Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:54

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 52-56 (Darsa ya 596)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 596 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya aya 52 ambayo inasema:

وَإِنَّ هَذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ

Na hakika Umma wenu huu ni Umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi, basi nicheni Mimi.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyokuwa na agizo la Allah SW kwa Mitume na wafuasi wao kuwataka wafanye amali njema na kujiepusha na vitu vichafu na kula na kutumia vile vilivyo safi na vya halali tu. Baada ya aya hiyo, aya hii inawahutubu watu wote na kusema: Nyinyi nyote ni umma mmoja na ni wafuasi wa itikadi moja ambayo ni imani ya tauhidi ya Mola mmoja tu wa haki. Mitume wote wametumwa na Mola mmoja tu na wote hao waliwalingania watu wote tauhidi na kumcha Mwenyezi Mungu. Kutumwa Mitume mbalimbali hakumaanishi kuwepo waumbaji wawili au zaidi wa ulimwengu na viumbe vilivyomo ndani yake. Mafundisho ya Mitume wote yana lengo na kusudio moja. Wao ni mithili ya walimu wanaofundisha katika ngazi za msingi, ya kati na ya juu katika mfumo wa elimu ambao wote wanafanya kazi kwa lengo na muelekeo mmoja. Kiwango cha elimu wanachotoa na mitalaa ya masomo wanayopanga inategemea hali za wale wanaowapa elimu hiyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mola mmoja tu wa haki anawataka waja wake wote wawe wamoja, na wote kwa pamoja wafuate dini moja ya tauhidi, yaani kumwabudu Yeye Mola mmoja tu wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa usuli na misingi ya wito wa Mitume wote ilikuwa mimoja kama ambavyo wanadamu wote wana fitra na hali moja ya maumbile.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 53 na 54 ambazo zinasema:

فَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ زُبُرًا كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ

Lakini walilikataa jambo lao (hili la dini) baina yao sehemu mbali mbali. Kila kundi likafurahia kwa waliyonayo.

فَذَرْهُمْ فِي غَمْرَتِهِمْ حَتَّى حِينٍ

Basi waache katika upotevu wao kwa muda.

Aya iliyotangulia iliwalingania watu wote wito wa umoja. Aya hizi tulizosoma zinatahadharisha juu ya hitilafu na mifarakano na kueleza kwamba: kila kundi lilijitenga na wenzake kwa kisingizio cha kushikamana na mtume wao tu na kitabu alichokuja nacho ilhali mitume wote na vitabu walivyokuja navyo walitumwa na Mungu mmoja, na wito wao kwa watu ulikuwa ni kufuata dini moja na kumwabudu Mola mmoja tu wa haki. Lakini taasubi na ung'ang'anizi usio na sababu wa kushikilia watu fikra na itikadi zao pasina kuwa tayari kusikiliza mantiki na hoja za wengine ndio chanzo cha mifarakano iliyopo baina ya watu na chanzo cha kuwepo dini na nadharia mbalimbali zilizobuniwa na wanadamu. Ilhali akili na mantiki zinahukumu kuwa baada ya kuja mtume mpya na kuteremshwa kitabu kipya cha mbinguni wafuasi wa mtume aliyetangulia wamwamini mtume huyo na kuacha taasubi na ukaidi. Kwa hakika taasubi za aina hii za kidini zisizo na msingi hazitokani na mafundisho asili ya dini za mbinguni bali chimbuko lake ni ghururi na ubinafsi tu. Kisha sehemu inayofuatia ya aya inamhutubu Bwana Mtume SAW kwa kumwambia, kwa vile hivi sasa wapinzani wako hawako tayari kuiamini na kuifuata haki, na badala yake wanang'ang'ania na kushikilia imani na itikadi zao, wewe waache kama walivyo waendelee kubaki kwenye ujahili, mghafala na upotofu wao mpaka ima wafikie mahala waache mwenendo wao huo au uwadie muda wao wa kufikwa na mauti. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mifarakano baina ya wafuasi wa dini na dini, na kuwa katika matapo na madhehebu mbalimbali Wayahudi, Wakristo na Waislamu sivyo walivyotaka iwe Mitume wakubwa na wateule wa Allah Musa, Issa na Muhammad (AW). Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mfungamano wa kichama na kimatapo unapasa ujengeke juu ya msingi sahihi wa kiakili na kidini na si kwa kufuata hawaa za nafsi na mapenzi na chuki zinazotokana na sababu za binafsi.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 596 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 55 na 56 ambazo zinasema:

أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ

Je! Wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyowapa mali na watoto,

نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ بَل لّا يَشْعُرُونَ

Ndio tunawahimizia kheri? Lakini wenyewe hawatambui.

Aya hizi zinaashiria moja nyengine kati ya ufahamu usio sahihi ulioenea baina ya watu na kueleza kwamba baadhi ya watu wanadhani kwamba ikiwa makafiri wanaishi maisha mazuri na wana kila suhula za kimaada basi hiyo ni ishara ya kuridhiwa na kurehemewa na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amewateremshia watu hao neema za kimaada katika maisha na kuwafungulia milango ya kheri na baraka zake, kama ambavyo Qur'ani inasimulia kuhusu Qaruni kwamba watu walikuwa wakiziangalia kwa jicho la uchu mali na utajiri wake na hata wakawa wanatamani Mwenyezi Mungu angewapa na wao mali na utajiri kama huo.

Hali ya kuwa kwanza ni kwamba: Mwenyezi Mungu hatafautishi kati ya muumini na kafiri katika kutoa suhula na neema za kimaada na za kidunia, bali kila mwenye kufanya jitihada humkunjulia neema hizo. Pili, mali na utajiri ni njia ya kutahiniwa watu wote, waumini na makafiri, na kwa nafsi yake mali si kipimo na kigezo cha kuonyesha kuwa aliyejaaliwa ni mtu anayeridhiwa na kurehemewa na Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo ya kuzingatia katika aya hizi ni kwamba tusiingiwe na ghururi na majivuno kwa sababu ya mali na watoto kwani si chochote kati ya hivyo vinavyomdhaminia mtu nusura na uokovu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa tujiepushe na kufanya tathmini ya kijujuu na isiyo sahihi juu ya maisha ya makafiri, kwani haifai kuzichukulia neema za ustawi wa kimaada walizonazo kuwa ni kipimo cha kufuzu na saada. Wasikilizaji wapenzi, darsa ya 596 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azijaalie neema za kidunia alizotupa ziwe sababu ya sisi kuwa washukurivu kwake na si chanzo cha kutakabari na kumkufuru Yeye Mola.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)