi Mungu kwa nini mnakuwa na shaka kiasi hiki juu ya akhera na mnakataa katakata kuikubali haki? Sisi tumeshakubainishieni nyinyi haki, vipi tena mnaikana na kudai kuwa ni uwongo? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kimbilio na mwenye kutoa hifadhi kwa waja ni Allah SW pekee, na ghairi yake Yeye hakuna hifadhi wala kimbilio lolote la kweli kwa watu katika ulimwengu huu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa yale yaliyokuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndio haki, lakini kughariki kwenye dimbwi la mambo ya umaada kunamfanya mwanadamu aione haki kuwa ni batili na kutokuwa tayari kuikubali. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 601 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na kutupa taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)