Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:41

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 25-30 (Darsa ya 592)

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 25-30 (Darsa ya 592)Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 592 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya za 25 na 26 ambazo zinasema:

إِنْ هُوَ إِلاَّ رَجُلٌ بِهِ جِنَّةٌ فَتَرَبَّصُوا بِهِ حَتَّى حِينٍ

Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi mngojeeni tu kwa muda.

قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ

Akasema (Nuhu): Mola wangu Mlezi! Ninusuru kwa kuwa wamenikadhibisha.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizonukuu maneno machafu ya tuhuma yaliyotolewa na makafiri wa kaumu ya Nabii Nuh AS dhidi ya mtume huyo mteule. Aya tulizosoma zinaendelea kuzungumzia maudhui hiyo na kueleza kwamba watu hao hawakutosheka na tuhuma zao hizo walizotoa bali walikwenda mbali zaidi kwa kumwita Nabii Nuh majununi na mwendawazimu apayukaye maneno yasiyo na uhusiano wowote. Na kwa hivyo njia pekee ni kumpuuza na kumwacha kama alivyo aseme mpaka achoke mwishowe ataacha maneno yake hayo.

Madai ya uwendawazimu ni miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zikitolewa na wapinzani wa Mitume ambao walijaribu kutumia silaha hiyo ili kuwafanya watu wajiweke mbali na waja hao wateule wa Allah na kuwafanya watu waliotengwa katika jamii. Tab'an baadhi ya wakati, maadui hao wa wito wa mbinguni walikuwa wakifanikiwa katika mbinu chafu yao hiyo. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba Nabii Nuh AS alimwomba Mwenyezi Mungu ampe auni na msaada wa kukabiliana na watu hao wakaidi ambao hawakuwa tayari kuikubali haki kwa mantiki yoyote ile. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba waabudu masanamu na washirikina ambao wayafanyayo wao hayakubaliki kiakili na kimantiki, huwa wanawaona wale wanaomwambudu Mungu mmoja wa haki pamoja na Mitume kuwa ni majununi na wendawazimu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa katika kuzikabili tuhuma za makafiri, waumini wanatakiwa watawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuomba msaada kwake, kwa sababu Yeye yuko juu ya nguvu zote.

Ifuatayo sasa ni aya ya 27 ambayo inasema:

فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ فَاسْلُكْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلاَّ مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ مِنْهُمْ وَلا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ

Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi wetu! Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipokuwa yule ambaye katika wao kauli imekwishatangulia juu yake. Wala usinitajie hao waliodhulumu. Kwani hao bila ya shaka watagharikishwa.

Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Nabii Nuh AS alitumia muda wa miaka 950 kufanya kazi ya kuwalingania watu wake kalimatu tauhiid yaani Lailaha illa Allah lakini ni wachache tu miongoni mwao ambao walimwamini, na akthari yao walimkadhibisha na kumfanyia shere na stihzai Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. Hatimaye hali ikafikia marhala ambapo Allah SW alimpa habari Mtume wake kwamba hakuna mtu mwengine yeyote atakayekuamini, na hata watoto wa kaumu hii pia watakuwa watu makafiri. Ilipofikia hatua hiyo Nabii Nuh akamwomba Mwenyezi Mungu ateremshe adhabu yake kwa watu hao, na Mwenyezi Mungu akaitakabalia dua hiyo ya Mtume wake. Tufani kali na ya kutisha ilitokea ambayo iliwaangamiza makafiri na kuisafisha ardhi kwa kusomba athari zao zote pasina kusaza wala kubakisha chochote. Lakini ili kuwaokoa hao waumini wachache walioikubali haki pamoja na kizazi cha wanyama, Mwenyezi Mungu alimwamuru Mtume wake Nuh AS aunde jahazi kubwa ili pale itakapotoka amri yake Mola ya kuchimbuka maji kutoka ardhini na kumiminika mengine kutokea mawinguni awapakie jahazini humo dume moja na jike moja la kila mnyama, kisha wafuatie waumini na hatimaye familia yake mwenyewe isipokuwa mkewe pamoja na mmoja wa wanawe ambao kutokana na kushirikiana na kuwa kitu kimoja na makafiri, wao hawakuwa na haki ya kuabiri ndani ya safina hiyo ya uokovu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ikiwa tutafanya mambo yetu ya kidunia na masuala yetu ya kimaisha kulingana na mafundisho ya Wahyi na kwa kufuata maamrisho ya Allah tujue kwamba tutafanikiwa tu. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa mwanadamu ana mas-ulia juu ya wanyama na wala asikiache kizazi cha viumbe hao kikatoweka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kwamba mfungamano wa kidini una uzito zaidi na unautangulia mfungamano wa damu na wa kifamilia. Ikiwa wake na watoto wa Mitume watakuwa watu waovu hawatokuwa na mfungamano wowote wa kidini na manabii hao, na hivyo hawatosalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Wa aidha aya hii inatufunza kuwa kama Allah SW atataka, basi maji, ambayo ni asili ya maisha na uhai yatageuka kuwa kisababishi cha hilaki na maangamizi kwa madhalimu.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 592 ya Qur'ani inahatimishwa na aya za 28, 29 na 30 za sura yetu ya Al Muuminun ambazo zinasema:

فَإِذَا اسْتَوَيْتَ أَنتَ وَمَن مَّعَكَ عَلَى الْفُلْكِ فَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي نَجَّانَا مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

Basi utakapotulia wewe na walio pamoja nawe humo marikebuni, sema: Alhamdulillahi Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, aliyetuokoa na watu madhaalimu!

وَقُل رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ

Na sema: Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye baraka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji.

إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَاتٍ وَإِن كُنَّا لَمُبْتَلِينَ

Hakika katika hayo kuna ishara na kwa yakini Sisi ni wenye kuwafanyia (waja wetu) mtihani.

Katika aya hizi tulizosoma Mwenyezi Mungu Mtukufu anampa bishara Nabii Nuh AS ya kwamba baada ya jahazi kuwa tayari, na itakapotokea tufani ya gharika, makafiri wote wataangamizwa. Kwa hivyo waumini wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaokoa na shari ya madhalimu, kwani kama si rehma na nusra yake Mola waumini wasingeweza katu kusalimika na shari ya madhalimu hao. Kisha aya zinaendelea kuashiria moja ya kaida na utaratibu usiobadilika na usio na shaka wa Allah kwa kueleza kwamba adhabu hiyo haihusiani na makafiri wa kaumu zilizopita tu, bali Yeye Mola huwa anawatahini kila mara waja wake na kuwapa madhalimu jaza ya adhabu kwa sababu ya yale waliyoyatenda. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tunatakiwa tutawakali kwa Mwenyezi Mungu na pia tufanye juhudi na kutafuta njia ya kujiokoa na shari ya madhalimu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Qur'ani si kitabu cha kujielimisha na masuala ya historia. Habari za kaumu zilizotangulia zimetajwa ndani ya kitabu hicho cha mbinguni ili watu wapate funzo, ibra na mazingatio kutokana na yale yaliyozisibu kaumu hizo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kaida na utaratibu wa Allah ni kuwatahini watu katika kila zama na mahala. Kuitambua haki na batili, na kuifuata haki na kujiweka mbali na batili ndio njia ya kumwezesha mtu afuzu mtihani wa Mola. Kwa haya machache basi tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atupe mema hapa duniani, na akatupe mema huko    Akhera na atulinde na adhabu ya moto.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)