Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:58

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 57-62 (Darsa ya 597)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 597 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 57, 58 na 59 ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ هُم مِّنْ خَشْيَةِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ

Kwa hakika wale ambao kwa kumwogopa Mola wao Mlezi wananyenyekea,

وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ

Na wale ambao Ishara za Mola wao Mlezi wanaziamini,

وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لا يُشْرِكُونَ

Na wale ambao Mola wao Mlezi hawamshirikishi,

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia kundi la watu waliokuwa wakidhani kwamba kuwa na mali, watoto na neema za kimaada ni kielelezo cha kuwa na kheri, na kwa hivyo wakaelekeza hima na juhudi zao zote kwa ajili ya kuyapata mambo hayo. Amma aya hizi tulizosoma zinataja sifa za waumini ambao kwao wao maana ya kuwa na kheri ni kuweza kuwafanyia watu wema na ihsani na kuwafanya waja wa Allah wawe na ustawi na hali bora ya maisha. Sifa ya kwanza ya waumini wa kweli ni kuwa na khofu ndani ya nyoyo zao inayotokana na kuelewa adhama ya utukufu wa Mola Mwenyezi. Nao wanachunga na kuheshimu mipaka ya Yake Mola; hiyo ni khofu na haya inayotokana na utambuzi sahihi wa kumjua Mwenyezi Mungu unaowafanya waumini hao wasiwe tayari kumshirikisha Yeye Mola na yeyote yule au na kitu chochote kile bali wamwamini Yeye tu na kutii maamrisho yake Yeye tu. Khofu inayokusudiwa hapa si ile ya kawaida ya kuogopa watu au vitu vyenye hatari, bali ni khofu ya mtu anapochelea kufanya kitu au jambo lolote baya mbele ya wakubwa anaowaheshimu. Na je katika ulimwengu mzima yuko aliye mkubwa zaidi, wa kuheshimiwa zaidi na aliyetukuka zaidi ya Muumba wa ulimwengu huu? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba khofu inayomfanya mtu ajiepushe na mwenendo wa kuasi na kukhalifu amri za Mola na badala yake kufuata njia sahihi ni khofu chanya na nzuri na humjenga na kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa imani yenye thamani ni ile yenye ikhlasi na iliyokamilika, na si kwamba katika ibada za kiroho mtu awe mja wa Allah lakini katika masuala ya uchumi, siasa na mengine muhimu ya maisha awe mfuataji wa fikra na itikadi zisizotokana na uongofu utokao kwa Yeye Mola.

Ifuatayo sasa ni aya ya 60 na 61 ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَى رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ

Na wale ambao wanatoa walichopewa, na hali nyoyo zao zinaogopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi,

أُوْلَئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ

Basi wote hao ndio wanaokimbilia kwenye mambo ya kheri, na ndio watakaotangulia kuyafikia.

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaendelea kutaja baadhi ya sifa za kimatendo za waumini zilizoanza kuashiriwa katika aya zilizotangulia na kueleza kwamba, watu hao hushindana na kila mmoja wao kuwa na pupa na hamu ya kuwa wa mbele zaidi kuliko wenzake katika kufanya mambo ya kheri; hulihisi kuwa ni jukumu na wajibu wao kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na daima huwa na wasiwasi kwamba isije amali zao wakawa wamezifanya bila ya ikhlasi na hivyo kutokubaliwa na Mola. Wao ni watu ambao katu hawaingiwi na ghururi kwa mema wanayotenda, hawajihisi kwamba wana ustahiki wowote mbele ya Allah na wala hawana masimbulizi wala matarajio kwa mema wanayowafanyia watu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba watu wanaopenda dunia wanashindana katika kulimbikiza mali na utajiri, lakini wale wanaofadhilisha akhera, wao wanashindana katika kufanya mambo mema na kuwahudumia waja wa Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kushindana na kupigania kuwa wa mbele katika mambo ya kidunia ya kumwasi Mola ni sawa na kujipalia makaa ya moto, lakini kushindana na kupigania kuwa wa mbele kwa ikhlasi katika mambo ya akhera ni jambo la maana na lenye kutakiwa kwa kila muumini.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 597 inahatimishwa na aya ya 62 ambayo inasema:

وَلا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلاَّ وُسْعَهَا وَلَدَيْنَا كِتَابٌ يَنطِقُ بِالْحَقِّ وَهُمْ لا يُظْلَمُونَ

Na hatuikalifishi nafsi ila kwa kadri ya uwezo wake. Na tunacho kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa.

Katika aya zilizotangulia imeelezwa kuwa kushindana na kujitahidi kuwa wa mbele katika kufanya mambo mema na ya kheri ni moja ya sifa maalumu za waumini. Baada ya kuelezwa hayo aya hii tuliyosoma inasema, hapana shaka kuwa Allah SW hana matarajio ya kiwango sawa kwa waja wake wote kwa sababu amewaumba na hali tofauti. Na kwa hivyo kila mtu hakalifishwi ila kulingana na uwezo wake wa kimwili na kiakili. Anapaswa kulikubali jambo kulingana na uwezo wake wa ufahamu na katika utendaji pia afanye jambo kwa kadiri uwezo wake wa kimali na kimwili unavyomruhusu na si zaidi ya hivyo. Ni wazi kwamba uwezo, suhula na hali za watu katika jamii zinatafautiana. Na ni kwa sababu hiyo ndio maana Allah SW hakuwakalifisha na kuwawajibishia mambo waja wake wote kwa hali sawa. Yeye Allah SW ni Haki, yuko katika haki na kila analowakalifishia waja wake katika dunia hii limesimama juu ya msingi wa haki na uadilifu. Na huko akhera pia hisabu ya amali za waja zitafanywa kwa kuzingatia uwezo waliokuwa nao na suhula walizojaaliwa kuwa nazo hapa duniani. Kwa maana hiyo tajiri na masikini hawatowajibika kwa namna sawa mbele ya Allah kama ambavyo jukumu la alimu na mwanazuoni mbele yake Yeye Mola ni kubwa zaidi kuliko alivyo mtu mjinga na maamuma. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kipimo anachotumia Allah katika kutoa majukumu na wajibu wa kidini kwa waja wake pamoja na malipo ya thawabu na adhabu huko akhera ni kuzingatia uwezo wao wa mali, vipawa vyao vya akili na nguvu na uzima wao wa kimwili. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kufanya jambo lolote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hakuna kushindwa wala hakumletei mtu majuto, kwa sababu Yeye Mola hamkalifishi mja wake kufanya jambo zaidi ya uwezo wake na wala hamshurutishi kwamba lazima afikie lengo ili kumpa malipo ya thawabu. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waumini wa kweli ambao imani zao zinathibitishwa na matendo yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)