Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:52

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 47-51 (Darsa ya 595)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 595 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 47, 48 na 49 ambazo zinasema:

فَقَالُوا أَنُؤْمِنُ لِبَشَرَيْنِ مِثْلِنَا وَقَوْمُهُمَا لَنَا عَابِدُونَ

Wakasema: Je, tuwaamini watu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?

فَكَذَّبُوهُمَا فَكَانُوا مِنَ الْمُهْلَكِينَ

Basi wakawakadhibisha, wakawa miongoni mwa walioangamizwa.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ

Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa Mwenyezi Mungu alimtuma Nabii Musa AS na nduguye Haroun wamwendee Firauni na wakuu wa kasri lake ili kuwafikishia wito wa haki wa tauhidi, lakini mataghuti hao walitakabari na kuikataa haki. Baada ya hayo, aya tulizosoma zinaashiria tabia ya kujikweza na kujitukuza aliyokuwa nayo Firauni na watu wake ambao walisema: Musa na Haroun ni watu kama sisi tu; isitoshe, watu wote wa kaumu yao, yaani Bani Israil ni watumwa kwetu sisi. Kwa hivyo si Musa wala Haroun aliye na ubora juu yetu na wala kaumu yao si ya kulinganisha na yetu. Na kwa hivyo vipi wanatarajia sisi maashrafu na wakubwa wa kaumu yetu tuyakubali maneno yao na kuwatii wao?

Ni ajbu, kwamba Firauni na watu wake wa karibu walikuwa wakiwatuhumu Mitume hao wa Mwenyezi Mungu kuwa ni watu wapenda jaha na kujikweza hali ya kuwa wao kina Firauni walikuwa wakiwaona watu wa kaumu ya Bani Israil kuwa ni watumwa na wajakazi wao na walikuwa wakiwanyongesha na kuwatumikisha watu hao wa tabaka la wanyonge kwa namna ya kutisha na ya kusikitisha mno.

Kwa hivyo hatima na mwisho wa uasi na kutakabari huko ulikuwa ni kuangamizwa Firauni na watu wake kwa kugharikishwa kwenye Mto Nile, tukio ambalo liliwaokoa na kuwakomboa Bani Israil na madhila ya Firauni. Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria kuteremshwa Taurati kwa Nabii Musa AS ambayo Allah SW aliiteremsha ili iwe kitabu cha mwongozo wa uongofu kwa Bani Israil ili wajiepushe na kujiweka mbali na mwenendo potofu wa Mafirauni na kushikamana na njia iliyoonyoka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mfumo wa Kifirauni hoja na mantiki huwa hazina thamani yoyote; nafasi na hadhi za kijamii za watu ndivyo vipimo vya kuainisha thamani na itibari ya maneno yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa waisitikbari na madhalimu wanaoyanyongesha mataifa na kuyafunga minyororo ya dhulma na uonevu, iko siku watatiwa mkononi tu na Allah na mwishowe  wataangamizwa.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 50 ambayo inasema:

وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَى رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ

Na tukamfanya mwana wa Mariamu na mama yake kuwa ni Ishara, na tukawapa kimbilio kwenda mahali palipoinuka penye utulivu na chemchem za maji.

Baada ya Nabii Musa AS, Nabii Issa AS ndiye Mtume mwengine mkubwa aliyebaathiwa na kutumwa kwa Bani Israil ambaye ujudi wake ulikuwa ishara na muujiza wa Allah kwa Bani Israil. Sababu ni kwamba mama yake Nabii Isa, yaani bibi Maryam AS ambaye alikuwa mja mteule kwa utakasifu na usafi wa maadili, katika hali ambayo alikuwa hana mume, kwa irada ya Allah SW na kupitia malaika Jibril alijaaliwa kupata uja uzito na kumzaa Nabii Isa Masih AS. Mwana huyo alikuwa moja ya ishara ya qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, kwa sababu bibi Maryam aliweza kupata ujauzito pasina kuguswa na mwanamume yeyote na hivyo kumzaa Nabii Isa pasina kuwa na baba. Baadhi ya nukta za mazingatio katika aya hii ni kwamba Nabii Isa AS ni mwana wa Maryam na si mwana wa Mungu; na ni alama ya uwezo wa Mwenyezi Mungu na si Mungu mwenyewe. Nukta nyengine ya mafunzo tunayopata katika aya hii ni kwamba Mwenyezi Mungu aliwalinda Nabii Isa na mama yake na shari za maadui na kuwaweka mahali pa amani, utulivu na penye baraka nyingi.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 595 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 51 ambayo inasema:

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ

Enyi Mitume! Kuleni katika vitu vizuri na tendeni mema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa mnayoyatenda.

Baada ya aya 50 za sura hii ya al Muuminun ambazo ndani yake yamezungumziwa kwa muhtasari mambo yaliyojiri katika maisha ya Mitume mbalimbali aya hii ya 51 inasema: kinyume na walivyokuwa wakisema wapinzani wa haki kwamba kwa nini Mitume wako sawa na watu wengine, Mwenyezi Mungu amewafanya Mitume watokane na wanadamu, na wao kama walivyo wanadamu wengine wanahitajia kula na kunywa. Lakini wakati huohuo wamepambanuka na kutafautiana na watu wengine katika vitu viwili. Cha kwanza ni kwamba wao wanajiepusha na kujiweka mbali na vilaji na vinywaji haramu ambavyo vinaifanya nafsi ya mtu iwe na hulka ya kinyama na kihayawani na kitu cha pili ni kwamba nishati inayopatikana kutokana na vyakula hivyo wanaitumia kwa ajili ya mambo ya kheri na yenye faida tu. Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa wanaichukulia riziki ya chakula kuwa ni wenzo wa kuutumia kwa ajili ya ukamilifu wa kiutu. Na ndiyo maana walikuwa wakitumia vyakula safi na vya halali tu, wakati ambapo kwa watu ambao kula na kunywa ndio ghaya na lengo kuu la maisha yao ya kimaada hapa duniani, huwa hawajali wala hawauzingatii msingi huo bali wanachojali wao ni kupata vile vinavyokidhi na kuridhisha matashi yao ya kihayawani tu, kiwe kitu hicho ni kizuri au kibaya. Katika aya nyengine za Qur'ani Tukufu baada ya kutajwa amri ya kula, yaani kuluu yamefuatia maamrisho mengine, hali inayoonyesha kuwa kula na kunywa sio ghaya na lengo kuu bali ni wenzo wa kuutumia kwa ajili ya kumjenga mtu na kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu. Mifano ya aya hizo ni kama zile zisemazo: Na kuleni, na kunyweni na wala msifanye israfu; Kuleni katika riziki ya Mwenyezi Mungu, na mumshukuru; Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mitume wa Allah waliweza kufikia daraja za juu za ukamilifu na umaanawi kwa kutumia atiya hizi hizi za maisha ya kimaada. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mawalii wa Mwenyezi Mungu hawakuwa wakijifanya watawa na watu wa kuzihini nafsi zao, bali walikuwa wakizitumia neema za kimaada na za kimaumbile na kuishi maisha ya kawaida. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba sharti la kupata taufiki ya kufanya amali njema ni mtu kula chakula cha halali. Riziki ya haramu humzuia mtu kufanya amali njema. Wapenzi wasikilizaji darsa yetu ya Qur'ani kwa leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah aturuzuku riziki ya halali hata kama ni chache na atuepushe na riziki ya haramu hata kama ni nyingi.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)