Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 24 Februari 2014 11:16

Sura ya Al-Muuminun, aya ya 1-7 (Darsa ya 588)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani, darsa inayotoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura za Qur'ani Tukufu kulingana na mpangilio wa sura hizo ndani ya Mas-haf. Hii ni darsa ya 588 ambayo itaanza kutoa tarjumi na maelezo ya sura ya 23 ya Al Muuminun. Kwa pamoja tuitegee sikio aya ya kwanza na ya pili za sura hii ambazo zinasema:

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ

Hakika wamefaulu Waumini,

الَّذِينَ هُمْ فِي صَلاتِهِمْ خَاشِعُونَ

Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao,

Baada ya kuhatimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 22 ya Al Hajj, kama nilivyotangulia kusema darsa yetu hii itaanza kutoa tarjumi na maelezo ya Suratul Muuminun ambayo ni ya 23 kwa mpangilio wa sura za Qur'ani ndani ya Mas-haf. Sura hii iliteremshwa Makka na ina jumla ya aya 118. Aya za mwanzo za sura hii zinaelezea sifa za waumini na kisha aya zinazofuatia zinasimulia habari za maisha ya Mitume kama Manabii Nuh, Musa na Issa (AS) na watu wa kaumu zao.

Aya ya kwanza ya Suratul Muuminun inaeleza bayana na kwa uwazi kabisa na kutoa hakikisho kwa kutumia maneno mafupi kwamba bila ya shaka yoyote waumini ni wenye kufaulu na kufuzu duniani na akhera. Kufuzu kuna maana ya kuondoa vizuizi vilivyoko na kuyashinda matatizo ili kuweza kufikia lengo, hali inayomfanya mtu apate ushindi na uokovu.

Kwa kumtegemea Allah SW, waumini hufanya jitihada ukomo wa uwezo wao ili kufikia lengo lililokusudiwa; na kuna ushindi na mafanikio wanayopata hapa duniani kwa kadiri hali na uwezo wa dunia hii ya kimaada inavyoruhusu, lakini thawabu kamili na malipo hasa ya jitihada walizofanya kwa ajili ya Mola wao watakwenda kupata huko akhera ambapo watapata rehma za Allah na kuishi kwenye Pepo ya milele pamoja na waja wema na wateule. Kisha aya zinazofuatia za sura hii zinataja sifa kadhaa zinazowafanya waumini wafuzu na kufaulu, ya kwanza kabisa ikiwa ni khushuu na unyenyekevu wao ndani ya Sala. Mtu anayekuwa na khushuu na unyenyekevu anapokuwa ndani ya Sala, huwa haihisi ibada hiyo tukufu kuwa ni mzigo na taklifu ya ziada aliyowajibishiwa, bali kwake yeye hiyo ni tunu adhimu ya kunong'ona na kufanya mazungumzo na mahabubu wake yenye utamu na raha ya kipekee. Kama tujuavyo waumini wote wanatekeleza ibada ya Sala, lakini sharti la kuweza kufuzu ni kuwa na khushuu na unyenyekevu mtu anapokuwa ndani ya Sala. Kwa sababu Sala inayosaliwa kwa khushuu huondoa uchafu wa kibri na ghururi ndani ya nafsi ya mtu na badala yake kutoa fursa ya kuchanua ndani ya nafsi ya mtu huyo sifa tukufu za ukamilifu wa kiakhlaqi.

Athari ya kuwa mnyenyekevu mbele ya Allah SW hudhihiri na kuonekana hata katika dhahiri ya mwenye kusali; na heshima, adabu na murua wake huonekana wakati anapokuwa ndani ya Sala. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba waumini ndio washindi hasa hapa duniani na huko akhera hata kama hapa duniani makafiri wanaonekana kuwa na anuai za vivutio vya marembo na mapambo ya kimaada.  Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa imani bila ya Sala ina kasoro na walakini; na Sala ya kweli humfanya muumini kuwa mwenye khushuu na unyenyekevu.

Ifuatayo sasa ni aya ya 3 na ya 4 ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ

Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi,

وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ

Na ambao wanatoa Zaka,

Waumini wa kweli si watu wanaotekeleza ibada ya Sala tu pamoja na dhikri na dua. Ni watu wanaowafikiria wanyonge na wahitaji pia katika jamii na wanatoa sehemu ya mali zao na kuwapatia watu hao kwa njia ya Khumsi na Zaka au ya msaada na sadaka.

Kwa kawaida mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu anaitakidi kwamba ulimwengu una lengo na ratiba maalumu, na kwa hivyo huwa hauharibu wakati wake kwa mambo ya lahau na upuuzi. Kwani kuna mambo mengi ya mubaha yaani yanayojuzu kufanya lakini hayana faida yoyote kwa mtu, familia yake wala jamii anayoishi bali ni mambo ya kupoteza wakati tu au kufuja mali na rasilimali. Mtu muumini anatakiwa ajiepushe na kuachana na mambo kama hayo. Aidha kama mtu atakumbana na watu wenye maneno au matendo ya kipuuzi anatakiwa aepuekane nao kwa kujiweka mbali nao au kupishana nao kwa kuchunga murua na heshima yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba maneno na matendo ya muumini yanapasa yawe ya kimantiki na yenye lengo maalumu na yaepukane na kila aina ya lahau na mambo ya kipuuzi. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa kuonyesha uja kwa Mola Muumba na kumwabudu Yeye kusiwe sababu ya kumfanya mtu akate mahusiano na kujiweka mbali na waja wake Mola. Kwa maneno mengine ni kwamba kuwashughulikia na kuwahudumia wanyonge na wahitaji ni sehemu ya imani juu ya Mwenyezi Mungu.

Wapenzi wasikiklizaji, darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 5, ya 6 na ya 7 za sura yetu ya al Muuminun ambazo zinasema:

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ

Na ambao wanazilinda tupu zao,

إِلاَّ عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ

Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa.

فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاء ذَلِكَ فَأُولَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ

Lakini anayetaka kinyume cha hayo, basi hao ndio warukao mipaka.

Baada ya kuonyesha khushuu na unyenyekevu ndani ya Sala, kutoa Zaka na kujiweka mbali na mambo ya lahau na upuuzi, aya hizi tulizosoma zinakuelezea kuzilinda tupu na kujihifadhi na uchafu wa zina kuwa ni moja ya sifa muhimu zaidi anazopaswa kuwa nazo muumini, na kueleza kwamba kuyadhibiti matamanio na kujiweka mbali na kila aina ya ufuska na mahusiano haramu ya kijinsia ni sehemu ya imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu. Watu waumini huwa wanakidhi matamanio yao ya kijinsia kupitia mahusiano sahihi ya ndoa na hujiweka mbali kabisa na njia nyengine zote za mahusiano na maingiliano ya kijinsia, kwa sababu wanajua kwamba kufanya hivyo ni kuchupa mipaka ya fitra na maumbile ya mwanadamu na mafundisho ya dini.

Kinyume na imani ya baadhi ya madhehebu za Kikristo zinazoichukulia ndoa kuwa ni kitu kichukivu na cha kukirihisha na hivyo kutowaruhusu watawa na makasisi wao wafunge ndoa, Qur'ani Tukufu imetoa mwongozo na njia ya wastani na ya kati na kati kuhusiana na kukidhi mahitaji ya kimaumbile na ghariza za kibinadamu. Aya hizi tulizosoma zinasisitiza kwamba ikiwa mtu atakidhi matamanio yake ya kijinsia kwa njia ya ndoa halaumiki kwa hilo na wala hakuna mtu mwenye haki ya kumlaumu na kumkemea. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba moja ya masharti ya imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu ni mtu kulinda na kuchunga tupu yake; na vitendo vyovyote vya ufuska na maingiliano holela ya kijinsia huuchafua moyo na kuidhoofisha imani yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Uislamu ni dini ya wastani wa mambo, haikubali mahusiano na maingiliano holela ya kijinsia, wala haipigi marufuku kikamilifu mahusiano hayo bali inayawekea ruhusa yenye mpaka kupitia njia ya ndoa kati ya mwanamke na mwanamme. Darsa ya 588 ya Qur'ani wapenzi wasikilizaji imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa waumini wa kweli wa imani na matendo kama yalivyoelezwa ndani ya sura hii ya al Muuminun, amin.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)