Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:44

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 31-37 (Darsa ya 593)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 593 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 31 na 32 ambazo zinasema:

ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ

Kisha baada yao tukaanzisha kizazi kingine.

فَأَرْسَلْنَا فِيهِمْ رَسُولا مِنْهُمْ أَنِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَهٍ غَيْرُهُ أَفَلا تَتَّقُونَ

Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu! Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Je, hamwogopi?

Katika darsa mbili zilizopita tulizungumzia hatima iliyowapata watu wa kaumu ya Nabii Nuh (AS) na jinsi makafiri wa kaumu hiyo walivyoangamizwa. Aya tulizosoma zinaashiria habari za watu wa kaumu ya Thamudi ambao Mtume aliyetumwa kwao alikuwa ni Nabii Saleh AS. Yeye pia kama walivyokuwa Mitume wengine wa kabla yake aliwalingania watu tauhidi, yaani kumwabudu Mola mmoja tu wa haki na kuwatahadharisha na shirki, yaani kumwamudu mola mwengine ghairi ya Allah SW. Kwa sababu ukafiri na shirki unafuta athari ya hofu na taqwa ndani ya moyo wa mtu na kufungua njia kwa mtu kufanya maovu na madhambi mbalimbali; kinyume na kumwamini Mwenyezi Mungu na kuhofu adhabu yake Mola ambayo humzuia mtu kufanya machafu na maovu mengi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba utaratibu aliouweka Mwenyezi Mungu SW ni kuwapa mwongozo na maonyo watu kwa njia ya kuwapelekea Mitume. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa Mitume walikuwa wanadamu na walitokana na jamii za watu wao wenyewe ili wawe ruwaza na mfano wa kivitendo wa kuweza kuigwa na kufuatwa na watu wa jamii hizo na vilevile iweze kuondoka dhima na visingizio vya watu.

Zifuatazo sasa ni aya za 33 na 34 ambazo zinasema:

وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِلِقَاء الآخِرَةِ وَأَتْرَفْنَاهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا مَا هَذَا إِلاَّ بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يَأْكُلُ مِمَّا تَأْكُلُونَ مِنْهُ وَيَشْرَبُ مِمَّا تَشْرَبُونَ

Na wakubwa katika watu wake waliokufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera, na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binaadamu kama nyinyi; anakula mlacho, na anakunywa mnywacho.

وَلَئِنْ أَطَعْتُم بَشَرًا مِثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ

Na nyinyi mkimt'ii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa khasarani.

Badala ya kuukubali wito wenye mantiki wadhiha na ya wazi kabisa wa Mitume ambao uliwataka kufuata njia ya haki na kufanya amali na matendo mema, watu waliojilimbikizia mali na utajiri na wale wakubwa na maashrafu wa kaumu za Mitume hao waliupinga na kuukadhibisha wito huo kwa sababu waliuona unapingana na kukinzana na mwenendo wao na maslahi yao na wakahisi kwamba ikiwa watu watawaamini na kuwafuata Mitume hadhi na nafasi yao wao katika jamii itashuka na kudhoofika. Hoja ya kwanza ya kuutia ila na kasoro wito wa Mitume iliyotolewa na watu hao ni kwamba hawa Mitume ni watu kama sisi na wala hawatafautiani chochote na sisi. Kama Mwenyezi Mungu anataka kutufikishia uongofu itapasa atuletee viumbe wa juu zaidi yetu sisi kama malaika ndio tutakaoweza kuyakubali maneno yao. Hawa Mitume ambao ni watu wanaoishi kama tulivyo sisi, wanaokula, kunywa na kuvaa mavazi kama tuvaayo sisi, vipi wanaweza kutupa muongozo wa maisha? Walichotarajia na walichokuwa wakitaka wakubwa hao wa kaumu hizo ni kwamba watu wayakubali maneno yao wao na wala wasiwapinge, lakini kuyakubali watu hao maneno ya mtu ambaye ni msafi wa maneno na matendo, hilo halikubaliki na ni kitu chenye madhara kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wito wa tauhidi wa kumwabudu Mola mmoja tu wa haki huandaa mazingira ya kuwakomboa watu na kuwatoa kwenye minyororo ya kunyongeshwa na maashrafu na watawala madhalimu. Kwa sababu hiyo makundi mawili hayo ndio yaliyokuwa wapinzani wakubwa zaidi wa Mitume kuliko matabaka mengine ya jamii. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kutii na kufuata maneno ya watu wengine kama yatakuwa yamesimama juu ya msingi wa hoja na mantiki, sio tu si jambo baya bali husaidia kumjenga mwanadamu kuelekea kwenye ukamilifu wa kiutu. Na ukweli hasa ni kwamba mfumo wa elimu na malezi umejengeka juu ya msingi huo.

Aya za 35, 36 na 37 za sura yetu ya al Muuminun ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

أَيَعِدُكُمْ أَنَّكُمْ إِذَا مِتُّمْ وَكُنتُمْ تُرَابًا وَعِظَامًا أَنَّكُم مُّخْرَجُونَ

Hivyo anakuahidini ati ya kwamba mtakapokufa na mkawa udongo na mifupa kuwa mtatolewa?

هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ لِمَا تُوعَدُونَ

Hayawi! Hayawi hayo mnayoahidiwa.

إِنْ هِيَ إِلاَّ حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ

Hapana ila uhai wetu wa duniani tu, tunakufa na kuishi basi. Wala sisi hatutafufuliwa.

Awamu na marhala ya kwanza ya wito wa Mitume ilikuwa ni kuwataka watu wajiepushe na shirki na kuikubali tauhidi; kisha baada ya hapo kwa wale waliokuwa wameikubali tauhidi, yaani Laa ilaha illa Allah walikuwa wakibainishiwa suala la Kiyama na kurejea wanadamu kwenye ulimwengu wa akhera.  Lakini wapinzani wa Manabii hao, badala ya kujadili suala la tauhidi na shirki wakakurupuka na kudakia suala la maadi, yaani kufufuliwa viumbe na kutaka kuonyesha kuwa hilo ni jambo muhali na lisiloingia akilini ili kwa njia hiyo kuwazuia watu wasiwafuate Mitume. Hali ya kuwa kulikubali suala la Kiyama kunafuata baada ya kuikubali tauhidi, na kwa mtazamo wa kiakili pia hakuna hoja ya kulipinga na kulikana jambo hilo, japokuwa kwa wale wanaotosheka na kutegemea njia za hisi tu na za tajiriba katika kukubali mambo, kwao wao kujiri kwa Kiyama si jambo linaloingia akilini kirahisi. Kwa watu matajiri wenye ukwasi wa mali, na maashrafu ambao nyoyo zao zimetekwa na maisha ya raha na ya uhuru wa kufanya watakalo na kuzistarehesha nafsi zao kwa raha na anasa za kimaada, wao wanajua kwamba hawatopata nafasi yoyote kwenye Pepo iliyoahidiwa na kubashiriwa na Mitume na ndio maana wanajaribu kulifanya suala la maadi lionekane kuwa ni kitu kilicho mbali kuweza kutokea na kulitolea hoja hewa hii na ile ya kulipinga na kulikadhibisha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mungu aliyemuumba mwanadamu mara ya kwanza kutokana na udongo vipi atashindwa kumfufua na kumpa uhai tena mwanadamu huyo kwa sababu tu ya kugeuka udongo? Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuyawekea kikomo maisha ya mwanadamu kuwa mwisho wake ni hapa duniani ni kumdunisha kiumbe huyo kufikia hadi ya mnyama, kwa sababu wanyama ndio ambao mwisho wa maisha yao ni papa hapa duniani. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 593 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Mola azifanye imara imani zetu, atutakabalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)