Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Septemba 2014 10:46

Sura ya Al Furqan, aya ya 60-63 (Darsa ya 633)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 633 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 25 ya Al Furqan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 60 ambayo inasema:


وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اسْجُدُوا لِلرَّحْمَنِ قَالُوا وَمَا الرَّحْمَنُ أَنَسْجُدُ لِمَا تَأْمُرُنَا وَزَادَهُمْ نُفُورًا


Na wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe? Na huwazidishia chuki.

Washirikina wa Makka walikuwa wakiyasujudia na kuyaabudu masanamu. Bwana Mtume Muhammad SAW akawaambia: kama mnataka kusujudia kitu au mtu sio tu haifai kuvisujudia vitu visivyo na uhai bali hata kuwasujudia wanadamu ambao ni sawa na nyinyi wenyewe. Anayestahiki kuabudiwa ni yule ambaye kwa rehma zake amekuumbeni nyinyi, na daima anakuruzukuni riziki zake na anakuneemesheni kwa neema zake. Hata hivyo badala ya Washirikina kuyakubali maneno hayo ya haki na ya mantiki ya Bwana Mtume wakawa wanajibu kwa jeuri na utovu mkubwa wa adabu kwa kusema: Ni nini huyo Ar Rahmani unayezungumzia? Hatukijui kitu sisi kwa jina hili hata tukiabudu. Na kwa kuwa wewe unatuamrisha sisi tumwabudu yeye basi sisi hatukubali na wala hatuko tayari abadani kufanya hivyo. Naam! Hivyo ndivyo ilivyokuwa; yaani kila Bwana Mtume alipokuwa akiwalingania wamwabudu Mwenyezi Mungu kiburi na ghururi waliyokuwa nayo iliwatia upofu wa kutouona uongofu na kuwafanya wawe mbali zaidi na njia ya haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba sijda ni dhihirisho la kumwabudu Mola mmoja tu wa haki na ni roho ya dini zote za tauhidi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa wale wanaojinasibu kuwa Waislamu lakini wakawa hawasali na hivyo kutomsujudia Mola wao wajue kwamba katika hali hii wako sawa na Washirikina. Wa aidha aya hii inatutaka tuelewe kwamba neno la haki huwa na athari kwa watu walio tayari kuikubali haki, lakini kwa watu wakaidi, wenye inadi na wenye kutakabari hukabiliwa na radiamali hasi na kuwafanya wawe mbali zaidi na haki.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 61 na 62 ambazo zinasema:


تَبَارَكَ الَّذِي جَعَلَ فِي السَّمَاء بُرُوجًا وَجَعَلَ فِيهَا سِرَاجًا وَقَمَرًا مُّنِيرًا


Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara.


وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً لِّمَنْ أَرَادَ أَن يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا


Naye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru.

Aya hizi zinatoa jibu kwa wale waliokuwa wakimwambia Bwana Mtume kwa nini sisi tumwabudu Mungu wako! kwa kuwaambia kwamba: Mwenyezi Mungu hana haja ya sijda zenu na kuabudu kwenu; na wala si kwamba kwa kuasi kwenu na kuipa mgongo kwenu haki, mtakuwa mumemshinda Yeye na kumpunguzia kitu katika adhama Yake ya Uungu. La hasha. Kwa sababu mbingu hizi zenye adhama, zote ziko chini ya mamlaka na utawala wake. Bali hata nyota zisizohesabika pamoja na jua na mwezi. Mola ambaye ni mwenye kumiliki na mwenye kuutawala ulimwengu huu wa maumbile wenye adhama hana haja hata ya nyinyi wenyewe seuze sijda na kuabudu kwenu. Kisha aya zinaendelea kwa kueleza kwamba usiku na mchana ambao nyinyi mnauhisi huko ardhini unatokana na Yeye Mwenyezi Mungu ambaye anavileta viwili hivyo kupitia harakati ya sayari ya dunia kulizunguka jua ili kwa mchana unaokuja kwa kuchomoza jua muweze kujishughulisha na kazi zenu na usiku unaokuja baada ya kuzama kwake muutumie kwa mapumziko. Kama ni hivyo kwa nini basi hamukumbuki na hamuwi washukurivu kwa Mola wenu? Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba uumbwaji wa mbingu zilizojaa nyota pamoja na jua na mwezi ni miongoni mwa madhihirisho ya rehma na baraka za Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa usiku na mchana ni neema zinazostahili ushukurivu mkubwa wa waja kwa Mola wao. Kadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba kuiona na kuijua tu hakika ya jambo na ukweli wake hakutoshi. Watu wanaoweza kuifikia hakika na ukweli hasa ni wale wenye irada na nia ya kweli ya kuijua na kuikubali haki na wakataka kubadilika kwa kujirekebisha; vinginevyo hawawezi kuifikia hakika na ukweli.
Wapenzi wasikilizaji, tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 63 ambayo inasema:


وَعِبَادُ الرَّحْمَنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلامًا


Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa unyenyekevu, na wajinga wakiwasemesha hujibu: Salama!

Kinyume na mwenendo wa kejeli, istihzai, kiburi na kutakabari wa makafiri ambao unawafanya wawe mbali na haki, kuanzia aya hii hadi mwishoni mwa Suratul Furqan, Qur'ani tukufu inataja na kuelezea sifa na tabia za waumini ili kuweza kuonyesha kwa uwazi kabisa tofauti iliyopo baina ya makundi mawili haya katika maneno na matendo yao.
Sifa ya kwanza ya waja wema wa Allah inayobainishwa na Qur'ani ni kujiepusha na kujiweka mbali kwao na tabia chafu ya kiburi, ghururi na kupenda kujikweza ambayo hujidhihirisha katika mlahaka na harakati zote za mtu. Kwani hata katika utembeaji wa mtu unaweza kufahamu kama yeye ni mtu mwenye tawaadhui na unyenyekevu au mwenye ghururi na kiburi. Kwa hivyo Qur'ani inasema: alama ya kwanza ya mja wa kweli wa Allah ni unyenyekevu wake mbele ya waja wa Allah; unyenyekevu na tawaadhui ambayo huonekana pia hata katika harakati na kitendo cha kawaida kabisa kama cha kutembea. Kuhusiana na sifa hii aya ya 37 ya Suratul Israa pia inasema: "Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima." Sifa ya pili ya waja wema na wa kweli wa Allah ni upole na kuwa na subira wanapoambiwa maneno machafu na mabaya. Wakati watu hao wanapokutana na watu watovu wa adabu wasemao maneno machafu na yasiyopendeza, badala ya wao pia kuwajibu watu hao maneno kama hayo hupishana nao kiuungwana na kistaarabu; na badala ya kuzozana na kugombana nao huamiliana nao kwa upole, salama na amani. Baadhi ya mafunzo ya kuzingatiwa katika aya hii ni kwamba kumwamini Allah hakuishii katika ufanyaji ibada za kiroho tu bali kuyapa umuhimu masuala ya kiakhlaqi na kijamii pia ni miongoni mwa nguzo muhimu za imani ya kweli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tawaadhui na unyenyekevu ni matunda ya uja wa kweli na ndio alama ya kwanza ya sifa hiyo. Kadhalika aya hii inatutaka tusiichukulie subira na uvumilivu unaoonyeshwa na waja wema na wa kweli wa Allah mbele ya maneno na vitendo vya utovu wa adabu wanavyofanyiwa na watu kuwa ni alama ya woga na udhaifu bali tujue kuwa hiyo ni alama ya ustaarabu na uungwana wa waja hao. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa tusiwatendee watu majahili sawa na wanayotutendea, kwani kufanya hivyo kutatufanya tuwe sawa na wao. Bali tuwapuuze na kuwaacha kama walivyo. Aidha tuseme maneno mazuri na ya upole katika kukabiliana na lugha isiyofaa wanayotumia dhidi yetu. Darsa ya 633 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wa kweli wanaodhihrisha uja wao kwa maneno yao na vitendo vyao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)