Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 17:02

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 63-69 (Darsa ya 598)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 598 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 63 ambayo inasema:

بَلْ قُلُوبُهُمْ فِي غَمْرَةٍ مِّنْ هَذَا وَلَهُمْ أَعْمَالٌ مِن دُونِ ذَلِكَ هُمْ لَهَا عَامِلُونَ

Lakini nyoyo zao zimeghafilika na hayo, na wanavyo vitendo vinginevyo wanavyovifanya.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoelezea sifa za waumini na makafiri. Aya hii ya 63 inazungumzia sifa nyengine ya makafiri na kueleza kwamba watu wenye uchu wa dunia na wanaopaparikia vitu vya kimaada hughariki na kuzama kwenye mambo hayo mpaka kufikia hadi ya kughafilika na kusahau chanzo na asili yao na maadi na marejeo yao kwa Mola wao. Wao si wenye kudhihirisha uja wao kwa kumwabudu Mola aliyewaumba wala si wenye kufikria juu ya ulimwengu wa baada ya kifo. Ni wazi kwamba amali na matendo ya watu kama hao yatakuwa tofauti kabisa na mwenendo na matendo ya watu waumini, kwani hao huwa hawana soni wala hawaoni haya kufanya maasi na maovu. Bali si hasha hata wakawa wanajifakharisha na kujisifu kwa matendo yao maovu wanayofanya na kuyahisi kuwa ni alama ya ustaarabu na maendeleo! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kughafilika na kuielewa haki na ukweli humfanya mtu apotoke katika fikra na matendo yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kukitihirisha na kudumu katika kufanya matendo maovu huigeuza hulka ya mtu na kumfanya mateka na mtumwa wa amali na matendo hayo maovu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 64 na 65 ambazo zinasema:

حَتَّى إِذَا أَخَذْنَا مُتْرَفِيهِم بِالْعَذَابِ إِذَا هُمْ يَجْأَرُونَ

Mpaka tutakapowatia katika adhabu wale waliodekezwa kwa starehe kati yao, hapo ndipo watapoyayatika.

لا تَجْأَرُوا الْيَوْمَ إِنَّكُم مِّنَّا لا تُنصَرُونَ

Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.

Mghafala na kujisahau kwa makafiri kutaendelea tu kama hautofika wakati wa watu hao kuamshwa na kuzinduliwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Lakini wakati wanapofikwa na adhabu ya Allah inayowachanganya makafiri wote, watu hao ambao walikuwa wamelewa neema na raha za dunia huanza kulalama na kunung'unika kwa sababu ya kupoteza mali na utajiri na raha za maisha walizokuwa nazo. Lakini kulalama kwao huko hakutokuwa na tija wala faida yoyote, kwani wakati huo hakutokuwepo na fursa ya mara ya pili ya kurudi tena hapa duniani. Hakuna kitu chochote wala mtu yeyote atakayekuwa na uwezo wa kusimama na kuwasaidia kukabiliana na adhabu ya Allah, na wala wao hawatokhafifishiwa wala kupunguziwa adhabu hiyo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba huwa ni kazi ngumu zaidi na yenye mushkili zaidi kwa mtu kuuvua moyo wake na mapenzi ya dunia  baada ya kuikumbatia na kupaparikia raha na starehe zake. Aya hii inatuelimisha pia kwamba adhabu ya Allah inatolewa kwa msingi wa haki na uadilifu, kwa hivyo watu waovu wasiwe na matarajio ya kupata auni na msaada wa Mola.

Zifuatazo sasa ni aya za 66 na 67 ambazo zinasema:

قَدْ كَانَتْ آيَاتِي تُتْلَى عَلَيْكُمْ فَكُنتُمْ عَلَى أَعْقَابِكُمْ تَنكِصُونَ

Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa, nanyi mkirudi nyuma kwa visigino vyenu,

مُسْتَكْبِرِينَ بِهِ سَامِرًا تَهْجُرُونَ

Na huku mkitakabari na usiku mkiizungumza (Qur'ani) kwa dharau.

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaashiria chimbuko la kufru na ukanushaji uliofanywa na makafiri wa Kikureishi na kueleza kwamba watu hao hawakuwa makafiri kwa sababu ya ujinga na kutojua bali waliamua kuikana haki kwa utambuzi na uelewa. Na sababu ni kwamba wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipokuwa akiwasomea aya za Qur'ani waliamua kuzipa mgongo kutokana na ghururi na kutakabari kwao, na walipokuwa wakikutana katika majlisi na vikao vyao vya faragha walikuwa wakimvurumizia Bwana Mtume na maneno yake tuhuma za kila aina. Ni wazi kwamba mwisho wa vitendo vya watu wenye kutakabari na wenye inadi kama hao hauwi mwengine ila ni kupatwa na ghadhabu na adhabu ya Allah. Na hakika ni kwamba wao wanavuna yale yaliyopandwa na mikono yao wenyewe. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba moyo wa kiburi humfanya mtu asiwe tayari hata kuisikiliza haki seuze kuikubali na kuifuata. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa watu wanaoshindwa kukabiliana na wito wa Mitume kwa mantiki na hoja za wazi huishia kuropokwa na kuvurumiza maneno ya tuhuma na matusi.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya 598 inahitimishwa na aya za 68 na 69 ambazo zinasema:

أَفَلَمْ يَدَّبَّرُوا الْقَوْلَ أَمْ جَاءَهُم مَّا لَمْ يَأْتِ آبَاءَهُمُ الأَوَّلِينَ

Je, hawakuifikiri kauli, au yamewajia yasiyowafikia baba zao wa zamani?

أَمْ لَمْ يَعْرِفُوا رَسُولَهُمْ فَهُمْ لَهُ مُنكِرُونَ

Au hawakumjua Mtume wao, ndio maana wanamkataa?

Aya hizi zinaendelea kuzungumzia yale yaliyotajwa katika aya zilizotangulia kuhusu chanzo cha ukafiri na kutakabari na kueleza kwamba ukweli ni kuwa wapinzani wa Bwana Mtume SAW hawakuwa tayari kutadabari na kuyatafakari yale yaliyomo ndani ya kitabu hiki ambayo ni maneno ya Mwenyezi Mungu, vinginevyo wangeweza kutambua kwamba kitabu hiki ni sawa na vitabu walivyokuja navyo Mitume waliotangulia, na yametajwa ndani yake mambo yanayofanana na yale yaliyokuwemo kwenye vitabu vya Mitume hao. Wao ni watu wenye uelewa wa vitabu vya Taurati na Injili, na wanajua kwamba wito wa Tauhidi na kufanya matendo mema ni mambo yaliyotajwa ndani ya vitabu hivyo pia na wala si kitu kipya cha kudai kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW ndiye aliyekileta kwa mara ya kwanza. Isitoshe ni kuwa yeye Bwana Mtume ameishi umri wake wote na nyinyi watu wake, na nyote mnamtambua yeye kwa lakabu za "As Sadiq" yaani mkweli na "al Amin" yaani mwaminifu. Sasa kama nyinyi mnamjua yeye kwa sifa hizo inakuwaje tena mnaukadhibisha wito wake na kumtuhumu yeye kuwa ni mwongo? Baadhi ya mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hizi ni kwamba ikiwa Allah SW anawakemea makafiri kwamba kwa nini hawatadabari na kuyatafakari yaliyomo ndani ya Qur'ani, hali itakuwaje kwa waumini wasiotadabari juu ya yale yaliyomo ndani ya kitabu hicho kitukufu? Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wito wa Mitume wote una asili moja, kwa hivyo hakuna mantiki yoyote kwa mtu kushikilia kumfuata Mtume mmoja na kumkana yule anayefuatia baada yake. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah azisafishe nyoyo zetu na maradhi ya nafsi, yakiwemo ya kiburi na ghururi.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)