Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 01 Oktoba 2014 11:48

Sura ya Al Furqan, aya ya 74-77 (Darsa ya 636)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 636 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya aya 74 ambayo inasema:


وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا


Na wale ambao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.
Katika aya tulizosoma kwenye darsa zilizopita Allah SW alitutajia sifa kadhaa za waumini wa kweli. Aya hii tuliyosoma inataja sifa ya kumi na moja ya waja hao kwa kueleza kwamba wao ni watu wanaoipa umuhimu na mazingatio maalumu familia na malezi ya watoto wao, huku wakiamini kwamba wana mas-ulia kwa watu wao hao. Kwa sababu hiyo wanamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awape auni na msaada wake ili waweze kupata kizazi cha watoto safi na wema. Watoto ambao kila watakapokuwa wakiwatazama nyoyo zao zijawe na furaha, na kama watakuwa na majonzi na huzuni nyoyoni mwao basi zifutike na kusahaulika.
Ni kawaida kwamba watoto wa aina hii hulelewa na kukulia kwenye familia ambazo uhusiano baina ya mke na mume hujengeka juu ya misingi ya akhlaqi na upendo wa kiutu, na kila mmoja kati ya baba na mama huwa anatekeleza vizuri na kwa usahihi majukumu na mas-ulia yake kwa mwenzake na kwa watoto wake. Kisha aya inaendelea kutaja sifa nyengine bora ya waja wa kweli wa Allah kwa kueleza kwamba wao si watu wa kutawa, wakajitenga na kujiweka mbali na jamii, bali hushiriki kikamilifu katika harakati za kijamii na kuiongoza jamii yao kuelekea kwenye ustawi na utukukaji wa kimaanawi. Wao hawafikirii fanaka na saada yao wenyewe tu bali wanawatakia mema na saada wenzao pia katika jamii na wanamwomba Mola awape auni na msaada wa kuwawezesha kuwaongoza waumini na kuwa pamoja nao katika kufuata njia iliyonyooka ya uongofu. Watu hao hujipinda na kujitahidi kuzijenga nafsi zao ili waweze kuwa kigezo na mfano wa kuigwa na wenzao katika maisha. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika suala la malezi ya mtoto mbali na kuhitaji sisi wenyewe kuwa na uelewa wa kutosha na kufanya idili, jitihada na juhudi kubwa inatupasa kumwomba Mwenyezi Mungu pia atupe auni na msaada katika jambo hilo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mtoto mwema ni nuru ya macho na kitulizo na kipoza nyoyo cha wazazi; na ni jambo la fahari na kujivunia kwao kuwa na mtoto kama huyo. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa mke na mume wanatakiwa waandae anga na mazingira ya kufurahishana na kuburudishana nyoyo zao; na wakati wanapotizamana watizamane kwa jicho la shauku, raghaba na mahaba. Wa aidha aya hii inatuonyesha kwamba waja safi na wenye ikhlasi wa Allah ndio wanaostahili kushika hatamu za uongozi na uendeshaji jamii ya Kiislamu, si watu wanaopapatikia dunia na wapenda jaha na madaraka.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 75 na 76 ambazo zinasema:


أُوْلَئِكَ يُجْزَوْنَ الْغُرْفَةَ بِمَا صَبَرُوا وَيُلَقَّوْنَ فِيهَا تَحِيَّةً وَسَلامًا


Hao ndio watakaolipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu.


خَالِدِينَ فِيهَا حَسُنَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا


Wadumu humo; ni kituo na makao mazuri kabisa.
Aya hizi zinahatimisha ubainishaji wa sifa kumi na mbili za waja wema na wa kweli wa Allah kwa kuashiria makazi na maskani yao peponi na kueleza kwamba subira na istiqama ya kuvumilia tabu na misukosuko na kusimama imara na kudumu katika kutekeleza wajibu wao na maamrisho ya Mola vimewafanya wastahiki kuingizwa mahali bora kabisa peponi na kulakiwa na watu wa peponi pamoja na kukirimiwa na malaika wa huko. Watu hao wataendelea kuishi maisha yao ya milele huko peponi kwa uhakika na utulivu kamili na wala hawatokuwa na wasiwasi wa kuondokewa na makaazi hayo. Nukta yenye kutoa mguso katika aya hizi ni mkazo iliotilia Qur'ani juu ya subira na istiqama. Japokuwa kabla yake ilishazitaja sifa kumi na mbili za "Ibadur Rahman" yaani waja wa kweli wa Mola Ar Rahman lakini wakati wa kuelezea malipo watakayolipwa waja hao na Mola wao, Qur'ani haitaji wala haitilii mkazo yoyote kati ya sifa hizo bali inaitaja subira tu kuwa ndio sababu ya watu hao kuingia peponi. Yamkini sababu yake ni kwamba ni jambo linalowezekana kwa watu wengi kujipamba kwa sifa mbalimbali njema za ukamilifu, lakini kudumu na kuendelea kuwa nazo sifa hizo mtu katika uhai wake wote ni jambo zito na gumu; na ni wachache tu miongoni mwa watu wanaoliweza na kulimudu jambo hilo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuwa mja wa kweli wa Allah kunahitaji subira na istiqama ya hali ya juu, na bila ya kuwa na azma thabiti haiwezekani kuwa miongoni mwa waja waliojikurubisha kwa Mola. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa miongoni mwa sifa maalumu za jamii ya peponi ni kuwepo hali ya amani, huba na upendo kati ya watu wa jamii hiyo.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 77 ambayo inasema:


قُلْ مَا يَعْبَأُ بِكُمْ رَبِّي لَوْلا دُعَاؤُكُمْ فَقَدْ كَذَّبْتُمْ فَسَوْفَ يَكُونُ لِزَامًا


Sema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe.
Aya hii ambayo pia ndiyo aya ya mwisho ya sura hii ya Al Furqan inagusia uhusiano wa dua na munajati na kupata rehma na fadhila za Allah na kueleza kwamba hakuna kingine kinachoweza kuwanusuru watu kufikwa na adhabu ya duniani na akhera ghairi ya kulilia hali zao na kutubia madhambi yao kwa Mola wao. Tab'an watu wengi wanazikadhibisha aya za Mwenyezi Mungu. Kuna makafiri na washirikina ambao wanaikana haki kwa nyoyo zao na kwa ndimi zao pia; lakini Waislamu, ambao wamemkubali Allah ndani ya nyoyo zao kuwa ndiye Mola wa haki na kulikiri hilo kwa ndimi zao, baadhi ya wakati hufanya mambo yanayokhalifu amri ya Mwenyezi Mungu ambayo ni namna mojawapo ya ukadhibishaji wa kimatendo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba dua na ibada ndivyo vinavyomfanya mja apate rehma na uraufu wa Allah; na maasi na ukadhibishaji ndivyo vinavyomfanya aghadhbikiwe na kufikwa na adhabu ya Mola. Aidha aya hii inatuelimisha kuwa kuacha dua na ibada ni namna mojawapo ya kukadhibisha aya na neema za Mwenyezi Mungu. Wasikilizaji wapenzi darsa yetu ya leo inaishia hapa na ndiyo inayohitimisha tarjumi na maelezo ya sura ya 25 ya Al Furqan. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kufaidika na yale tuliyojifunza katika sura hii na kuyatekeleza kivitendo katika maisha yetu ya kila siku. Wasslamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)