Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:07

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 70-74 (Darsa ya 599)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 599 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 70 ambayo inasema:

أَمْ يَقُولُونَ بِهِ جِنَّةٌ بَلْ جَاءَهُم بِالْحَقِّ وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ

Au wanasema: Ana wazimu? Bali amewajia na Haki, na wengi wao wanaichukia Haki.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia muamala mbaya wa wapinzani wa haki dhidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Aya hii tuliyosoma inataja tuhuma za uzushi za watu hao dhidi ya mtukufu huyo na kueleza kwamba kwa vile makafiri hawakuwa tayari kuikubali haki walikuwa hawazikubali aya za Qur'ani ambazo Allah SW alimteremshia Mtume wake na yeye kuwasomea watu kwamba ni wahyi utokao mbinguni bali walikuwa wakisema, yeye Nabii Muhammad SAW amesibiwa na umajununi na ndio unaomfanya aseme maneno hayo; au atakuwa na uhusiano na majini, na hivyo anachokifanya ni kuwasomea watu yale anayofikishiwa na majini hayo. Mwenyezi Mungu Mtukufu amezijibu shubha na tuhuma za watu hao kwa kusema: Tatizo linatokana na wao, ambao hawataki kuikubali haki, na si eti hawajabainikiwa kwa uwazi kwamba anayowaambia Mtume si ya kweli na si ya haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba miongoni mwa mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa kila mara na maadui wa dini ni kujaribu kuharibu na kuchafua shakhsia za viongozi wakuu wa dini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba wajibu na jukumu walilonalo viongozi wakuu wa dini ni kufikisha wito na ujumbe wa maneno ya haki hata kama akthari ya watu watachukizwa na maneno hayo au hawatokuwa tayari kuyakubali.

Ifuatayo sasa ni aya ya 71 ambayo inasema:

وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ

Na lau Haki ingelifuata matamanio yao, basi zingeliharibika mbingu na ardhi na waliomo ndani yake. Bali tumewaletea ukumbusho wao, nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao.

Aya hii wapenzi wasikilizaji inaendelea kuzungumzia yale yaliyokuja katika aya iliyopita ya 70 na kueleza kwamba sababu ya wapinzani wa haki kuipinga Qur'ani ni kwa kuwa kitabu hicho cha mbinguni hakiafikiani na hawaa na matamanio ya nafsi zao na matashi yao yasiyo na msingi, na laiti kama sheria zinazotawala ulimwengu wa maumbile zingefuata utashi wa wanadamu basi uharibifu, ufisadi na hali ya mchafukoge vingeugubika ulimwengu wote na wala kusingekuwepo na kipimo, kigezo wala mizani yoyote ya kupima na kupambanua baina ya lililo sahihi na la sawa na lisilokuwa la sawa. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba aya za Qur'ani Tukufu ni wenzo wa kuwazindua na kuwatoa watu katika usingizi wa mghafala na kuwafikisha kwenye uokovu, lakini kufuata hawaa na matamanio ya nafsi kunawafanya watu wazipe mgongo aya hizo za kitabu cha haki. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba watu wengi huwa wanapenda maamrisho ya dini yaafikiane na matashi na matakwa yao, hali ya kuwa dini inafuata haki, hakika na ukweli na si hawaa na matamanio ya nafsi ya watu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa mfumo unaotawala ulimwengu wa maumbile umesimama juu ya haki na uadilifu, lakini wanachotarajia na wanachotaka watu ni ulimwengu kuendeshwa kulingana na vile zinavyotamani nafsi zao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 72 ambayo inasema:

أَمْ تَسْأَلُهُمْ خَرْجًا فَخَرَاجُ رَبِّكَ خَيْرٌ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ

Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako Mlezi ni bora, na Yeye ndiye Mbora wa wanaoruzuku.

Aya hii inaendelea kuzungumzia maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizopita na kueleza kwa kuhoji, hivi hawa wapinzani wanakaidi na hawako tayari kuifuata haki,  kwani wewe Mtume umewaomba wao malipo na ujira kwa sababu ya kutangaza dini na kuwafikisha wao wito wa Tauhidi wa kuwataka wamwabudu Mola mmoja wa haki? Kisha aya inaendelea kwa kukana kisingizio hicho na kueleza kwamba ni wazi kuwa Mitume wanapata thawabu na malipo kwa Allah SW kutokana na kazi hiyo ya tablighi na ya kuutangaza wito wa haki, na wala hawatarajii chochote kile kutoka kwa watu. Baadhi ya nukta za mafunzo katika aya hii ni kwamba wafanya tablighi ya dini hawatakiwi kudai pesa wala malipo yoyote kwa watu kwa sababu ya kazi hiyo. Kama watu wenyewe watawapa kitu kama hidaya, hilo ni suala jengine. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa riziki za waja wote ziko kwa Allah SW. Mwenyezi Mungu amewadhaminia riziki yao watu wanaofanya tablighi ya kufikisha wito na ujumbe wa haki.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 599 inahatimishwa na aya za 73 na 74 ambazo zinasema:

وَإِنَّكَ لَتَدْعُوهُمْ إِلَى صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ

Na kwa yakini wewe unawaita kwenye Njia Iliyo Nyooka.

وَإِنَّ الَّذِينَ لا يُؤْمِنُونَ بِالآخِرَةِ عَنِ الصِّرَاطِ لَنَاكِبُونَ

Na hakika wale wasioiamini Akhera wanajitenga na Njia hiyo.

Katika sehemu hii ya mwisho ya aya hizi Mwenyezi Mungu SW anamuhutubu Mtume wake kwa kumwambia: Mwenendo usio sahihi na maneno yasiyo na msingi ya wapinzani yasikudhoofishe wala kukuvunja moyo katika kutekeleza jukumu lako, na wala kukanusha na kukataa kwao kusikufanye ukaingiwa na shaka juu ya njia ya haki unayoifuata. Elewa kwamba njia yako wewe ni haki na wito wako kwa watu ni wa kuwalingania kufuata njia sahihi na iliyonyooka. Tatizo linatokana na hao wanaokufuru na wanaokanusha maadi na kufufuliwa ambao wameacha kufuata akili, fitra na maumbile yao na kwa sababu hiyo hawatoweza kurejea kwenye njia ya Mola wako iliyonyooka. Kwa mujibu wa hadithi, sira na sunna za Mtume wa Allah na Maimamu maasumu wa kizazi cha mtukufu huyo ndio njia ya maisha iliyonyooka. Na kwa hivyo mtu yeyote mwenye kuikengeuka njia hiyo atakuwa ametoka nje ya mstari wa njia ya haki na kutumbukia kwenye upotofu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba njia ambayo Mitume waliwaonyesha watu ndio njia ya karibu zaidi na ya uhakika zaidi ya kuifikia saada. Na sababu ni kwamba njia iliyonyooka ndio njia ya mkato na ya karibu zaidi ya kuunganisha baina ya nukta mbili, lakini njia nyenginezo zimejaa mizunguko na kwa hivyo haziwezi asilani kumfikisha mtu kwenye nukta ya ghaya na makusudio. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 599 ya Qur'ani Tukufu imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwafikishe kufuata haki na atuwezeshe kujiepusha na batili.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)