Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:47

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 38-46 (Darsa ya 594)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 594 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 38, 39 na 40 ambazo zinasema:

إِنْ هُوَ إِلاَّ رَجُلٌ افْتَرَى عَلَى اللَّهِ كَذِبًا وَمَا نَحْنُ لَهُ بِمُؤْمِنِينَ

Huyu si lolote ila ni mtu anayemzulia Mwenyezi Mungu uwongo, wala sisi wenye kumuamini.

قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ

Akasema: Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa wanavyonikanusha.

قَالَ عَمَّا قَلِيلٍ لَيُصْبِحُنَّ نَادِمِينَ

(Mwenyezi Mungu) akasema: Baada ya muda mchache hakika watakuwa wenye kujuta.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia habari za kaumu ya Thamudi waliomkadhibisha mtume wao Nabii Saleh AS kwa kisingizio cha kuwa ni mwanadamu tu kama wao na kwa hivyo hawakuwa tayari kumwamini na kumfuata. Aya tulizosoma zinaendelea kuzungumzia maudhui hiyo kwa kusema: watu hao walijenga hoja ya kutetea na kuhalalisha ukafiri wao kwa kudai kwamba, kama yeye, yaani mtume wao, angekuwa ametumwa na Mwenyezi Mungu tungelimwamini, lakini anasema uwongo kujitambulisha kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na ni kwa sababu hiyo ndio maana sisi hatuko tayari kumwamini.

Kwa maneno yao hayo ni kana kwamba watu hao walikuwa wakitaka kusema kwamba sisi tunamkubali Mwenyezi Mungu, lakini mtu huyu hatumtambui kuwa ni Mtume na mjumbe wake. Yaani walichotarajia wao, Mwenyezi Mungu awatume malaika kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Kutokana na kufikia hatua hiyo, Mtume huyo wa Allah aliyekabiliwa na ukaidi, inadi na ukadhibishaji wa wapinzani hao wa haki alimuelekea Mola na kumwomba nusra na msaada wake, na Allah SW akaliitikia ombi lake kwa kumwahidi kwamba karibuni hivi makafiri hao watapata malipo ya adhabu ya ukafiri na ukadhibishaji wao itakayowafanya wajute kwa mwenendo wao huo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya wakati makafiri na wapinzani wa haki hujionyesha na kujitangaza kuwa wao ni watetezi na wachungaji wa mipaka ya Mwenyezi Mungu na kuwadunisha na kuwakadhibisha mawalii wa Allah. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa ni jambo zuri na lenye faida kwa mtu kujuta kwa matendo maovu aliyotenda huko nyuma, lakini kuja kujuta pale anapoiona adhabu ya Mwenyezi Mungu iko mbele ya macho yake, majuto ya wakati huo ya mtu hayatokuwa na tija wala faida yoyote kwake.

Zifuatazo sasa ni aya za 41, 42 na 43 ambazo zinasema:

فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ بِالْحَقِّ فَجَعَلْنَاهُمْ غُثَاءً فَبُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

Basi ukawanyakua ukelele kwa haki, na tukawafanya kama takataka zinazoelea juu ya maji. Ikapotelea mbali kaumu ya madhaalimu!

ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قُرُونًا آخَرِينَ

Kisha tukaleta baada yao vizazi vingine.

مَا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ

Hapana umma uwezao kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.

Hatima ya watu wa kaumu ya Thamudi ilikuwa ni kupigwa na umeme uliotoka mbinguni na kushukiwa na mvua kali ya gharika iliyoambatana na mafuriko ya kutisha ambayo yaliusomba mji na majumba yao na kuwaangamiza wao wenyewe pia. Hilaki na maangamizi ndio hatima inayowangoja madhalimu wote. Kisha aya zinazofuatia zinaeleza kwamba baada ya hapo Mwenyezi Mungu alizileta kaumu nyengine chungu nzima katika pembe tofauti za dunia. Lakini kama ambavyo kila mwanadamu mmoja mmoja anaishi na kufa, kaumu na umma mbalimbali nazo pia zinapitia vipindi vya uhai na mauti, na kila kaumu inayoasi na kutenda dhulma mwishowe itahilikishwa na kutoweka. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba utaratibu wa utoaji malipo ya adhabu na thawabu wa Mola umesimama juu ya msingi wa uadilifu. Allah SW haiadhibu kaumu au umma wowote ule wa watu ila pale wanapostahiki kushukiwa na adhabu kutokana na matendo yao. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa matukio ya historia yanafuata kaida na utaratibu thabiti na usiobadilika aliouweka Allah. Kwa mujibu wa utaratibu huo kaumu za watu madhalimu huangamizwa na umma nyengine mpya huletwa kuchukua nafasi yao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 44 ambayo inasema:

ثُمَّ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا تَتْرَا كُلَّ مَا جَاءَ أُمَّةً رَّسُولُهَا كَذَّبُوهُ فَأَتْبَعْنَا بَعْضَهُم بَعْضًا وَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ فَبُعْدًا لِّقَوْمٍ لّا يُؤْمِنُونَ

Kisha tukawatuma Mitume wetu, mmoja baada ya mmoja. Kila umma alipowafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatanisha hawa baada ya hawa, na tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Ikapotelea mbali kaumu isiyoamini.

Mwenyezi Mungu SW ametuma Mitume wengi sana katika zama zote za historia, manabii ambao kutokana na huruma na kuwatakia kheri watu wao walifanya kazi kubwa na ngumu ya kuwalingania wito wa haki wa tauhidi, lakini baadhi ya watu wa kaumu zao, kwa sababu ya kulinda maslahi yao ya kimaada, na baadhi ya wengine kutokana na kufadhilisha raha, starehe na anasa hawakuwa tayari kuikubali haki na kufuata wito wenye mantiki wadhiha na ya wazi kabisa wa Mitume wao. Watu hao walitoa vitisho vya namna mbalimbali, wakawadunisha na kuwakadhibisha wajumbe hao wa Allah na hata baadhi yao wakawaua. Tab'an wakati uasi na ukafiri wa watu hao ulipokitithiri na kupindukia mpaka Mwenyezi Mungu alikuwa akitoa amri ya kuangamizwa kaumu za watu hao na kufutwa katika kumbukumbu za historia. Na kwa hivyo kilichosalia baada yao ilikuwa ni athari za majina ya tamaduni na staarabu zao tu ili viwe ni ibra na mazingatio kwa watakaofuatia baada yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kila umma ulipelekewa Mtume ili Mwenyezi Mungu asiwe na dhima tena kwa waja, na wao watu pia wasiwe na udhuru tena wa kutoa kwake Yeye Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kila umma unaopatwa na apizo na laana ya Mwenyezi Mungu huhilikishwa na kuangamizwa na hakuna kinachosalia ghairi ya kumbukumbu ya jina lao.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 594 ya Qur'ani inahatimishwa na aya za 45 na 46 ambazo zinasema:

ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَى وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ

Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, pamoja na ishara zetu na hoja zilizo wazi.

إِلَى فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا عَالِينَ

Kwenda kwa Firauni na wakuu wake. Lakini walijivuna, nao walikuwa ni kaumu waliojikweza.

Baada ya ayaa kadhaa zilizotangulia za sura yetu hii kuzungumzia hatima ilizozipata kaumu za Nuhu na Thamudi na baadhi ya kaumu nyenginezo, aya hizi tulizosoma zinaashiria harakati ya Nabii Musa AS ya kupambana na Firauni na kueleza kwamba Mwenyezi Mungu alimtuma Musa AS na nduguye Haroun waende kwenye kasri la Firauni. Akiwa na miujiza aliyopewa na Mola, na vilevile hoja za wazi na mantiki, Nabii Musa alimlingania Firauni pamoja na wakuu wa kaumu yake wito wa tauhidi, lakini kutokana na nguvu za madaraka na utajiri wa mali waliokuwa nao, watu hao walikuwa wakijiona wabora na watukufu kuliko Bani Israil na kwa hivyo walitakabari na hawakukubali katu kuiamini na kuifuata haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba watawala madhalimu ndio chanzo za kufisidika na kupotoka umma za watu. Kwa sababu hiyo kabla ya kuwalingania watu wa Misri, Nabii Musa AS alitakiwa kwanza amwendee na kumfikishia wito wa tauhidi Firauni na watu wake wa karibu kwa sababu jamii hairekebishiki pasina kurekebishwa na kuwekwa sawa kwanza viongozi wa jamii hiyo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa mantiki na hoja ni vitu vyenye nafasi muhimu na ya msingi katika kufanya tablighi ya dini na kuwalingania watu wito wa haki. Vilevile aya hizi zinatufunza kuwa katika kufanya tablighi, baadhi ya wakati huwepo ulazima wa kuifanya kazi hiyo watu kwa pamoja na mtu kupata msaada kutoka kwa wenzake. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Mola atuwafikishe kufanya yanayomridhisha na atuepushe na yale yanayomghadhibisha.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)