Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Septemba 2014 11:00

Sura ya Al Furqan, aya ya 70-73 (Darsa ya 635)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 635 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 70 na 71 ambazo zinasema:


إِلاَّ مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلا صَالِحًا فَأُولَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا


Isipokuwa atakaye tubia, na akaamini, na akatenda matendo mema, basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.


وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّهِ مَتَابًا


Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia madhambi makuu kama shirki, kuua na kuzini ambazo athari zake mbaya humwandama mtu kuanzia hapa duniani hadi huko akhera. Baada ya kubainishwa hayo aya hizi zinasema: Mwenyezi Mungu SW mwenye huruma na mwingi wa rehma na urehemevu ni mwenye kusamehe hata madhambi hayo pia. Kwa sharti tu kwamba mwenye kutubia madhambi hayo awe ametubia toba ya kweli na kufanya mema na ya kheri ya kufidia maovu na mabaya hayo aliyoyafanya huko nyuma. Yaani aache kumshirikisha Allah na badala yake ashikamane na tauhidi na kumpwekesha Yeye Mola, na kuhakikisha anazirejesha na kuzifidia kwa kadiri hali na uwezo unavyomruhusu haki za watu aliowadhulumu na kuwaendea kinyume. Aya hizi wapenzi wasikilizaji hazizungumzii kusamehewa madhambi tu kutokana na athari ya toba bali zinaeleza pia kwamba toba ya kweli huleta mageuzi na mabadiliko ndani ya nafsi ya mtu kwa kiwango ambacho tabia zote chafu alizokuwa nazo hubadilika na kuwa sifa na tabia njema. Moyo wa shirki na ria hubadilika kuwa wa tauhidi na ikhlasi; kuwadhulumu wanyonge hubadilika kuwa jihadi dhidi ya madhalimu; na maadili safi huchukua nafasi ya ufuska na maadili machafu. Na katika kuwashajiisha na kuwapa moyo zaidi wafanya madhambi, Qur'ani tukufu inasisitiza kwa mara nyengine kuwa ikiwa mtaacha matendo maovu na kuyafidia kwa amali njema na za kheri hakuna shaka yoyote toba zenu zitakubaliwa na mtapata uraufu na rehma za Allah. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Uislamu haufikii kwenye hali ya mkwamo na kugonga mwamba. Walioghariki kwenye madhambi nao pia wamewekewa njia ya kuweza kurudi kwa Mola wao; na kila dhambi inaweza kufidiwa kwa toba na amali njema. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa toba ni mapinduzi na mageuzi ya batini na ndani ya nafsi ya mtu; si harakati ya kijuujuu na ya kimaonyesho inayothibiti kwa kutamka baadhi ya maneno tu. Toba ya kweli ni ile inayofuatanishwa na amali njema. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba toba hubadilisha fikra na matendo ya mtu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 72 ambayo inasema:


وَالَّذِينَ لا يَشْهَدُونَ الزُّورَ وَإِذَا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا


Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao.
Aya hii inataja sifa nyengine ya waja wa kweli wa Allah na kueleza kwamba: miongoni mwa sifa kubwa za watu hao ni kuchunga na kuheshimu haki za wenzao. Wao hawako tayari kwa namna yoyote kutoa ushahidi wa kuthibitisha jambo la batili na wala hawasemi yale yatakayosababisha kupotea haki za watu. Kama ambavyo huwa hawashiriki pia kwenye vikao vya mambo ya batili na wala hawasikilizi maneno ya batili. Kwa sababu kuhudhuria majlisi na vikao vya aina hiyo huwa ni sawa na kuyaunga mkono na kuyaridhia madhambi yafanywayo kwenye vikao hivyo na huo ni mwanzo wa kuchafuka moyo na roho ya mtu. Kisha aya inaendelea kubainisha sifa nyengine maalumu ya waja wema na wa kweli wa Allah kwa kueleza kwamba watu hao si wasemaji wala wafanyaji mambo ya lahau, upuuzi na yasiyo na maana, na wanapokutana na mambo kama hayo hujiepusha na kujiweka mbali nayo kiungwana. Waja hao wa kweli wa Allah ni waungwana na wenye kujiheshimu kiasi kwamba huwa hawaathiriki na kutekwa na mazingira mabaya ya maovu; pamoja na hayo kujiweka mbali kwao na mazingira hayo hukufanya kwa uungwana wa tabia na akhlaqi pasina kuziungulisha na kuzisononesha nyoyo za watu wanaojumuika kwenye mazingira hayo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba haijakatazwa kufanya madhambi tu bali haijuzu pia hata kuangalia madhambi hayo yanapofaywa. Watu waumini wa kweli hujiepusha na vikao vya maasi na madhambi hata kama wao wenyewe hawatofanya maasi endapo watakuwepo kwenye vikao na mijumuiko hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mojawapo ya njia za kukataza maovu ni kumpuuza mtu anayejionyesha katika kufanya madhambi na kuondoka kwenye vikao yanapofanywa madhambi na maasi. Wa aidha aya hii inatuelimisha kwamba waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu huwa na lengo katika maisha, na kwa hiyo hawauharibu umri na uhai wao kwa mambo ya kipuuzi na yasiyo na faida.
Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 73 ambayo inasema:


وَالَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَمْ يَخِرُّوا عَلَيْهَا صُمًّا وَعُمْيَانًا


Na wale ambao wanapokumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi ni viziwi nazo na vipofu.
Miongoni mwa sifa kubwa za waja maalumu wa Allah ni kuwa na uono mpana na wa mbali na maarifa ya mambo. Wao huwa hawalikubali jambo kibubusa; na wakati wanaposoma au kusomewa aya za Mwenyezi Mungu huwa wanatafakari ili kuweza kufahamu madhumuni ya Mola juu ya aya hizo pamoja na kuelewa maana yake ya kina. Waumini hao wenye uwezo mpana wa kutafakari na uono wa mbali wa mambo hawawezi kuchezewa na kughilibiwa na huyu na yule bali huwa wako imara muda wote mithili ya jabali kwa sababu hawayatazami mambo kidhahiri tu au kuyaangalia kijuujuu tu; na kwa hivyo hawaishii kuangalia dhahiri ya aya tu wakakosa kuifahamu batini yake. Kinyume na watu hao ni wale wasiotafakari na kutumia akili zao, ambao hufuata mambo kibubusa tu. Hao ni watu wanaodanganyika na kughilibika kirahisi, wakaikengeuka njia ya haki na kutumbukia kwenye lindi la kufru na upotofu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kutumia akili na kutafakari ndio msingi wa mambo yote ayafanyayo muumini; na Yeye mwenyewe Allah SW ametaka waja wake waifuate dini kwa uelewa, urazini na uono mpana na wa kina. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 635 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake walio waumini wa kweli, ambao imani zao zinathibitishwa na matendo yao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)