Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 24 Februari 2014 11:45

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 8-14 (Darsa ya 589)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 589 ambayo kwa sasa inatoa tarjumi na maelezo ya sura ya 23 ya Al Muuminun. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 8 na ya 9 ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ

Na ambao wanachunga amana zao na ahadi zao,

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ

Na ambao wanazihifadhi Sala zao.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizotaja baadhi ya sifa za waumini. Aya hizi za 8 na 9 tulizosoma hivi punde zimetaja sifa nyingine za watu hao na kueleza kwamba waumini ni watu wenye muamana kwa amana wanazopewa. Wanachunga amana za Mola na vilevile amana wanazopewa na watu. Inapasa kuashiria hapa kuwa Kitabu cha Allah cha Qur'ani, Suna za Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bayt wake AS ni amana kubwa na nzito. Kuchunga amana hizo kunawezekana kwa mtu kutekeleza wajibu na majukumu ya kidini. Kwa mujibu wa hadithi, katika suala la kuchunga amana za watu hakuna tofauti baina ya muumini na kafiri, bali amana aliyopewa mtu anapaswa kuirejesha kwa mwenyewe, awe mwenye amana hiyo ni mtu mwema au mbaya, na iwe amana hiyo ya kitu cha thamani au kisicho na thamani. Sifa za kuwa na muamana wa kuchunga amana na kuwa mkweli na mwaminifu zina umuhimu kwa kiasi ambacho Maimamu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume SAW wameusia kwa kusema, msipime uzuri na ubaya wa watu kwa kusali, kufunga na kuhiji kwao bali wapimeni kwa ukweli na uaminifu wao.

Kutimiza miadi na ahadi za ndani ya familia na kuheshimu mikataba na makubaliano ya kijamii ni sifa nyengine ya waumini wa kweli. Suala la kuchunga ahadi, mikataba na makubaliano, nalo pia kama lilivyo suala la amana haliwahusu waumini tu, na kwa hivyo muumini hawezi kuchukua hatua ya upande mmoja ya kukiuka na kuvunja makubaliano na mkataba aliofungiana na makafiri.

Baada ya kutaja sifa muhimu kadhaa za waumini, mwisho Qur'ani Tukufu imeiashiria tena Sala ambayo ndiyo sifa kuu kati ya hizo ambapo mara hii imetilia mkazo juu ya kuihifadhi na kuchunga hukumu na nyakati zake. Ni kitu chenye kutoa mguso hapa kuona kwamba sifa za waumini zimeanza kwa suala la khushuu na unyenyekevu ndani ya Sala na kuhitimishwa na kuichunga na kuihifadhi nguzo hiyo ya dini. Hii inadhihirisha nafasi kuu ya Sala katika kumlea na kumjenga mtu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kukubali majukumu na kuchunga na kutekeleza hukumu za dini na makubaliano ya kijamii ni miongoni mwa alama za mtu muumini. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kuchunga hukumu na maamrisho ya dini na kuwa makini katika utekelezaji wake humjenga na kumuinua mtu kiimani na kumkurubisha kwa Allah SW.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 10 na 11 ambazo zinasema:

أُوْلَئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ

Hao ndio warithi,

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

Ambao watairithi Pepo ya Firdausi, wadumu humo.

Aya hizi wapenzi wasikilizaji zinaeleza kuwa hatima ya waumini wa kweli ni Pepo ya milele ya Allah na ambayo itarithiwa na watu hao tu. Nukta yenye kutoa mguso katika aya hizi ni kutumika neno urithi na kukaririwa mara mbili katika aya hizi. Huenda sababu yake ni kwamba japokuwa malipo na thawabu anazolipa Allah SW zinatokana na amali za waja lakini malipo hayo ya Pepo ni makubwa na yasiyoweza kuelezeka adhama yake kulinganisha na amali tu za mtu; kwa sababu hiyo yatakuwa mithili ya mali ya urithi ambayo huipata mtu bila ya kuisumbukia wala kuihangaikia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba mali za mwanadamu zinabaki kuwa urithi kwa ajili ya watu wengine hapa duniani, lakini amali zake anazofanya hapa duniani ni urithi atakaokwenda kuupata yeye mwenyewe huko Akhera. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa Pepo ni zawadi ya milele kwa waumini ambayo haina mabadiliko wala uchakavu wowote ndani yake.

Aya za 12, 13 na 14 ndizo zinazotuhatimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الإِنسَانَ مِن سُلالَةٍ مِّن طِينٍ

Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo.

ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ

Kisha tukamjaalia awe tone la mbegu ya uzazi katika makao yaliyohifadhika.

ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ فَتَبَارَكَ اللَّهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ

Kisha tukaumba tone kuwa pande la damu, na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa, na mifupa tukaivika nyama. Kisha tukamfanya kiumbe mwengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa waumbaji.

Baada ya aya zilizopita kutaja sifa kadhaa za waumini aya hizi za 12, 13 na 14 za Suratul Muuminun zinamuelewesha mwanadamu jinsi alivyoumbwa kwa kumfahamisha awamu mbalimbali alizopitia akiwa ndani ya fuko la uzazi la mama. Aya zinasema asili ya mwanadamu ni maji na udongo, Naye Mola Muumba kwa qudra na uwezo wake amemjaalia kiumbe huyo kuwa na akili, kipawa na uwezo wote huu wa kumwezesha kufikia daraja za juu kabisa za ukamilifu wa kiutu. Tab'an Mwenyezi Mungu SW aliye Mweza, Mjuzi na Mwenye Hekima amekifanya kizazi cha mwanadamu kiendelee kubaki kupitia kanuni ya uchanganyikaji wa mbegu za uzazi za jinsia mbili za mume na mke ndani ya fuko la uzazi la mama, mbegu ambazo kwa muda wa miezi 9 zinapita kwenye vipindi vya mabadiliko ya kustaajabisha.

Miongoni mwa miujiza ya Qur'ani Tukufu ni kuzungumzia tangu miaka 1,400 nyuma kuhusu awamu za mabadiliko na ukuaji wa kiinitete ndani ya fuko la uzazi la mama, mtazamo ambao hauna mkinzano wala mgongano na ugunduzi wa kisayansi uliofanywa katika zama za sasa. Na hii ni katika hali ambayo katika zama za kuteremshwa Qur'ani hakukuwepo na njia yoyote ya umurikaji kuweza kuelewa yale yanayojiri ndani ya fuko la uzazi la mama. Ni katika karne za hivi karibuni tu na baada ya kuunda vifaa vya kisasa ndipo wanadamu wameweza kupiga picha ndani ya fuko hilo la uzazi na kuzishuhudia awamu za mabadiliko hayo.

Kisha sehemu ya mwisho ya aya ya 14 inaashiria awamu ambayo iko nje ya uoni na ushuhudiaji wa macho ya mwanadamu, nayo ni awamu ya kupuliziwa roho ndani ya kiwiliwili cha mwanadamu, ambayo Qur'ani Tukufu imeielezea kwa ibara ya "uumbaji mwengine". Uumbaji ambao umemfanya mwanadamu kuwa kiumbe bora kulinganisha na viumbe wengine, na kwa sababu hiyo Allah SW amejitambulisha mwisho wa aya kuwa ni mbora wa waumbaji. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba tafakuri na mazingatio juu ya qudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika uumbaji wa mwanadamu kunamfanya muumini audiriki na kuuelewa barabara uwezo na hekima ya Mola Muumba na hivyo kuifanya imani yake iwe thabiti na imara zaidi. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kujitambua mtu nafsi yake ni utangulizi wa kumtambua Mola wake. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 589 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atutakabalie amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)