Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 25 Februari 2014 16:30

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 15-18 (Darsa ya 590)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 590 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 15 na ya 16 ambazo zinasema:

ثُمَّ إِنَّكُمْ بَعْدَ ذَلِكَ لَمَيِّتُونَ

Kisha hakika nyinyi baada ya hayo mtakufa.

ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ

Kisha hakika nyinyi Siku ya Kiyama mtafufuliwa.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizobainisha awamu unazopitia uumbwaji wa mwanadamu. Baada ya kuelezwa hayo, aya tulizosoma zinasema, kumalizika kwa awamu hizo kunahatimisha umri na uhai wenu hapa duniani, na kwa kufikwa na mauti mtaondoka katika ulimwengu huu wa dunia kuelekea ulimwengu mwengine wa akhera, na huko mtarudishiwa tena uhai wenu na kuanza maisha mengine ya milele. Katika aya zilizotangulia iliashiriwa pia awamu ya kuumbwa kwa roho, roho ambayo haitoweki kwa sababu ya mauti ambayo ni kiunganishi tu cha kati ya maisha ya duniani na ya akhera ya kila mwanadamu. Mauti ni hakika isiyo na shaka wapenzi wasikilizaji, na wala hayawezi kuepukika kwa kadiri kwamba Imam Ali (AS) amesema:" Kama kuna watu ambao wangeweza kufikiria njia ya kufanya ili kuyaepuka mauti na kuweza kubakia milele duniani basi watu hao wangekuwa ni Mitume wa Mwenyezi Mungu, lakini hata wao pia waliondoka duniani kutokana na mauti, na hakuna mtu yeyote atakayebaki hapa duniani". Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mauti maana yake si mwisho wa uhai bali ni awamu moja kati ya awamu za maisha ya mwanadamu ya kumhamishia kwenye ulimwengu wa akhera. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kwa mtazamo wa kidini maisha ya mwanadamu hayamalizikii kwenye maisha ya kimaada ya hapa duniani, na watu waumini wanaitakidi kuwepo maisha ya kimaanawi yatakayodhihiri kwa tukio la Kiyama.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 17 ambayo inasema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعَ طَرَائِقَ وَمَا كُنَّا عَنِ الْخَلْقِ غَافِلِينَ

Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye kughafilika na viumbe.

Aya zilizotangulia zimegusia alama za uumbaji wa Allah SW katika nafsi ya mwanadamu, alama na ishara ambazo kiistilahi zinajulikana kama "Aayaatul anfus". Aya hii ya 17 imeashiria ishara za qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu Mola Muumba katika ulimwengu huu mpana ambazo kiistilahi zinajulikana kama "Aayaatul aafaaq". Badala ya kutumia neno mbingu saba yaani "Sab-a Samawat", aya hii imezungumzia njia saba yaani "Sab-a Taraaiq" ambayo inavyoonyesha muradi na makusudio yake ni zile njia zinazopita nyota angani ambazo idadi yake ni kubwa mno. Na kutumika hapa idadi ya saba ni ishara ya kuonyesha wingi wa vitu. Kisha aya inaendelea kwa kusema: Isidhaniwe kwamba wingi, anuai na mtawanyiko wa viumbe mbinguni na ardhini utamfanya muumbaji wake aghafilike na uendeshaji wa masuala ya viumbe hivyo na kukiacha kila kimoja kama kilivyo. Kutokana na aya hii tunajifunza haya yafuatayo: Mosi, muumba wa mwanadamu, mbingu na ardhi ni mmoja, na ulimwengu wote wa viumbe unaendeshwa kwa tadbiri na irada moja. Na pili ni kwamba Mwenyezi Mungu, Yeye ni Muumba na vilevile ni Mwangalizi na hakuna chochote kinachoweza kutoka nje ya mamlaka ya ujuzi na elimu yake mutlaki.

Darsa ya 590 inahatimishwa na aya ya 18 ambayo inasema:

وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاء مَاء بِقَدَرٍ فَأَسْكَنَّاهُ فِي الأَرْضِ وَإِنَّا عَلَى ذَهَابٍ بِهِ لَقَادِرُونَ

Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza katika ardhi. Na hakika Sisi ni wenye uwezo wa kuyaondoa.

Aya hii wapenzi wasikilizaji inaashiria uteremkaji na unyeshaji wa mvua ikiwa ni moja ya neema kubwa za Mola na kueleza kwamba maji yanayohitajika katika maeneo mbalimbali ya ardhi yanapatikana kupitia unyeshaji wa mvua. Maji hayo hufyonzwa na kuzama ardhini na kuhifadhiwa kwenye matabaka ya chini ya ardhi yanayohifadhi maji kwa muda wa kipindi chote cha mwaka ili kuweza kutumiwa na wanadamu kwa ajili ya kunywa, kilimo na matumizi mengineyo.

Ni wazi kwamba Mungu ambaye ametumia tadbiri muhimu kama hiyo kwa ajili ya kudhamini na kukidhi mahitaji muhimu zaidi ya wanadamu, mimea na wanyama ni mweza wa kuiondoa hali hiyo na kuwafuta viumbe vyote katika uso wa ardhi. Na bila ya shaka hakuna mtu yeyote mwenye nguvu na uwezo wa kuzuia lile atakalo Allah au kuweza kuleta mbadala wa njia hii aliyoiweka Yeye Mola kwa ajili ya ufikishaji maji kwa viumbe. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kwa tadbiri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, maji, ambayo ndio chanzo cha maisha kwa ajili ya viumbe vyote vyenye uhai akiwemo mwanadamu yanamiminika kutokea mawinguni na kutawanyika kwenye sehemu mbalimbali za ardhi ili yaweze kunufaisha viumbe vyote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa thamani ya neema za Mwenyezi Mungu huwa tunaielewa pale inapotuondokea hata kwa muda mfupi tu. Ni kama pale mvua zinapopungua kunyesha ukazuka ukame na njaa ambapo mwanadamu huemewa na kutokuwa na uwezo wa kufanya lolote. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 590 imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa neema zake, tunazozijua na tusizozijua.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)