Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Septemba 2014 10:52

Sura ya Al Furqan, aya ya 64-69 (Darsa ya 634)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 634 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 64, 65 na 66 ambazo zinasema:


وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا


Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama.


وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا


Na wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ni kali na yenye kuendelea.


إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا


Hakika hiyo ni mbaya kuwa kituo na mahali pa kukaa.

Katika darsa iliyopita tulianza kutaja sifa makhsusi za waja wa kweli wa Allah kwa kuashiria sifa mbili za waja hao. Aya hizi tulizosoma zinaendelea kutaja sifa hizo kwa kueleza kwamba: hao ni watu wanaofanya ibada kwa ikhlasi na kwa mapenzi makubwa. Wakati wa usiku, ambapo watu wote wanakuwa wamelala, huamua kuusamehe usingizi wao mtamu na mnono na kutumia sehemu ya usiku huo kufanya munajati na kumwomba Mola wao kwa hamu na shauku isiyoelezeka. Ni wapi na wapi kati ya waumini hawa na wale wanaojinasibu kwa maneno matupu kuwa wameamini lakini hata Sala tano za faradhi tu wanazisali kivivu na kwa taklifu kubwa?!
Waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu katu hawawi na ghururi kwa sababu ya ibada na amali njema wazifanyazo. Kwani muda wote huwa na hofu ya hisabu ya Allah yenye umakini usio na kifani na humwomba Mola wao Mtukufu kwa unyenyekevu awalinde na awaepushe na adhabu ya moto. Wao wanajua kwa yakini kwamba motoni si mahali pa kuwa maskani ya mtu na hakuna yeyote awezaye kuhimili na kustahamili mateso ya adhabu ya moto. Na ni hiyo hofu ya batini juu ya hisabu na ikabu ndiyo inayowafanya watekeleze sawasawa wajibu na majukumu yao ya kidini kwa kuyashika yaliyoamrishwa na kuyaepuka yaliyokatazwa. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba usiku si wakati wa kulala na kupumzika tu bali pia ni fursa bora kabisa kwa mja kufanya munajati, kuomba na kunong'ona na Mola wake. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa waja wa kweli wa Allah huwa kila mara wanakumbuka Kiyama na kuhofia hali zao zitakavyokuwa huko Akhera. Maisha ya dunia na kushughulishwa na mazonge mbalimbali hakuwaghafilishi na suala hilo muhimu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 67 ambayo inasema:


وَالَّذِينَ إِذَا أَنفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَلِكَ قَوَامًا


Na wale ambao wanapo tumia hawafanyi israfu wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.

Baada ya aya zilizotangulia kutaja sifa za kiakhlaqi na kiibada za waja wa kweli wa Allah aya hii inasema: katika masuala ya kiuchumi, waja hao ni watu wanaofanya mambo kwa kadiri na wastani na wala hawafurutu na kupindukia mipaka katika matumizi. Iwe ni kugharamia matumizi ya kila siku katika maisha kwa kukidhi mahitaji ya familia zao au katika utoaji kwa kuwasaidia wanyonge na wahitaji, si watu wafanya israfu wala wenye kufanya ubakhili, bali hufanya mambo kwa kadiri na wastani. Suala la kuchunga kadiri na wastani hata katika utoaji kuwasaidia wahitaji limezungumziwa pia katika aya nyengine za Qur'ani na limetiliwa mkazo pia katika sira na miongozo ya viongozi wa dini. Kwa mujibu wa hukumu na sheria za Kiislamu haijuzu mtu kuacha wasia wa kugaiwa zaidi ya thuluthi ya mali yake au kutoa mali yake yote kuwagaia watu wengine. Bwana Mtume Muhammad SAW alisema kuhusu mtu aliyekuwa amefanya hivyo kabla ya kufa kwake kwamba: "kama mungekuwa mumenipa habari nisingeruhusu maiti yake izikwe kwenye makaburi ya Waislamu." Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kusisitizwa kusali Sala ya usiku na kufanya ibada nyenginezo hakumaanishi kuwa mtu ajitenge na jamii na kutoshughulishwa nayo, kwa sababu waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu huwa daima wanawafikiria wanyonge kwa kuwakidhia mahitaji yao na kuwatatulia matatizo na shida zao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa haijuzu kufanya israfu hata katika kutoa kuwasaidia wahitaji seuze kufanya israfu na ubadhirifu katika mambo ya batili na yasiyo na faida. Kadhalika aya hii inatuelimisha kwamba waja maalumu wa Allah si watu mabakhili. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kujiepusha na upindukiaji mipaka katika kufanya au kujizuia na jambo katika masuala ya mtu binafsi na ya kijamii ni miongoni mwa masuala muhimu zaidi yanayousiwa na Uislamu.
Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 634 inahatimishwa na aya za 68 na 69 ambazo zinasema:


وَالَّذِينَ لا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَلا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا


Na wale ambao hawamwombi mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapatwa na adhabu kali,


يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا


Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka.


Aya hizi zinaendelea kutaja sifa nyengine makhsusi za waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu zilizoanza kuelezewa katika aya zilizopita na kubainisha kwamba, watu hao hawakiweki kitu au mtu yeyote yule katika daraja sawa na ya Allah, na ni Yeye Mola wa haki tu ndiye wanayemwabudu na kumwomba auni na msaada. Si chochote kati ya mali na kipato cha matajiri, wala nguvu na madaraka ya watawala vinavyoweza kuwavuta na kuwateka watu hao, bali ni kwa Allah pekee wanatawakali na kutegemea. Waja wa kweli wa Mwenyezi Mungu yaani Ibaadur rahman ni wenye kuheshimu uhai na maisha ya mtu na hawafanyi jambo lolote la kuwadhuru na kuwahasiri watu. Hawachukui hatua ya kuidhulumu roho ya mtu ila kama wao wenyewe watadhulumiwa ambapo katika hali hiyo huchukua hatua kukabiliana na dhulma hiyo kwa msingi wa haki na uadilifu. Waja hao wema na wa kweli wa Allah ni wenye kuwaheshimu na kuwastahi maharimu za watu kwa kutotaka kuwakashifu na kuwavunjia heshima, na wanazilinda tupu zao na ufuska na uchafu wa zinaa. Kwani wanajua kwa yakini kwamba kila mwenye kunuka uvundo wa tabia hiyo ovu na chafu ataandamwa na masaibu hapa duniani na huko akhera atapatwa na adhabu kali ya moto. Na kwa kuwa dhambi za shirki, kuua na zinaa, kila moja peke yake ni dhambi kubwa mno, hivyo kama madhambi yote hayo matatu yatakusanyika katika nafsi ya mtu mmoja yatamfanya apatwe na adhabu maradufu na ya milele katika moto wa Jahannamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba muumini anapaswa kudhibiti ghariza na matamanio yake ya kijinsia, kwa sababu kuua na kuzini kunatokana na ghariza za ghadhabu na za shahawa; na ghariza mbili hizi huwa daima zinamsukuma na kumuelekeza mtu kwenye madhambi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa damu ya mtu asiye na hatia inapasa kuheshimiwa kikamilifu, lakini kwa mtu anayemwaga damu za wengine kidhulma au anayehatarisha amani na usalama wa jamii, damu yake huwa haina heshima yoyote. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba uhusiano haramu wa kijinsia umewekwa katika nafasi moja na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumuua mtu asiye na kosa. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba amri ya Qur'ani kuhusu kujiweka mbali na shirki, zinaa na kuua si suala la mawaidha na nasaha tu bali ni sheria ambayo anayeikiuka hupatwa na adhabu kali. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 634 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wa kweli wanaozipamba nafsi zao kwa sifa njema na kuzitakasa na tabia chafu kama zilivyobainishwa ndani ya sura hii ya Al Furqan. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)