Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:33

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 19-24 (Darsa ya 591)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 591 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 na 20 ambazo zinasema:

فَأَنشَأْنَا لَكُم بِهِ جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ لَّكُمْ فِيهَا فَوَاكِهُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ

Basi kwa maji hayo tukakufanyieni bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula;

وَشَجَرَةً تَخْرُجُ مِن طُورِ سَيْنَاءَ تَنبُتُ بِالدُّهْنِ وَصِبْغٍ لِّلْآكِلِينَ

Na mti utokao katika Mlima Sinai, unatoa mafuta na kitoweo kwa walaji.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoashiria kuteremka kwa mvua kutoka mawinguni na kuhifadhiwa maji hayo kwenye matabaka ya hifadhi yake chini ya ardhi na kulielezea suala hilo kuwa ni moja ya neema kwa ajili ya uhai wa viumbe. Baada ya hayo aya tulizosoma zinasema konde, mabustani pamoja na anuai za miti na mimea inayoota katika maeneo mbalimbali ya ardhi inastawi kwa maji ya mvua anayoteremsha Mwenyezi Mungu; na matunda yanayopatikana kutokana na miti na mimea hiyo ndiyo yanayokidhi mahitaji ya chakula ya wamiliki wake na pia mauzo yake matunda hayo yanawapatia pato kubwa la fedha. Ni kama ilivyo mathalani mizaituni ambayo inalimwa zaidi katika maeneo ya Sham na Palestina; kama tujuavyo mizaituni ni chanzo kikuu cha mafuta kwa ajili ya kupikia na vilevile yanatumika kama sehemu ya kiungo cha chakula kwa saladi, mboga na kachumbari. Wapenzi wasikilizaji, kuyapa umuhimu wa kuyazungumzia matunda kama tende, zabibu na zaituni kunakofanywa na Qur'ani kati ya anuai za matunda mengine aliyoyaumba Allah SW kunaonyesha umuhimu wa matunda hayo katika kukidhi mahitaji ya kimwili ya mwanadamu. Nukta ya kuvutia ni kwamba baada ya utafiti wao, leo hii wataalamu wa masuala ya lishe nao pia wamefikia natija kwamba matunda matatu haya yana umuhimu mkubwa sana wa kinga na tiba ya maradhi mengi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba maji ndiyo chanzo cha uhai wa mimea, wanyama na watu. Mwenyezi Mungu amekifanya chanzo hiki muhimu cha uhai kipatikane kupitia mzunguko wa maji katika mfumo wa maumbile na hatimaye kuteremka kutoka mawinguni kwa njia ya mvua. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumba wa mwanadamu amemhakikishia kiumbe huyo kupata mahitaji yake ya chakula kutoka kwenye mfumo na njia za maumbile. Hivyo kuzipuuza neema hizi na kwenda kutafuta vilaji na vinywaji visivyo vya halali ni kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya za 21 na 22 ambazo zinasema:

وَإِنَّ لَكُمْ فِي الأَنْعَامِ لَعِبْرَةً نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهَا وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ

Na hakika mnayo mazingatio makubwa katika nyama hoa - tunakunywesheni katika vile vilivyomo matumboni mwao, na mnapata katika hao manufaa mengi, na katika hao mnawala.

وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ

Na juu yao na juu ya marikebu mnabebwa.

Katika kuendelea kutaja neema za Mwenyezi Mungu aya hizi tulizosoma zinaashiria mchango wa wanyama hoa yaani wa miguu minne katika kudhamini mahitaji ya maisha ya mwanadamu na kueleza kwamba katika njia iliyopo baina ya damu na uchafu wa ndani ya matumbo ya wanyama kama ng'ombe na kondoo, Mwenyezi Mungu SW anakutoleeni maziwa safi kabisa ambayo hayana chembe ya rangi ya damu wala uvundo wa harufu mbaya. Ni kinywaji kitamu na murua kabisa ambacho chenyewe kama kilivyo ni chakula, na yanatumika pia kutengeneza vyakula vingine mbalimbali kama mtindi, jibini, siagi, malai na anuai nyenginezo za bidhaa za maziwa. Kutokana na ngozi, sufu na manyoya yao wanyama mnatengeneza aina mbalimbali za nguo na mavazi; nyama yao mnaitumia kupika na kutayarisha anuai za vyakula na mnaitumia migongo yao kama vipando vitulivu na maridhia kwa ajili yenu wenyewe na mizigo yenu. Mnafaidika nao wanyama kwa kiwango ambacho takribani hakuna sehemu yoyote ya kiwiliwili cha mnyama kama ng'ombe na kondoo ambacho ni kitu cha ziada, ila hutumika kwa namna moja au nyengine katika maisha ya mwanadamu. Ikiwa meli, marikebu na majahazi makubwa na madogo yanatumika kubeba na kupeleka mizigo na abiria huku na kule baharini, farasi, ngamia na punda vimekuwa ndio vipando vya mwanadamu katika nchi kavu; na hata katika dunia ya leo iliyoendelea pia vipando hivyo havijapoteza nafasi yao hiyo hususan katika maeneo ya mashambani na ya vijijini au ya milimani yaliyo magumu kupitika. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tusikuchukulie kuwepo kwa wanyama kuwa ni kitu cha kawaida tu. Kwani kama tutakaa na kutafakari kwa makini juu ya mchango wao katika maisha ya wanadamu, hilo lenyewe ni somo la kumjua Mwenyezi Mungu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa safari za kubeba na kupeleka bidhaa au wasafiri huku na kule ni miongoni mwa mahitaji ya lazima ya mwanadamu hapa ardhini, na Yeye Mola mwingi wa rehma amemwandalia kiumbe huyo nyenzo na suhula anazohitajia kwa kazi hiyo nchi kavu na baharini.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 591 ya Qur'ani inahatimishwa na aya za 23 na 24 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَى قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَهٍ غَيْرُهُ أَفَلا تَتَّقُونَ

Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je! Hamwogopi?

فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا هَذَا إِلاَّ بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُرِيدُ أَن يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ وَلَوْ شَاء اللَّهُ لَأَنزَلَ مَلائِكَةً مَّا سَمِعْنَا بِهَذَا فِي آبَائِنَا الأَوَّلِينَ

Wakasema wale wakuu waliokufuru katika watu wake: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipa ubora juu yenu. Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda basi yakini angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa baba zetu wa kwanza.

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha alama za adhama na qudra ya Mwenyezi Mungu katika mfumo wa ulimwengu wa maumbile, aya hizi zinaashiria uraufu na wema wa Mola Muumba na Mlezi kwa waja wake wa kuwaelekeza kwenye uongofu, na kugusia kisa cha wito wa Mtume wa kwanza kati ya Mitume Ulul-azm, yaani Nabii Nuh AS. Mtume huyo mteule hakuwalingania watu wa kaumu yake kitu kingine ghairi ya kuwataka waache kuabudu masanamu na badala yake wamwabudu Mungu mmoja tu wa haki. Lakini watu waliokuwa na madaraka na utajiri ambao walihisi kuwa wito huo wa Nabii Nuh utasababisha wao kupoteza hadhi na nafasi zao walianzisha propaganda za uwongo za kudai kwamba Nuh AS ni mtu mpenda mamlaka na jaha ambaye dhamira yake ni kuwahodhi watu na kuwafanya watumwa na vibaraka wake; na wakadai kwamba nabii huyo hana nia ya kuiletea jamii yao saada na uongofu. Watu hao wakawa wanasema kwamba, kama Mwenyezi Mungu angekuwa anataka kuwaongoa watu angetuma malaika ambao wamejitenga na kujiepusha na mambo yote ya kidunia na kimaada wakafanya kazi hiyo ya kuwabainishia watu maneno ya Mwenyezi Mungu. Hali ya kuwa utaratibu wa Mwenyezi Mungu ni kuwafikishia wanadamu wito wa uongofu kupitia mwanadamu mwenzao na si malaika, kwa sababu ufikishaji uongofu haufanyiki kwa tablighi tu na maneno matupu bali mfikishaji mwenyewe wa uongofu anapaswa awe ruwaza na mfano wa kuigwa katika jamii kwa tabia na matendo yake ili watu waweze kuyakubali na kuyafuata maneno yake. Lakini kwa kuwa malaika hawatokani na jinsia ya wanadamu hawawezi kuwa mfano wa kivitendo wa kuigwa na kufuatwa na wanadamu hao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume walikuwa wakiwalingania na kuwataka watu wamwabudu Mwenyezi Mungu na kumwelekea Yeye Mola na si kuwaelekea wao walinganiaji. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa wapinzani wa Mitume walikuwa maashrafu, mabwanyenye, matajiri na watu wenye mamlaka na madaraka ambao walitaka waendelee kudumisha nguvu na satua zao hizo kwa watu. Kwa haya machache wapenzi wasikilizaji tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Mola atuonyeshe haki na kutupa taufiki ya kuifuata, na atuonyeshe batili na kutuwezesha kuiepuka.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)