Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:14

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 75-80 (Darsa ya 600)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 600 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Darsa yetu hii inafunguliwa na aya ya 75 ambayo inasema:

وَلَوْ رَحِمْنَاهُمْ وَكَشَفْنَا مَا بِهِم مِّن ضُرٍّ لَّلَجُّوا فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ

Na lau tungeliwarehemu na tukawaondolea shida waliyonayo bila ya shaka wangeliendelea katika upotofu wao vile vile, wakitangatanga.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoashiria baadhi ya visingizio vya wapinzani wa Bwana Mtume na majibu yaliyotolewa dhidi ya visingizio hivyo. Aya hii tuliyosoma inasema: Kama Mwenyezi Mungu atawarehemu watu hao na kuwaondolea mazonge na mashaka waliyonayo, badala ya kumuelekea Yeye Mola na kutubia kwake kwa madhambi na makosa waliyofanya huko nyuma, wataendelea kushikilia na kufuata njia na mwenendo wao huo potofu na kuishia katika hali ya kutangatanga.

Kwa kawaida mtu ambaye amelala wapenzi wasikilizaji huwa unapomwita mara kadhaa tu basi huamka; lakini mtu anayejifanya amelala, hata kama utaamua kumtikisa pia hatoamka. Kwa sababu hiyo mtu ambaye yuko katika upotofu endapo atausikia wito wa haki anaweza kuongoka, lakini mtu ambaye anang'ang'ania kubakia katika dhalala na upotofu, huyo yeye hawezi kuongoka. Mtu kama huyo huwa kana kwamba yeye ni kiziwi wa kutoweza kusikia maneno ya haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba badala ya kuitumia kwa njia sahihi fursa waliyopewa na Allah, watu waliopatwa na mghafala wakatumbukia kwenye lindi la maasi huwa wanaitumia vibaya neema ya fursa hiyo kwa kuendelea kufanya madhambi na kumwasi Mola. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa hatima na mwisho wa uasi ni kuselelea kwenye hali ya kutangatanga.

Zifuatazo sasa ni aya za 76 na 77 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ أَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ فَمَا اسْتَكَانُوا لِرَبِّهِمْ وَمَا يَتَضَرَّعُونَ

Na hakika tuliwatia katika adhabu; lakini hawakuelekea kwa Mola wao Mlezi wala hawakunyenyekea.

حَتَّى إِذَا فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا ذَا عَذَابٍ شَدِيدٍ إِذَا هُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ

Mpaka tulipowafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata tamaa.

Ni kaida na utaratibu alioweka Allah SW kwamba ikiwa watu walioghafilika hawatozinduka kwa njia ya neema na rehma walizojaaliwa, huwa hakuna njia nyengine kwa maasi na madhmabi waliyofanya ila kufikwa na adhabu na kupatwa na masaibu papa hapa duniani. Pamoja na hayo tajiriba imeonyesha kuwa watu wabishi na wakaidi huwa hawako tayari kuzinduka na kunyenyekea kwa Mola na Muumba wao. Katika hali ya maumbile, wakati mwanadamu anapofikwa na mabalaa na kusibiwa na matukio machungu na ya kuhuzunisha huwa anarejea kwa Mola wake kwa vilio na kwikwi, akatubia madhambi aliyofanya huko nyuma na kwa moyo wa unyenyekevu akaomba msamaha na maghufira kwa Allah. Lakini wakati wingu zito la kibri na ukaidi linapotanda juu ya moyo wa mwanadamu, kiumbe huyo hufikia mahala hata anapokuwa ametingwa na kuelemewa na misukosuko na masaibu huwa hayuko tayari kumuelekea Mwenyezi Mungu na kuomba auni na msaada wake Mola.

Kutokana na nyoyo zao kuzongwa na kibri na uchafu wa maasi watu wenye sifa hiyo huselelea na kuendelea kubaki katika hali hiyo hadi mwisho wa uhai wao, lakini wakati watakapokabiliwa na adhabu kali Siku ya Kiyama hapo ndipo watakapoelewa kwamba wamebaki mikono mitupu bila ya kuwa na jema lolote na pasina kuwepo njia yoyote wala kitu chochote cha kuwaokoa. Lakini wakati huo tena watakuwa wamechelewa. Yatakayobakia hapo ni majuto, na majuto ni mjukuu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba makafiri waliokubuhu, wenye inadi na wakaidi hawaongoki kwa rehma na uraufu wa Allah wala hawazinduki kutoka kwenye usingizi wa mghafala kwa ghadhabu na adhabu ya Mola. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa adhabu za duniani ni aina ya adabu ya kimalezi ili kumfanya mtu atanabahi na kujitambua. Tab'an kama adabu hiyo haitokuwa na taathira ndipo hufuatiwa na adhabu ya Akhera.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 600 ya Qur'ani inahatimishwa na aya za 78, 79 na 80 ambazo zinasema:

وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالأَبْصَارَ وَالأَفْئِدَةَ قَلِيلا مَّا تَشْكُرُونَ

Na Yeye ndiye aliyekuumbieni usikizi na uoni na nyoyo za kufahamu. Ni kuchache mno kushukuru kwenu.

وَهُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ

Na Yeye ndiye aliyekuenezeni katika ardhi, na kwake Yeye mtakusanywa.

وَهُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ وَلَهُ اخْتِلافُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ أَفَلا تَعْقِلُونَ

Na Yeye ndiye anayehuisha na kufisha, na yake Yeye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?

Aya hizi zinataja neema mbalimbali za Mola kwa waja wake ili kuamsha hisia za ushukurivu ndani ya nafsi ya mwanadamu. Neema ambazo ziko katika nafsi ya mwanadamu mwenyewe na katika ulimwengu uliomzunguka ambazo kiumbe huyo anazielewa na haziwezi kukanushika. Bila ya shaka kati ya viungo vya mwanadamu, viungo vya hisi na utambuzi, yaani macho, masikio na akili vina nafasi maalumu na ya juu. Na ndio maana vimetajwa kwanza katika aya hizi tulizosoma kabla ya neema nyenginezo. Aya zinazofuatia zinaashiria uumbwaji na ukuaji wa mwanadamu katika sayari hii ya dunia, uwezo wa kufaidika na kuneemeka na fursa ya maelfu ya usiku na mchana katika dunia hii na kufikia tamati umri na uhai wa mwanadamu kwa kufikwa na mauti. Kisha aya zinamalizia kwa kueleza kwamba mwisho na marejeo ya wanadamu wote ni kwa Mwenyezi Mungu, Mola na Muumba wao.

Ni muhimu kuashiria pia hapa kuwa katika aya hizi haikutajwa neema ya ulimi, pamoja na kwamba ulimi ni miongoni mwa na neema na atiya kubwa za Allah kwa mja. Huenda sababu yake ni kwamba ikiwa mtu atakuwa hakujaaliwa kuwa na neema ya kusikia na hivyo akazaliwa akiwa kiziwi, kwa kuwa hawezi kusikia chochote hatoweza pia kujifunza kusema. Na ndio maana watu wote wanaozaliwa na uziwi hubakia maisha kuwa mabubu na wala huwa hawawezi kusema hata kama ndimi zao katika hali ya kiviungo huwa nzima bila ya kuwa na kasoro yoyote ya kimaumbile.

Jambo la kusikitisha ni kuwa licha ya kujaaliwa neema zote hizi, akthari ya watu ni watovu wa shukurani, na ni wachache miongoni mwao walio washukurivu kwa neema walizojaaliwa na Mola wao. Ndipo sehemu ya mwisho wa aya hizi ikamalizia kwa kutumia lugha ya kukemea na kusema: kwani hatukumpa mwanadamu nyenzo za utambuzi, basi kwa nini hazitumii kwa ajili ya kuelewa hakika za ulimwengu na kutafakari kuhusiana na nafsi yake na ulimwengu aliomo ndani yake?

Baadhi ya mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kwamba macho na masikio ni vitu walivyojaaliwa kwa pamoja wanadamu na wanyama na vinatumika kwa ajili ya kutambua vitu vya hisi, lakini akili ni maalumu kwa mwanadamu tu. Kwa hivyo mbali na vitu vya hisi, mwanadamu ana uwezo wa kuvitambua pia vitu visivyohisika. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mauti sio mwisho wa mwanadamu bali ni daraja la kumvukisha kiumbe huyo kuelekea kwenye ulimwengu wa juu zaidi ambako ndiko itakakothibiti ghaya na lengo kuu la kuumbwa mwanadamu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 600 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atakabalie dua zetu, atusamehe madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)